1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yakiri ilikuwa kosa kutangaza ujenzi mpya wa makaazi ya Wayahudi

11 Machi 2010

<p>Matumaini ya kuwa na majadiliano yasio ya moja kwa moja yanafifia,baada ya Wapalestina kusema hawatofanya majadiliano hayo mpaka mpango wa kujenga nyumba za Wayahudi katika Jerusalem ya Mashariki utakapofutwa.

https://p.dw.com/p/MPYu
U.S. Vice President Joseph Biden, left, talks with Palestinian President Mahmoud Abbas ahead of their meeting in the West Bank city of Ramallah, Wednesday, March 10, 2010. Israel's new plan to build 1,600 homes for Jews in Palestinian-claimed east Jerusalem overshadowed Vice President Joe Biden's visit to the West Bank on Wednesday. Biden was to hold talks with Palestinian President Mahmoud Abbas and Prime Minister Salam Fayyad, in part to ease their doubts about the latest U.S. peace efforts. (AP Photo/Tara Todras-Whitehill)
Makamu wa Rais wa Marekani,Joe Biden(kushoto) pamoja na Rais wa Wapalestina Mahmoud Abbas.Picha: AP

Wapalestina wametamka hayo baada ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu hapo awali kuamua hivyo hivyo. Wakati huo huo Israel inazidi kushinikizwa na jumuiya ya kimataifa kuhusu mradi wa ujenzi wa makaazi ya Wayahudi uliotangazwa wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani Joe Biden katika Mashariki ya Kati, katika jitahada ya kufufua majadiliano ya amani kati ya Israel na Wapalestina. Biden alisema:

"Ni muhimu kwa pande zote mbili kuhakikisha kuwa kuna mazingira yatakayosaidia majadiliano kufanyika na sio kukorofisha."

Israel ikizidi kushinikizwa na jumuiya ya kimataifa, hii leo imesema ilikuwa kosa kutangaza mpango wa kujenga nyumba 1,600 katika Jerusalem ya Mashariki wakati wa ziara ya Biden. Afisa wa ngazi ya juu amesema, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alikuwa na mazungumzo marefu pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani Eli Yishai kuhusu tangazo hilo.

Biden alitarajia kuwa ziara yake ingesaidia kuzidisha uwezekano wa kufanywa majadiliano yasio ya moja kwa moja. Badala yake,amejikuta akishughulika na mvutano mpya uliosababishwa na tangazo la Israel.Hiyo jana Biden mara nyingine tena alieleza fikra zake waziwazi alipozungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari pamoja na Rais wa Wapalestina Mahmoud Abbas,katika mji wa Ramallah ulio katika Ukingo wa Magharibi.

Nae Rais Abbas alisema, tangazo hili la Israel pamoja na uamuzi uliopitishwa hapo awali kujenga nyumba 112 kwa ajili ya walowezi wa Kiyahudi katika Ukingo wa Magharibi, unadhoofisha imani na ni pigo kubwa kwa jitihada zilizofanywa miezi iliyopita kuanzisha majadiliano yasiyo ya moja kwa moja. Amesema, haitoshi kulaani tu mpango huo wa Israel bali unapaswa kuzuiliwa. Wapalestina wanaiangalia Jerusalem ya Mashariki kama mji mkuu wa taifa la siku za mbele la Palestina.

European Commissioner designate for the position of High Representative for Foreign Policy Catherine Ashton speaks during a hearing at the European Parliament in Brussels on Monday Jan. 11, 2010. Catherine Ashton, the 53-year-old former European Union trade commissioner and leader of Britain's House of Lords, was expected to face intensive questioning at the European Commission confirmation hearings, which began in Brussels on Monday. (AP Photo/Virginia Mayo)
Mkuu wa sera za nje za Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton.Picha: AP

Wakati huo huo Umoja wa Ulaya imelaani uamuzi wa Israel. Katika taarifa iliyotolewa na mkuu wa sera za nje za Umoja wa Ulaya Catherine Ashton amesema, Umoja wa Ulaya unasisitiza kuwa kuambatana na sheria ya kimataifa, makaazi hayo si halali. Hata nchi moja moja za Umoja wa Ulaya zimeshambulia msimamo wa Israel. Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza David Milliband amesema huo ni uamuzi mbaya uliopitishwa wakati usio muwafaka. Uamuzi huo, amesema, utawapa nguvu wale wanaoshikilia kuwa Israel haitii maanani suala la amani.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imeeleza waziwazi kuwa tangazo la Israel halitopuuzwa. Mjumbe maalum wa Marekani katika Mashariki ya Kati, George Mitchell atalishughulikia suala hilo atakaporejea katika kanda hiyo wiki ijayo. Siku ya Jumatatu Mitchell alifanikiwa kupata makubaliano ya kuanzishwa majadiliano yasiyo ya moja kwa moja. Duru ya mwisho ya mazungumzo ya ana kwa ana yalivunjika Desemba mwaka 2008 kufuatia mashambulio yaliyofanywa na Israel katika Ukanda wa Gaza unaodhibitiwa na Hamas.

Muandishi: Martin,Prema/DPA/AFPE

Mhariri: Josephat Charo