1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

James Rodriguez aiangamiza Uruguay

29 Juni 2014

Colombia wamewabandua nje Uruguay ili kufuzu katika robo fainali. Bila Luis Suarez, safu ya mashambulizi ya Colombia bila shaka ingekuwa ni mlima mkubwa kwa vijana wa kocha Oscar Tabarez.

https://p.dw.com/p/1CSB6
WM 2014 Achtelfinale Kolumbien Uruguay
Picha: Reuters

James Rodriguez alifunga goli moja katika kila kipindi jana usiku na kuwapa Colombia ushindi wa magoli mawili kwa sifuri dhidi ya Uruguay. Vijana hao wa kocha Jose Pekerman waliendeleza matokeo yao bora, kwa kusajili ushindi wa nne mfululizo katika Kombe la Dunia.

Luis Suarez aliungwa mkono na mashabiki wengi sana katika uwanja wa Estadio Maracana mjini Rio de Janeiro. Mshambulizi huyo alilazimika kuangalia mchuano huo kutoka nyumbani kwao Uruguay, baada ya kitendi cha kumng'ata mchezaji wa Italia kumsababishia adhabu ya kumfungia kucheza mechi tisa na pia kutojihusisha na shughuli zozote za kandanda kwa kipindi cha miezi minne.

WM 2014 Achtelfinale Kolumbien Uruguay
Edinson Cavani aliachwa peke yake kuongoza mashambulizi ya Uruguay, bila mafanikioPicha: Reuters

Uruguay walitaraji kuweka kando kashfa hiyo iliyoangaziwa mno na vyombo vy ahabari, huku Diego Forlan mwenye umri wa miaka 35 akivaa viatu vya Suarez. Lakini kama tu ilivyokuwa safu ya mashambulizi ya Uruguay, isipokuwa Edinson Cavani, gwiji huyo alishindwa kufanya lolote la maana katika mchuano huo.

Colombia walianza mchuano kwa mashambulizi makali, huku Juan Caudrado, Teo Gutierrez, Jackson Martinez na Rodriguez wakishirikiana vyema kumfanyika kazi kubwa kipa wa Uruguay Fernando Muslera. Cavani pekee ndiye aliyejaribu kusababisha usumbufu kwa safu ya ulinzi ya Colombia, lakini alikosa yale makali ya kusonga mbele ambayo Suarez huwa anayaonyesha.

Rodriguez aliiweka Colombia kifua mbele kwa kufunga bao safi sana muda mfupi kabla ya kukamilika nusu saa. Aliipokea pasi na kuituliza kifuani nje ya kijisanduku, akageuka na kuvurumisha shuti kali kuelekea langoni. Shuti yake ililenga wavuni baada ya kuugonga mlingoti. Lilikuwa goli maridadi kutoka kwa chipukizi ambaye anawania nafasi ya kuwa mchezaji bora wa dimba hili kufikia sasa.

Dakika tano baadaye baada ya kuanza kipindi cha pili, Rodriguez alibusu wavu tena. Beki wa kushoto Pablo Armero alikimbia kuelekea mbele pembeni mwa uwanjan, akasukuma mpira kuingia kwenye eneo la hatari. Caudrado akafanya kazi nzuri kuupiga kichwa karibu na lango, ambako Rodriguez alikuwa tayari kumalizia.

Magoli mawili kwa sifuri bila shaka yaliuuwa kabisa mchezo huo. Kocha Tabarez akamwondoa uwanjani Forlan, Alvaro Pereira na baada ya Alvaro Gonzalez, ili kuwaleta washambuliaji Christian Stuani, Gaston Ramirez na Abel Hernandez lakini tayari jahatzi lilikuwa limezama.

Mwandishi: Bruce Amani/DW/DPA/AFP
Mhariri: Sekione Kitojo