1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Iraq kuwashambulia wanamgambo mjini Fallujah

6 Januari 2014

Waziri Mkuu wa Iraq Nuri al-Maliki amewataka wakaazi wa Fallujah wawatimue magaidi wanaoudhibiti mji huo, na kuuepusha dhidi ya shambulizi la kijeshi. Ameyaamuru majeshi kutoyashambulia maeneo ya makaazi

https://p.dw.com/p/1Alh1
Irak Gefechte Falludscha 4.1.2014
Picha: picture-alliance/dpa

Wanajeshi wa serikali jana walifanya mashambulizi ya kutokea angani katika mji wa Ramadi na kuwauwa wanamgambo 35. Marekani imesema itatoa msaada kwa jeshi la Iraq, lakini imefuta uwezekano wa kulituma tena jeshi lake nchini humo.

Fallujah, ambao ni mji wa magharibi ya Baghadad, ambako wanajeshi wa Marekani walipambana kwa muda mrefu na wanamgambo, sasa hauko tena mikononi mwa serikali. Wapiganaji pia wameyashikilia kwa siku kadhaa maeneo ya mji mkuu wa Mkoa wa Anbar, Ramadi. Mapigano yameendelea mapema leo katika upande wa kaskazini, kaskazini mashariki na Kusini mwa Ramadi.

Kamanda wa jeshi la nchi kavu Jenerali Ali Ghaudan Majeed amesema mji wa Fallujah unapaswa „kusubiri kile kinachokuja“ akimaanisha shambulizi la kijeshi. Mapigano katika mkoa wa Anbar yamesababisha vifo vya watu 200 katika siku tatu pekee.

Waumini Waislamu wa madhehebu ya Sunni katika ji wa Fallujah, Iraq
Waumini Waislamu wa madhehebu ya Sunni katika ji wa Fallujah, IraqPicha: picture-alliance/AP Photo

Maafisa wa serikali katika mkoa wa magharibi wa Anbar walikutana na viongozi wa makabila ili kuwaomba wasaidie kuwafurusha wapiganaji wenye mafungamano na al-Qaeda ambao wametwaa maeneo ya Ramadi na Falluja, ambayo ni miji muhimu ya Iraq kwenye mto wa Euphrates (Frati).

Kundi la al-Qaeda la Taifa la Kiislamu la Irak na Sham– ISIS limekuwa likijiimarisha katika mkoa mzima wa Anbar katika miezi ya karibuni, katika juhudi za kuunda taifa la Waislamu wa madhehebu ya Sunni katika mpaka na Syria.

Lakini hatua ya wiki iliyopita ya kutwaa maeneo ya miji ya Ramadi na Fallujah ilikuwa ni ya kwanza katika miaka mingi ambapo wapiganaji wa Sunni wamejiimarisha katika miji mikuu ya mikoa hiyo na kuidhibiti kwa siku kadhaa. Maafisa wa Ramadi na viongozi wa makabila wamesema watu 35 wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wenye itikadi kali za kiislamu waliuawa katika shambulizi la kutokea angani, ambalo liliyalenga maeneo ya mashariki ya nchi hiyo.

Majeshi ya serikali yanaendelea kupambana na wanamgambo wenye itikadi kali za kiislamu mjini Fallujah
Majeshi ya serikali yanaendelea kupambana na wanamgambo wenye itikadi kali za kiislamu mjini FallujahPicha: picture-alliance/dpa

Mjini Fallujah, kazi ya ISIS ilifanywa kuwa rahisi na watu wa makabila ambao wameungana katika vita dhidi ya serikali. Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani John Kerry amesema kuwa Marekani itayapa msaada majeshi ya Iraq katika vita vyao dhidi ya wapiganaji lakini hivyo vitakuwa ni vita vyao. Amesema Marekani ina wasiwasi mkubwa sana kuhusiana na kuibuka kundi la ISIS lakini haifikirii kurudisha nchini humo jeshi la nchi kavu la Marekani, baada ya kuondoka kwao Desemba 2011.

Iran pia imetangaza kutoa msaada, huku naibu mkuu wa jeshi Jenerali Mohammad Hejazi akisema kama Wairaq wataomba msaada, watawapa vifaa pamoja na ushauri, lakini hawahitaji wapiganaji. Mapigano yalizuka katika eneo la Ramadi mnamo Desemba 30, wakati polisi walipoivunja kambi ya maandamano yaliyodumu kwa mwaka mmoja ambako Waarabu wa Kisunni waliandamana dhidi ya kile walichokiona kuwa serikali inayoongozwa na Washia, kuwatenga na kuilenga jamii ya walio wachache.

Mwandishi. Bruce Amani/AFP

Mhariri: Daniel Gakuba