1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, Zuma kumuangusha Mbeki kwenye wadhifa mkuu wa ANC?

Mohamed Dahman17 Desemba 2007

Chama tawala nchini Afrika Kusini cha ANC leo kinapiga kura kuchaguwa uongozi wake baada ya kuahirishwa hapo jana uchaguzi ambao unaweza kumsafishia njia naibu wa chama hicho Jacob Zuma kuja kuwa rais wa Afrika Kusini.

https://p.dw.com/p/CcU3
Jacob Zuma Makamo wa Rais wa zamani wa Afrika Kusini na Naibu Rais wa Chama tawala cha ANC.Picha: dpa

Zuma ambaye ni mashuhuri miongoni mwa vyama vya wafanyakazi na wanachama wa kawaida wa chama hicho anatazamiwa sana kunyakuwa wadhifa huo kutoka kwa Rais mtetezi wa chama Thabo Mbeki wakati wanachama 4,000 watakapopiga kura leo hii katika mji wa Polokwane ulioko kilomita 350 kutoka Johannesburg na ambapo matokeo yake pia yanaweza kujulikana leo hii.

Katika kile kinachoonekana kama kujibu mapigo ya kutaka kumn’gowa kweye wadhifa huo Mbeki akizungumza kwenye mkutano mkuu wa chama hicho amemshambulia kwa njia isio wazi mpinzani wake mkuu na naibu wake wa chama Zuma aliekumbwa na kashfa kwa kuwataka wanachama wamchaguwe mtu mwenye maadili.

Mshindi atarithi hatamu za uongozi wa chama ambacho kimetawala taifa hilo lenye nguvu kubwa za kiuchumi barani Afrika bila ya kupingwa tokea kumalizika kwa utawala wa ubaguzi wa rangi hapo mwaka 2004 lakini kilichogawika vibaya kutokana mapambano ya kuwania madaraka ya uongozi.

Wagombea hao wote wawili wenye umri wa miaka 65 maveterani au wakongwe wa mapambano dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi ambao kwa miaka mingi walikuwa wakiishi uhamishoni mapambano yao yamekuja kugeuka kuwa mfarakano mkubwa uliozusha mbinu za kupakana matope,ununuzi wa kura na juhudi za kufanya udanganyifu katika uchaguzi huu.

Kambi ya Mbeki imekuwa ikitowa hoja kwamba Zuma hafai kwa wadhifa huo wa juu wa taifa kutokana na mikingamo yake na sheria.Zuma mwenye kipaji cha kisiasa alionekana kuwa hana hatia hapo mwaka 2006 kwa kumbaka mwanamke mwenye virusi vya HIV ambapo alidai kuwa alifanya naye mapenzi kwa ridhaa yake mwenyewe na polisi hivi sasa inachunguza madai kwamba alikubali hongo katika mkataba wa silaha.Wafuasi wa Mbeki pia wamekuwa wakizusha wasi wasi kwamba Zuma ataitumbukiza nchi hiyo kwenye sera za mrengo wa shoto.

Mbeki ambaye anaungwa mkono na wafanyabiashara na wananchi wa ngazi ya kati nchini Afrika Kusini akihutubia mkutano huo mkuu wa chama hapo jana ameonya kwamba rushwa,matumizi mabaya ya madaraka na mgawanyiko wa ndani ya chama kunatishia kukiangamiza chama hicho.Ametaka wajumbe wasikubali rushwa au chama chao kununuliwa.

Iwapo tumegawika tunapaswa kufanya nini kushughulikia changamoto hii, kwa kuzingatua ukweli ulio wazi chama cha ANC kilichogawika hakiwezi kamwe kutekeleza majukumu yake ya kihistoria kwa umma wa wananchi.

Ingawa Mbeki hakumtaja Zuma hususan kwa jina wakati wa hotuba yake kuu katika mkutano huo mkuu kwenye mji wa Polokwane lakini kulikuwa hakuna shaka kwamba alikuwa amemkusudia nani.Mamia ya wafuasi wa Zuma walizomea wakati wale wa Mbeki walishangilia.

Juu ya kwamba lazima ajiuzulu urais wa Afrika Kusini hapo mwaka 2009 Mbeki anataka kuendelea kukidhibiti chama hicho ili kuhakikisha kwamba anaweza kuongoza bila udhia wakati wa muda wake uliobakia madarakani kadhalika asaidie kumchaguwa na kumuongoza mrithi wake.

Zuma alikuwa makamo wa rais wa Afrika Kusini hadi pale alipotimuliwa na Rais Mbeki hapo mwaka 2005 kwa sababu ya uchunguzi wa rushwa.Wafuasi wake wamewashutumu maafisa waanadamizi wa serikali kwa kutumia asasi za taifa kumchafulia jina shujaa wao na kumnyima wadhifa wa urais.

Zuma mwenyewe anasisitiza kuheshimiwa kwa mchakato wa demokrasia. Amesema: "Hatupaswi kushutumu mchakato wa demokrasia na kujaribu kuipotosha demokrasia.Katika mchakato huo nimeteuliwa kuwania wadhifa wa urais wa chama na nimekubali uteuzi huo."

Zuma pia ameidhinishwa kuwania wadhifa huo na jumuiya za wanawake na vijana za ANC kadhalika chama chenye nguvu kubwa kabisa cha wafanyakazi nchini Afrika Kusini COSATU na hata wanachama wa Chama cha Kikomunisti nchini humo.

Rais mstaafu wa Afrika Kusini Mzee Nelson Mandela hahudhurii mkutano huo na ametuma ujumbe kuelezea masikitiko yake juu ya mgawanyiko ulioko ndani ya chama.