1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je kutatangazwa Hali ya Hatari Pakistan?

P.Martin9 Agosti 2007

Kinyume na ripoti za vyombo vya habari vya Pakistan,Rais Pervez Musharraf wa Pakistan hatotangaza hali ya hatari,bali angependa uchaguzi ufanywe kama ulivyopangwa hapo mwakani.

https://p.dw.com/p/CH9o

Hapo awali stesheni binafsi za televisheni na magazeti nchini Pakistan,yaliripoti kuwa Rais Pervez Musharraf yutayari kuchukua hatua itakayoweza kuchelewesha uchaguzi uliopangwa kufanywa mwakani na hatua hiyo,huenda ikazuia haki ya kufanya mikutano na kubana vyombo vya habari.

Hata Naibu-Waziri wa Habari wa Pakistan,Tariq Azim Khan alisema,hatua ya kutangaza hali ya hatari inaweza kuhalalishwa kutokana na hali inayokutikana hivi sasa katika Wilaya ya Kaskazini-Magharibi pamoja na yale matamshi ya wanasiasa wa Kimarekani kuwa Washington iwe tayari kushambulia vituo vya Al-Qaeda au Taliban ndani ya Pakistan,ikiwa itapata habari za upelelezi,zitakazowezesha mashambulizi hayo.

Lakini Waziri wa Habari wa Pakistan,Mohammad Ali Durrani amekanusha ripoti hizo akisema,rais Musharraf anaamini kuwa hivi sasa hakuna haja ya kutangaza hali ya hatari.

Hata hivyo,wachambuzi na viongozi wa upande wa upinzani wana hofu kuwa Musharraf huenda akatumia mamlaka ya dharura,kukwepa matatizo ya kikatiba yanayomkabili nyumbani.Kwani Musharraf angependa kuchaguliwa tena kati ya Septemba na Oktoba,kabla ya mabunge ya mikoa na la taifa,kuvunjwa kwa matayarisho ya chaguzi za bunge zilizopangwa kufanywa mwezi wa Desemba au Januari ijayo.

Ukweli wa mambo ni kuwa muungano wa vyama tawala ndio utakoapata hasara ikiwa kutafanywa uchaguzi. Hata Musharraf binafsi,amepoteza umaarufu wake, tangu alipojaribu kumfukuza kazi,jaji mkuu wa nchi hiyo bila ya kufanikiwa.

Akikabiliwa na hali hiyo,Rais Musharraf hii leo,kinyume na ilivyopangwa hapo awali,aliamua kutokwenda Afghanistan kushiriki katika mkutano wa Baraza la Amani au Jirga mjini Kabul.Musharraf alimuarifu Rais Karzai kuwa shughuli za nyumbani zinamzuia kuhudhuria mkutano huo na badala yake, amemtuma Waziri Mkuu Shaukat Aziz kuongoza ujumbe wa Pakistan.

Azma ya mkutano huo wa siku nne,ni kutafuta njia za kukomesha mashambulizi kwenye mpaka wa Afghanistan na Pakistan pamoja na kuimarisha usalama katika nchi hizo mbili.Rais Hamid Karzai wa Afghanistan,alipofungua mkutano huo leo hii alisema:

“Vipi tunaweza kupambana na Taliban?Hilo ni suala kuu linalohitaji kupatiwa jawabu hivi sasa.“

Mkutano wa Kabul unahudhuriwa na zaidi ya viongozi 600 wa makundi ya kikabila kutoka Afghanistan na Pakistan,kuzungumza matatizo ya usalama kwenye maeneo ya mpakani,ambako wanamgambo wa Kitaliban wameimarisha mashambulizi yao.Vile vile kuna hofu kuwa wanamgambo wa Al-Qaeda wamejikusanya upya katika eneo hilo.