1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika Magazeti ya Ujerumani Wiki hii

Oumilkheir Hamidou
6 Januari 2017

Matumaini ya amani katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo, na vitisho nchini Gambia baada ya Yahya Jammeh kukataa kung'atuka ni miongoni mwa mada katika magazeti ya Ujerumani kuhusu bara la Afrika wiki hii.

https://p.dw.com/p/2VOf2
Kongo tödliche Proteste gegen Kabila
Picha: Getty Images/AFP/E. Soteras

Matumaini ya kupatikana amani katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo, na vitisho nchini Gambia baada ya Yahya Jammeh kukataa kung'atuka madarakani licha ya kushindwa katika uchaguzi wa rais ni miongoni mwa mada zilizochamabuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani kuhusu bara la Afrika wiki hii.

Tunaanzia jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo."Matumaini mema ", ndio kichwa cha maneno cha ripoti ya gazeti la "Süddeutsche" linalozungumzia makubaliano yaliyofikiwa kati ya  serikali na upande wa upinzani makubaliano yanayofungua njia kwa rais Joseph Kabila kukabidhi madaraka. Baada ya kuzungumzia kuhusu  maandamano na machafuko ya miezi kadhaa ya umwagaji damu, gazeti hilo la mjini Munich, limemnukuu mwenyekiti wa tume ya upatanishi toka kanisa katoliki, askofu mkuu wa Kisangani Marcel Utembi akitangaza usiku wa kuamkia mwaka mpya, makubaliano yaliyofikiwa na yanayofungua njia  ya kumalizika mzozo. Kuambatana na makubaliano hayo, uchaguzi utabidi uitishwe kabla ya mwaka huu kumalizika. Hata hivyo rais Joseph Kabila hatoruhusiwa kuwania. Na haruhusiwi pia kuifanyia marekebisho yoyote katiba  katika kipindi hicho, kwa lengo la kusaka njia ya kugombea tena wadhifa huo.

Kiu cha madaraka kinaweza kuhatarisha makubaliano yaliyofikiwa

"Makubaliano ya kukabidhi madaraka katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo" yamechambuliwa pia na mhariri wa gazeti mashuhuri la Frankfurter Allgemeine linalozungumzia pia kuhusu kung'atuka madarakani rais Kabila hadi ifikapo mwisho wa mwaka huu, kuundwa serikali ya mpito na kuitishwa uchaguzi nchini humo. Frankfurter Allgemeine linakumbusha jinsi Joseph Kabila alivyoingia madarakani mwaka 2001 baada ya babaake kuuliwa pamoja na jinsi alivyoibuka na ushindi uchaguzi wa kwanza huru ulipoitishwa mwaka 2006. Zoezi la kuhesabiwa kura, uchaguzi mwengine ulipoitishwa mwaka 2011 limepita katika hali ya vurugu kwa namna ambayo hakuna anaeweza kusema kwa uhakika kama Joseph Kabila alishinda au la.

Tangu wakati huo malalamiko na hasira miongoni mwa wananchi zikaanza kuenea na mbinu za rais kutaka kung'ang'ania madaraka zikazusha hofu ya kuripuka vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo. Licha ya ahadi zilizotolewa na Kabila za kutogombea mhula wa tatu, Frankfurter Allgemeine linamalizia kwa kuelezea hofu za wananchi pengine asizitekeleze kutokana na kiu cha kupenda madaraka cha wale wanaomzunguka na hasa mkewe na nduguye wa kike ambae  yeye nae ni mapacha.

Hali inatisha pia Gambia

Lilikua gazeti hilo hilo la mjini Frankfurt lililoichambua hali nchini Gambia na vitisho vilivyoenea baada ya rais wa nchi hiyo ndogo ya Afrika Magharibi,Yahya Jammeh kusema hatong'atuka madarakani, january 19 inayokuja  licha ya kushindwa katika uchaguzi mkuu desemba mosi iliyopita. Nchi jirani ya Senegal inatishia kutuma wanajeshi linaandika gazeti la Frankfurter Allgemeine. Miito ya jumuia ya kimataifa na hasa jumuia ya ushirikiano wa kiuchumi wa nchi za Afrika Magharibi -ECOWAS kumtaka akabidhi madaraka kwa amani january 19 itakapowadia, anaitajata Jammeh kuwa ni "tangazo la vita" na tangu wakati huo anakataa kuzungumza na wawakilishi wa ECOWAS.

Frankfurter Allgemeine linahisi Jammeh anabidi azingatie onyo la Senegal, na kukumbusha mvutano katika jimbo la kusini mwa Senegal la Casamance ambako tangu mwaka 1984 waasi wanapigania uhuru, ungekuwa umeshamalizika pindi waasi hao wangekuwa hawapatiwi hifadhi nchini Gambia. Frankfurter Allgemeine linamaliza kwa kutahadharisha Ubishi wa Jammeh usije ukampatia sababu rais Macky Sall wa Senegal ya kuiingiza madarakani serikali inayoelemea upande wake. Maoni kama hayo yameelezewa pia na gazeti la die Tageszeitung la mjini Berlin linalozungumzia vitisho vinavyoendelea Gambnia na kufikia hadi  vituo vya radio kufungwa na mwenyekiti wa tume ya uchaguzi kukimbilia Senegal.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir

Mhariri: Iddi ssessanga