1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je Machar atarudi Juba?

20 Aprili 2016

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lina wasiwasi mkubwa kuhusiana na kushindwa kwa Riek Machar kurejea mjini Juba kwa ajili ya kuchukua wadhifa wa makamu wa rais na kufungua njia ya kuundwa serikali mpya

https://p.dw.com/p/1IYw9
Kiongozi wa waasi Riek Machar
Kiongozi wa waasi Riek MacharPicha: Reuters/T. Negeri

Wanaofuatilia hali ya kisiasa katika taifa hilo jipya kabisa duniani wanasema hatua hiyo inayaweka pabaya makubaliano ya amani.

Kiongozi huyo wa waasi Sudan Kusini Riek Machar alitarajiwa kuwasili Jumatatu mjini Juba kukabidhiwa rasmi wadhifa wake wa zamani wa makamu wa rais na kujiunga na utawala wa rais Salva Kiir kama ilivyoafikiwa katika makubaliano ya amani ya mwezi Agosti mwaka jana yaliyotiwa saini na pande zote mbili. Hata hivyo hadi kufikia wakati huu Machar hajawasili mjini mkuu juba na badala yake msemaji wake William Ezekiel ameeleza.

Viongozi wawili wa Sudan Kusini wakikubaliana juu ya kusitisha vita 01.02.2014 Addis Ababa
Viongozi wawili wa Sudan Kusini wakikubaliana juu ya kusitisha vita 01.02.2014 Addis AbabaPicha: Reuters/T. Negeri

''Tunataka kuwaarifu kwamba Dr Riek Machar makamu wa kwanza wa rais mtarajiwa ambaye anatakiwa kuwasili hatowasili leo mpaka itakapotangazwa tena sababu bila shaka inahusiana na mipangilio ya usafiri. Ndege iliyotakiwa kumbeba mkuu wa majeshi ya SPLA katika chama cha SPLM upinzani jenerali Simon Garwich haijapewa idhini ya kutumia anga ya Sudan Kusini''

Ni kauli hii na kutowasili kwa Machar ndiko kulikoutia wasiwasi Umoja wa Mataifa.Mkuu anayehusika na masuala ya amani katika Umoja huo Herve Ladsous ameliarifu juu ya hali ya Sudan Kusini baraza la usalama la Umoja huo lenye wanachama 15 kufuatia ombi la Marekani,kwamba hali iliyopo nchini humo inatia wasiwasi.

China ambayo kwa mwezi huu wa Aprili ndiyo inayoshikilia uwenyekiti wa baraza hilo la Usalama la Umoja wa Mataifa,kupitia naibu balozi wake katika Umoja huo Wu Haitao imesema wanachama wa baraza hilo wamesisitiza utayarifu wao wa kushughulikia hatua yoyote itakayojitokeza ya kutatiza utekelezaji wa makubaliano ya amani ya Sudan Kusini.

Salva Kiir alipokutana na Jakaya Kikwete rais wa Zamani wa Tanzania na Riek Machar,Oktoba ,2014
Salva Kiir alipokutana na Jakaya Kikwete rais wa Zamani wa Tanzania na Riek Machar,Oktoba ,2014Picha: AFP/Getty Images

Kwa mujibu wa balozi wa Urusi ndani ya Umoja huo, Peter Llichev alichokibaini Ladsous ni kwamba kuna hali ya kutoaminiana kwa kiasi kikubwa kati ya pande hizo mbili ingawa mjumbe huyo wa amani ameelezea pia matumaini kwamba Machar huenda akawasili Jumatano mjini Juba.

Maelfu ya wasudan Kusini waliuwawa na zaidi ya milioni 2 katika nchi ya watu milioni 11 wameachwa bila makaazi kwa kipindi cha zaidi ya miaka miwili ya mapigano yaliyozuka mwishoni mwa mwaka 2013, ikiwa ni chini ya miaka miwili baada ya taifa hilo kujipatia uhuru wake. Mzozo huo ulitokana na kutimuliwa kwa Machar serikalini na rais Kiir na kuzua vita ambavyo viligeuka kuwa vya kikabila kati ya Dinka kabila la rais Kiir dhidi ya Nuer kabila la Machar.

Mwandishi: Saumu Mwasimba

Mhariri: Grace Patricia Kabogo