Je Wapalestina kuunganishwa tena na mazungumzo,uchaguzi au mtutu? | Matukio ya Kisiasa | DW | 13.07.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Je Wapalestina kuunganishwa tena na mazungumzo,uchaguzi au mtutu?

Kitendo cha kundi la Hamas kuutwaa Ukanda wa Gaza kwa kutumia nguvu mwezi uliopita kimesababisha kuwepo kwa tawala mbili tafauti za Wapalestina ambazo utengano wao yumkini ukaendelea kudumu kwa muda mkubwa ujao.

Wanamgambo wa kundi la Hamas wakiikanyaga picha ya Rais Mahmoud Abbas wa Wapalestina.

Wanamgambo wa kundi la Hamas wakiikanyaga picha ya Rais Mahmoud Abbas wa Wapalestina.

Maafisa katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi eneo lililo kubwa zaidi na wachambuzi wa mambo wa Kipalestina na Israel wanasita kutabiri kwamba hali hiyo itaweza kudumu kwa muda gani.Sababu kuu yumkini zikawa ni uwezo fulani wa viongozi hasimu kuleta usalama na kuimarisha uchumi pamoja na shinikizo kwa viongozi kuwa na msimamo wa pamoja katika mazungumzo na Israel ya kuanzisha taifa la Palestina.

Kundi la wanamgambo wa Kiislam ambalo kiongozi wake huko Gaza Ismail Haniyeh bado anajihesabu kuwa waziri mkuu wa Wapalestina amesema yuko tayari kuwa na mazungumzo na Rais Mahmoud Abbas kiongozi wa kundi la Fatah ambaye ameiteuwa serikali mpya ya dharura huko Ukingo wa Magharibi chini ya waziri mkuu mpya Salam Fayyad.

Abbas ambaye kuwatimuwa kwake mawaziri wa Hamas hapo Juni nne kumepeleka kukomeshwa uwekaji wa vikwazo vya Israel na mataifa ya magahribi kwa utawala wake anasema atazungumza lakini anayakata masharti ya Haniyeh.Anasisitiza kwamba kamwe hatowasamehe waasi wa Gaza ambao anawashutumu kwa kujaribu kumuuwa.

Wapalestina wengi katika maeneo yote mawili wamefadhaika kwamba utengano huo yumkini ukadhoofisha juhudi za kuanza tena mazungumzo na Israel juu ya kuanzisha taifa huru la Palestina katika Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza.

Makundi yote mawili inaonekana kuwa yamenuia kuwaonyesha Wapalestina kwamba wanaweza kuyaongoza maeneo yao vizuri zaidi kuliko mahasimu wao ushindani ambao kwayo misimamo ya Israel na jumuiya ya kimataifa huenda ikawa na dhima muhimu.

Katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na Israel Fayad amepatiwa mapato ya kodi na ushuru yaliokuwa yakishikiliwa kwa muda mrefu na Israel lakini bado hakuondolewa vituo vya ukaguzi wa kijeshi na vikwazo vyengine dhidi ya nyendo hatua ambazo wakaazi wa eneo hilo wangelizithamini mno.

Huko Gaza Hamas na wakaazi wa eneo hilo wametengwa kabisa.Kumalizika kwa mapigano ya makundi kulikohitimishwa na umwagaji damu hapo mwezi wa Juni wa Hamas kuitwaa Gaza kumeliweka kundi hilo kwenye taswira nzuri kwa wakaazi wengi wa Gaza angalau lwa hivi sasa.

Viongozi wa Hamas wamekuwa wakilalama kwamba vikwazo vya kimataifa vimekuwa haviwapi nafasi kuongoza serikali ambayo imechaguliwa kwa haki miezi 18 uliopita na wanawashutumu baadhi ya viongozi kwenye kundi la Fatah kwa kushirikiana na Israel dhidi yao.

Ahmed Youssef mshauri wa Haniyeh anaona hatua ya Abbas kutangaza serikali ya dharura ni kamari ya kisiasa ambayo itakuja kushindwa na kwamba uamuzi wa busara ni kuzungumza na Hamas.

Juu ya kwamba waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert amesisitiza wiki hii kwamba Israel itakuwa mpumbavu kutoendeleza umoja wa Wapalestina baadhi ya maafisa wa Kipalestina wanaona watu pekee wa kunufaika na utengano huo ni Waisrael.

Wachambuzi wanaona kuna njia mbili zinazoweza kuwaunganisha tena Wapalestina ambazo ni uchaguzi au utumiaji wa nguvu wa kundi moja dhidi ya jengine.

Fursa za kuandaa uchaguzi wa haki mara moja katika maeneo hayo mawili ni finyu na kuna suala iwapo kuna kundi litakalokubali kushindwa.

Baadhi ya watu wanaamini kwamba uingiliaji kati kutoka nje tu ndio utakoweza kuziunganisha pande hizo mbili.

 • Tarehe 13.07.2007
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHAz
 • Tarehe 13.07.2007
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHAz

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com