1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ethiopia katika 'hatua ya mwisho' ya mashambulizi Tigray

Daniel Gakuba
26 Novemba 2020

Wakati waziri mkuu wa Ethiopia akisema jeshi lake limepewa amri ya kuanza ''hatua ya mwisho'' ya mashambulizi dhidi ya mji mkuu wa jimbo lililoasi la Tigray duru zinaarifu kuwa mji huo unalindwa vikali na maelfu ya watu.

https://p.dw.com/p/3lszu
Tigray-Konflikt | Äthiopisches Militär
Picha: Ethiopian News Agency/AP/picture alliance

 

Mazingira katika mji huo mkuu wa jimbo la Tigray, Mekelle uliozingirwa ni ya mvutano mkubwa, kama ilivyoelezwa na mwanadiplomasia mmoja anayeilewa hali ilivyo. Amesema maelfu ya watu wamekusanyika katika viunga vya mji huo, wakichimba mahandaki, huku kila mmoja akijihami kwa bunduki aina ya AK47.

Haya yanafuatia tangazo la waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, kwamba ametoa amri kwa vikosi vyake kuanza kuushambulia mji huo, katika kile alichokiita, ''hatua ya mwisho'' ya mashambulizi dhidi ya viongozi wa chama cha Ukombozi wa Watu wa Tigray, TPLF ambao wanalidhibiti jimbo hilo la kaskazini mwa Ethiopia, baada ya kumalizika muda wa saa 72 aliowapa kuwa wamejisalimisha.

Äthiopien Ministerpräsident Abiy Ahmed Ali
Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy AhmedPicha: Office of the Prime Minister/Reuters

Watetezi wa haki za binadamu waonya kuhusu maafa

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanapiga mbiu, wakitahadharisha juu ya janga linalowakabili raia wa kawaida walionaswa katikati ya uhasama huo wa kijeshi, huku ikiarifiwa kuwa tayari maelfu tayari wameuawa katika mzozo huu ulioanza tarehe nne mwezi huu wa Novemba.

Karibu Waethiopia 43 elfu wamekwishayatoroka mapigano hayo na kukimbilia nchi jirani ya Sudan, ambako wanakabiliwa na uhaba wa mahitaji muhimu.

Afisa mmoja wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi, UNHCR ameiambia DW kwamba ''Watu wanahitaji kila kitu; kuanzia maji, chakula na mahali pa kulala'' na kuongeza kuwa  wanawahudumia kwa chakula watu 90,000 kila siku, kupitia kwa washirika wao, huduma ambayo amesema haitoshi. 

Äthiopien | Menschen fliehen aus der Tigray Region
Waethiopia walioyakimbia mapigano wanakabiliwa na uhaba wa huduma muhimuPicha: Mohamed Nureldin Abdallah/REUTERS

Serikali ya Ethiopia yashutumiwa kuwazuia watu kukimbia

UNHCR inasema idadi ya wakimbizi wanaovuka mpaka kila siku imepungua mnamo siku za hivi karibuni, na wale wachache wanaowasili wanasimulia kuwa wengine wengi wanazuiwa na kulazimishwa kubaki nchini mwao.

Serikali ya mjini Addis Ababa imesema imeanzisha vituo vya msaada katika sehemu za mkoa wa Tigray inazozidhibiti, na kuongeza kuwa msaada huo utaongezeka kutokana na kufunguliwa kwa njia ya kuupeleka.

Akijibu miito ya kimataifa ya kutaka usalama wa raia uheshimiwe katika mzozo huu, waziri mkuu Abiy Ahmed amesema kupitia taarifa, kuwa jeshi la serikali kuu limeweka mkakati wa kuwafikisha mbele ya haki wale aliowaita ''genge la TPLF'' bila kuwadhuru raia na mali zao, turathi za kale za taifa, majengo ya ibada na taasisi za maendeleo.

Wakati huo huo, ujumbe wa Umoja wa Afrika unaowajumuisha marais watatu wa zamani unatarajiwa kufanya mazungumzo na waziri mkuu Abiy mjini Addis Ababa leo, ingawa kiongozi huyo amekataa kata kata usuluhishi wowote kutoka nje ya nchi.

 

rtre, ape