1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jee Kusini mwa Sudan itajitenga?

Miraji Othman5 Novemba 2009

Mustakbali wa Kusini mwa Sudan haujulikani

https://p.dw.com/p/KOyB
Aliyekuwa makamo wa rais wa Sudan, Ali Osman Mohammed Taha(kushoto), akizungumza na na aliyekuwa mkuu wa jeshi la SPLA, marehemu John Garang, baada ya kutiwa saini mkataba wa NaivashaPicha: AP

Mwaka 2005 ulitiwa saini mkataba wa amani wa Naivasha, huko Kenya, uliovikomesha vita virefu kabisa vya kienyeji kuonekana katika Bara la Afrika, vilivokuwa vikiendeshwa na waasi wa Kusini mwa Sudan, kupitia jeshi lao la SPLA, ambalo lilitaka sehemu ya kusini mwa Sudan ijitenge kutoka nchi hiyo. Kiini cha vita hivyo kilitokana na watu wengi wa Kusini mwa Sudan kupinga utawala wa nchi hiyo uliojiketi upande wa kaskazini na kudhibitiwa na watu wenye asili ya Kiarabu.

Mapatano hayo ya amani yaliopelekea sehemu ya Kusini mwa Sudan, inayokaliwa na watu wengi wenye imani ya dini ya kikristo na asili ya Kiafrika, kupewa mamlaka ya utawala wa ndani, makao yake makuu yakiwa mjini Juba, ikiongozwa na wakuu wa zamani wa waasi wa Chama cha Sudan People's Liberation Movement, SPLM. Pia ilitolewa nafasi, ikiwa wananchi watakubali katika kura ya maoni, kwa mkoa wa Kusini mwa Sudan kuwa nchi huru hapo Januari 2011.

Punde baada ya kutiwa saini mapatano ya amani, kuliundwa serekali ya mikoa ya Kusini mwa Sudan, rais wake wa sasa ni Salva Kiir, na pia serekali kuu ya mseto huko Khartoum baina ya chama hicho cha SPLM na kile cha National Congress kinachoongozwa na Rais Hassan al-Bashir. Mapatano ya Naivasha japokuwa yalitoa upenu kwa watu wa Kusini mwa Sudan kujitenga kutoka nchi hiyo, hata hivyo, moyo wa waliotia saini ulisisitiza jhaja ya kuubakisha umoja wa nchi hiyo, kukitolewa ahadi za kuziondoa kero walizokuwa nazo watu wa Kusini mwa Sudan dhidi ya serekali kuu ya Khartoum.

Lakini hali ya wasiwasi kama kweli Sudan itabakia nchi moja baada ya kura ya maoni ya mwaka 2011 inachomoza.

Ismail Mfaule, mwandishi wa habari anayeishi Kairo, nchini Misri, anasema hoja za wenye kutaka kujitenga Kusini mwa Sudan na wale wasiotaka zimejengeka hivi....

Karibuni, mwishoni mwa mwezi uliopita Rais Salva Kiir wa Kusini mwa Sudan aliwahimiza watu wa Kusini mwa Sudan, katika kura ya maoni, wachaguwe eneo lao liwe huru pindi wanataka kuwa huru. Hilo ni takwa ambalo karibu kabisa na kusema kwamba mkoa huo wa kusini ulio na utajiri wa mafuta ujitenge. Kabla ya hapo, kwa hakika tangu kutiwa saini mapatano ya Naivasha Salva Kiir aliushikilia ule msimamo rasmi wa kuunga mkono ubakie Umoja wa Sudan. Salvar Kiir aliuwambie mkusanyiko wa hadharni wa watu katika kanisa mjini Juba kwamba pale watakapofika mbele ya masanduku ya kupigia kura, uamuzi utakuwa ni wao wenyewe, kama wanataka kupiga kura kubakia na Sudan moja, ambapo watakuwa raia wa daraja la pili katika nchi yao wenyewe. Kwa vyovyote, alisema wao, kama viongozi, wataheshimu matukeo ya wananchi.

