1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jamhuri ya Afrika Ya kati kuendelea na uchaguzi, licha ya mapigano

Admin.WagnerD21 Desemba 2013

Viongozi wa serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati wanadhamiria kuendelea na taratibu za uchaguzi licha ya mapigano yaliyozuka yaliyosababisha vifo vya maelfu ya watu huku wengine wakiwa wakimbizi wa ndani

https://p.dw.com/p/1Adsw
Wakimbizi wa ndani Afrika ya kati,kwenye kambi karibu na uwanja wa ndege wa Bangui
Wakimbizi wa ndani Afrika ya kati,kwenye kambi karibu na uwanja wa ndege wa BanguiPicha: Sia Kambou/AFP/Getty Images

Viongozi wa serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati wameazimia kuendelea na taratibu za uchaguzi licha ya machafuko yaliyozuka na kusababisha vifo vya maelfu ya watu huku wengine wakiwa ukimbizini. Msimamo huu unakuja baada ya ujumbe maalumu wa Marekani kuitembelea nchi hiyo jana, na kutoa wito wa sheria kuchukua mkondo wake kwa waliosababisha mauaji nchini humo.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Samantha Power, katika ziara yake ya siku moja mjini Bangui, ambapo alitembelea hospitali na makanisa na kukutana na viongozi wa ngazi ya juu serikalini, amesema ni jambo la msingi kwa serikali ya muda kuheshimu ratiba ya uchaguzi, na baadaye kuondoka.

Huku ikiwa imekabiliwa na shinikizo la kimataifa, serikali ya mpito inayoongozwa na Michel Djotodia, imeahidi kwamba matayarisho ya uchaguzi yanaendelea kama ilivyopagwa.

Waziri Mkuu Nicolas Tiangaye amesema kwamba wajumbe wa tume ya uchaguzi wataapishwa wiki ijayo. "Wajumbe hao watakuwa na jukumu la matayarisho na uendeshaji wa uchaguzi, ambao utafanyika mwaka 2014.

Wananchi wa Afrika ya kati kaskazini mwa mji wa Bangui
Wananchi wa Afrika ya kati kaskazini mwa mji wa BanguiPicha: Sia Kambou/AFP/Getty Images

Djotodia, aliwekwa kama rais wa muda chini ya mkataba maalumu ulioafikiwa na mataifa ya Afrika lakini kwa sasa anaonekana kuzidiwa nguvu na kushindwa kwake kuzuia umwagikaji damu ambao unaendelea. Kiasi cha watu laki sita wamegeuka kuwa wakimbizi wa ndani, na jumuiya ya kimataifa imeonya kujirudia historia ya mauaji ya maangamizi kama ilivyotokea Rwanda mwaka 1994.

Hata hivyo, kupelekwa kwa askari wa Kifaransa chini ya idhini ya Umoja wa Mataifa mapema mwezi huu kumerejesha amani kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Bangui, ingawaje bado mashambulizi ya kulipiziana kisasi yanaendelea hapa na pale.

Kikosi cha kimataifa kwa ajili ya Jamhuri ya Afrika ya kati, katika mitaa ya mji wa Bangui
Kikosi cha kimataifa kwa ajili ya Jamhuri ya Afrika ya kati, katika mitaa ya mji wa BanguiPicha: Fred Dufour/AFP/Getty Images

Kutokana na makubaliano kati yake na mataifa ya Afrika, Rais Djotodia anaendelea kuwepo madarakani mpaka mwaka 2015. Mwenyewe Djotodia alikuwa mkuu wa muungano wa Seleka uliomuondoa madarakani Rais Francois Bozize mapema mwaka huu, lakini jumuiya ya kimataifa inamuona sasa hana uwezo tena wa kuhimili machafuko ambayo yanachukuwa sura ya mgogoro wa kidini kati ya Waislamu na Wakristo.

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya nje wa Rwanda, Louise Mushikiwabo, amesema serikali yake inatuma askari wake huko Jamhuri ya Kati, ili kujiunga na jeshi la kulinda amani la Umoja wa Afrika.

Mwandishi: Diana Kago/REUTERS/AFP
Mhariri: Mohamed Khelef