1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

JERUSALEM: Olmert ataka kukutana na viongozi wa kiarabu

30 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCE2

Waziri mkuu wa Israel, Ehud Olmert, amesema yuko tayari kuzungumza na Saudi Arabia na mataifa mengine ya kiarabu yasiyo na msimamo mkali wa kidini ili kuutanzua mzozo baina ya Israel na Palestina.

Waziri Olmert ameyasema hayo baada ya kumalizika mkutano wa viongozi wa kiarabu mjini Riyadh, Saudi Arabia, ulioufufua mpango wa amani wa Mashariki ya Kati. Amesema mkutano wa Saudi Arabia unatoa changamoto kubwa.

´Nadhani makubaliano ya Saudi ni mazuri na yanatoa changamoto kubwa. Yanadhihirisha aina ya jukumu la mfalme Abdalla wa Saudi Arabia na ikiwa nchi zetu zitajaribu kusonga mbele na mchakato wa amani kuzingatia makubaliano ya Saudi, nitayatazama kama maendeleo mazuri sana.´

Olmert anaamini amani baina ya Israel na Palestina huenda ikapatikana katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Mpango wa amani ulioidhinishwa na viongozi wa kiarabu mjini Riyadh unaipa Israel uhusiano wa kawaida na mataifa ya kiarabu ikiwa itaihama ardhi iliyoiteka wakati wa vita vya Mashariki ya Kati vya mwaka wa 1967, kuruhusu kuundwa kwa taifa huru la Wapalestina na kutoa suluhisho la haki kwa Wapalestina waliopoteza makazi yao wakati wa kuundwa kwa taifa la Israel mnamo mwaka wa 1948.