1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yafunga vituo vya mpakani eneo la Gaza

19 Januari 2008
https://p.dw.com/p/Cupg

GAZA: Licha ya lawama kali za kimataifa,Israel imeimarisha hatua zake dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.Wizara ya Ulinzi ya Israel imetoa amri ya kufunga njia zote za mpakani zinazotumiwa kuingia eneo la Gaza linalodhibitiwa na Hamas tangu katikati ya mwaka uliopita.Hata misaada ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Wapalestina wanaoishi katika Ukanda wa Gaza haiwezi kupitishwa.Kiasi ya watu milioni moja na nusu huishi katika eneo hilo.

Christopher Gunness alie msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wakimbizi(UNRWA)amesema,eneo zima la Gaza limefungwa. Hakuna njia ya kupitisha misaada ya kiutu na hata wasaidizi hawana uwezo wa kuingia au kutoka eneo hilo.Kwa maoni yake,hali ya wanadamu itazidi kuwa mbaya kuliko ilivyo hivi sasa.Mkuu wa Umoja wa Nchi za Kiarabu,Amr Mussa vile vile amelaani vikali mashambulizi ya majeshi ya Israel katika eneo la Gaza pamoja na hatua ya kufunga vituo vyote vya mpakani kati ya Gaza na Israel.