1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dunia yaadhimisha Siku ya Vizuka

Mohammed Khelef
23 Juni 2017

Leo ni Siku ya Vizuka Duniani, ambayo imewekwa maalum kujenga uwelewa wa jamii juu ya dhuluma iliyofichikana inayowakabili mamilioni ya wanawake ulimwenguni ambao wamefiliwa na waume au wenza wao wa maisha.

https://p.dw.com/p/2fFp8
Sri Lanka Kriegswitwen
Picha: Getty Images/AFP/L. Wanniarachchi

Wengi miongoni mwa wanawake hao wanaripotiwa kuishi maisha ya ufukara na mateso, wengine wakinyang'anywa kila kitu kutoka urithi wa wenza wao wao kimaisha, huku wengine wakiingizwa utumwani na wakwe na mashemegi au mawifi zao, wakituhumiwa kuwa wachawi au kulazimishwa kushiriki matambiko ya kingono.

Hapa tunakuletea baadhi ya mambo yanayohusiana na vizuka,au wajane ambayo huenda ulikuwa huyajuwi:

- Kuna takribani vizuka milioni 258.5 ulimwenguni hivi sasa wakiwa na watoto milioni 584.6.

- Vifo vinavyotokana na mizozo na maradhi vilichangia ongezeko la asilimia tisa ya vizuka katika ya mwaka 2010 na 2015.

- Ongezeko kubwa zaidi liko Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, ambako kunakisiwa kuwako ongezeko la asilimia 24 ya vizuka kati ya mwaka 2010 na 2015, ikichangiwa kwa kiasi fulani na vita vya Syria na nchi nyengine za eneo hilo.

- Mmoja katika kila vizuka saba, yaani vizuka milioni 38, anaishi kwenye ufukara wa kutupwa.

- Katika kila wanawake 10 walio kwenye umri wa kuolewa duniani, mmoja wao ni kizuka, lakini idadi ni kubwa zaidi katika mataifa ya Afghanistan na Ukraine, ambako ni mwanamke mmoja katika kila watano.  

Indien Bildergalerie die Wasserfrauen von Maharashtra
Picha: Reuters/Danish Siddiqui

- India na China ndizo zenye idadi kubwa zaidi ya vizuka, ambapo hadi mwaka 2015 India ilikuwa na vizuka milioni 46, huku China ikiwa na milioni 44.6.

- Katika baadhi ya mataifa ya kusini mwa Jangwa la Sahara, kuna mila ya 'kumsafisha kizuka', ambapo mwanamke huyo hulazimika kunywa maji yaliyokoshewa maiti ya mumewe ama kulala na shemegi yake au mwanamme yeyote mgeni.

- Mara nyingi, vizuka hushukiwa kuwa wamewauwa waume zao ama kwa makusudi au kwa kuwadharau, ikiwemo kuwaambukiza virusi vya Ukimwi, hasa kwenye mataifa ya India, Nepal, Papua New Guinea na nchi za Afrika zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara.

- Kushikilia mali za mume na kuwafukuza vizuka kwenye majumba yao ni jambo mashuhuri katika maeneo mengi ya Angola, Bangladesh, Botswana, India, Ivory Coast, Ghana, Kenya, Malawi, Nigeria, Tanzania na Zimbabwe.

- Kuna wasichana kashaa ambao wamegeuka vizuka kutokana na kuwepo kwa tatizo la ndoa za utotoni kwenye mataifa kadhaa yanayoendelea na pia mila ya kuwaozesha wasichana kwa wanaume vikongwe.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters
Mhariri: Saumu Yussuf