Matamshi hayo yamezidisha mbinyo katika uhusiano ambao tayari ni mgumu katika ya Chama cha SPLM cha Bwana Kiir na kile cha National Congress, mshirika wake katika serekali kuu ya mseto mjini Khartoum.

Watu wengi wa Kusini mwa Sudan, ambao bado wanavikumbuka kwa uchungu vita virefu vilivojiri Kusini mwa nchi hiyo na wanakasirishwa kutokana na kukosekana maendeleo katika eneo lao tangu pale vita vya kieyneji vilipomalizika, wanachukuliwa sana kwamba wanaunga mkono uhuru. Lakini viongozi wao hadi sasa hawajaenda umbali kusema hadharani kwamba wanataka Kusini mwa Sudan ijitenge. Licha ya Salva Kiir, pia waziri wa mambo ya kigeni wa Sudan, Deng Alor, alisema wiki hii kwamba watu wengi wa Kusini mwa Sudan watachaguwa eneo lao liwe huru ingekuwa kura ya maoni inafanywa sasa. Alisema ni muujiza tu utakaoweza kulifanya chaguo la kuubakisha umoja wa Sudan kuwa la kuvutia kabla ya kupigwa kura ya maoni mwaka 2011. Deng Alor, mpiganaji wa zamani wa jeshi la SPLM, alisema wote wanataka umoja, lakini umoja ulijengeka katika msingi mpya ambap watu wote wa Sudan watakuwa sawa- kama ni Waislamu au Wakristo, au kama ni Waafrika au watu wanaofikiria kwamba wao ni wenye asili ya Kiarabu. Alipoulizwa kama mwaka mmoja unatosha kulifanya chaguo la kubakia na umoja wa Sudan kuwa la kuvutia, alijibu kwamba maisha kuna miujiza.

Uchunguzi uliofanywa na taasisi ya National Democratic ilio na makao yake mjini Washington umegundua miongoni mwa watu iliowauliza huko Kusini mwa Sudan, kwamba wengi wao wanataka mkoa wao ujitenge, kisiasa.

Suala la uhuru kwa Kusini mwa Sudan ni tete sana, hasa katika upande wa kaskazini mwa nchi hiyo. Sehemu kubwa ya akiba ya mafuta ya Sudan yako kusini mwa nchi, huku viwanda vya kusafishia mafuta hayo pamoja na bandari pekee ya kuyasafirisha ng'ambo ziko upande wa kaskazini. Viongozi wa Chama cha National Congress huko Khartoum walisikitihwa na miito hii ya kutaka uhuru kutoka upande wa SPLM, na kusema matamshi hayo yanakwenda kinyume na mkataba jumla wa amani uliotiwa saini Naivasha na uliosema kwamba kipa umbele upewe Umoja wa taifa.

Pia pande mbili hizo, serekali kuu ya Khartoum na ile ya mkoa huko Juba, zinagongana kuhusu kiwango cha asilimia ngapi ya kura ambacho kikifikiwa basi watu wa Kusini mwa Sudan wataweza kujitenga. Chama tawala cha National Congress cha Rais Hassan al-Bashir kinashikilia kwamba angalau thuluthi mbili ya wapig kura waseme wanataka kujitenga na Sudan, ndipo jambo hilo litatekelezwa, wakati Chama cha SPLM kinataka kiwango kiwe baina ya asilimia 50 na 66. Naye mwakilishi wa Marekani juu ya suala la Sudan, Scott Gration, ameziomba pande zote mbili kuachana na misimamo yao na zikubaliane baina ya asilimia 62 na 66. Wananchi wa Sudan wameanza kujiandikisha kupiga kura kwa ajili ya uchaguzi mkuu hapo mwakani na pia kwa ajili ya kura ya maoni mwaka 2011.

Jiografia ya kisiasa itabadilika katika Afrika ya Kati, kwa vile Sudan inapakana na nchi nyingi za eneo hilo, kwa hivyo uhusiano utakuaje pindi Sudan ya Kusini itajitenga...

Na kati ya nchi ilio na wasiwasi na nini kinafanyika nchini Sudan ni Misri. Ismail Mfaume kutoka Kairo anasema:

Mwandishi: Miraji Othman

Mhariri : Mohammed Abdulrahman