1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaendelea kushambulia Gaza

2 Agosti 2014

Israel imeushambulia kwa mabomu mji wa kusini wa Gaza wa Rafah siku ya Jumamosi, wakati huku vikosi vyake vikimtafuta mwanajeshi wake wanayeamini kuwa ametekwa nyara na Hamas.

https://p.dw.com/p/1Cnv3
Wanajeshi wa Israel wakielekea Ukanda wa Gaza.(02.08.2014)
Wanajeshi wa Israel wakielekea Ukanda wa Gaza.(02.08.2014)Picha: Reuters

Jeshi la Israel limesema linaamini mwanajeshi huyo ametekwa na Hamas wakati wa shambulio lililotokea kama saa moja baada ya kuanza kwa usitishaji wa mapigano kwa misingi ya utu uliofikiwa kutokana na juhudi za kimataifa hapo Ijuma asubuhi.

Kitengo cha kijeshi cha Hamas leo kimejitenganisha na madai ya kuhusika na kutekwa nyara kwa mwanajeshi hiyo jambo lililosababisha shutuma kubwa za kimataifa. Rais Barack Obama wa Marekani na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon pamoja watu wengineo wameishutumu Hamas kwa kukiuka usitishaji huo wa mapigano na wametaka kuachiwa mara moja na bila ya masharti kwa mwanajeshi huyo wa Israel.

Maafa yaongezeka

Takribani Wapalestina 35 wameuwawa kutokana na mashambulizi ya mizinga na mabomu kwenye na karibu na mji wa Rafah mapema leo hii ambayo yameuwa zaidi ya watu 100 tokea kuvunjika kwa makubaliano ya kusitisha mapigano.Wapalestina wameripoti kuwepo kwa zaidi ya mashambulizi ya anga 150 mengine yakielekezwa dhidi ya misikiti na kwenye Chuo Kikuu cha Kiislamu mjini Gaza chenye mafungamano na Hamas. Mashambulizi mazito ya mizinga pia yaliendelea kwenye maeneo ya mipakani.

Watu waliopotezewa makaazi wakijihifadhi katika shule za Shirika la la Wakimbizi wa KIpalestina Ukanda wa Gaza.
Watu waliopotezewa makaazi wakijihifadhi katika shule za Shirika la la Wakimbizi wa KIpalestina Ukanda wa Gaza.Picha: Shawgy al-Farra

Jeshi la Israel limesema limeshambulia sehemu 200 katika kipindi cha saa 24 zilizopita. Imesema imeshambulia misikiti ambayo inaficha silaha na kwamba chuo kikuu hicho kinatumiwa na Hamas kama kituo cha kufanyia utafiti na kutengeneza silaha.

Mapigano makali kabisa yametokea karibu na sehemu ya shambulio la Ijumaa ambapo inadhaniwa ndiko alikotekwa nyara mwanajeshi huyo wa Israel karibu na Rafah kama kilomita tatu ndani ya Ukanda wa Gaza na karibu na mipaka ya Israel na Misri. Maafisa wameripoti kwamba karibu nyumba kumi na mbili zimebomolewa au kuangamizwa na mashambulizi hayo ya anga.

Mwanajeshi yumkini ameuwawa

Kitengo cha kijeshi cha Hamas kimesema kwenye tovuti yake kwamba "hadi sasa hawajuwi kitu kuhusu mwanajeshi huyo aliyetoweka au mahala aliko au mazingira ya kutoweka kwake."

Wafuasi wa Hamas wakiandamana kulaani mashambulizi ya Israel Ukingo wa Magharibi. (01.08.2014)
Wafuasi wa Hamas wakiandamana kulaani mashambulizi ya Israel Ukingo wa Magharibi. (01.08.2014)Picha: Reuters/Abed Omar Qusini

Kundi hilo linasema mwanajeshi huyo yumkini akawa ameuwawa katika mapambano na wapiganaji wa Hamas saa moja kabla ya kuanza kutekelezwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano saa mbili asubuhi na kwamba pia limepoteza mawasiliano na wapiganaji wake.

Taarifa hiyo imesema wanaamini wapiganaji wote wa kundi hilo wameuwawa kutokana na shambulio la anga la Israel akiwemo mwanajeshi huyo Mzayuni ambaye adui anasema ametoweka.

Jeshi la Israel limekataa kuzungumzia taarifa hiyo.

Hamas inaweza kuwa inajizuwiya kutowa habari kuhusu mwanajeshi huyo ili kulazimisha kuridhiwa kwa madai yao na Israel makakati ambao ulitumiwa huko nyuma na kundi la Hezbollah la Lebanone ambalo lilikuwa halikufichuwa iwapo wanajeshi wawili wa Israel iliwateka nyara hapo mwaka 2006 walikuwa hai au walikuwa wamekufa hadi pale walipokabidhi maiti zao katika mabadilishano ya wafungwa na Israel.

Hamas kugharamika vibaya

Baraza la mawaziri la Israel limekutana katika kirefu kisicho cha kawaida Ijumaa usiku kujadili suala la kutoweka kwa mwanajeshi wao huyo. Hakukutolewa tangazo rasmi juu ya hatua itakayochukuliwa lakini afisa katika ofisi ya waziri mkuu amesema Israel inataraji Marekani na jumuiya ya kimataifa kuchukuwa hatua kali kukabiliana na kundi la kigaidi ambalo linakaidi maagizo yao.

Vifaru vya Israel vikielekea Ukanda wa Gaza.(01.08.2014)
Vifaru vya Israel vikielekea Ukanda wa Gaza.(01.08.2014)Picha: picture-alliance/dpa

Afisa wa Israel ambaye hakutaka kutajwa jina lake kutokana na kutokuwepo kwa tangazo rasmi la serikali amesema "Hamas na makundi mengine ya kigaidi yatagharimika vibaya sana kwa vitendo vyao hivyo."

Kutoweka kwa mwanajeshi huyo mwenye cheo cha Luteni Hadar Goldin na mapambano makali yaliyofuatia yalivuruga makubaliano ya kusitisha mapigano yaliofikiwa chini ya usimamizi wa kimataifa ambayo yalikuwa yatekelezwe kwa siku tatu na kufungua njia ya kufanyika kwa mazungumzo mjini Cairo ya kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano yatakayodumu kwa muda mrefu zaidi.

Israel na Hamas zimekuwa zikishutumina kwa kuvunja makubaliano hayo ya kusitisha mapigano kwa misingi ya utu.

Pendekezo la Misri ndio ufumbuzi

Rais Abdel Fateh al-Sisi amesema Jumamosi mpango wa suluhu wa Misri unatowa fursa ya dhati kukomesha mzozo wa Gaza na amesisitiza haja ya kutekelezwa haraka kwa mpango huo.

Rais Abdel Fattah al-Sisi wa Misri.
Rais Abdel Fattah al-Sisi wa Misri.Picha: picture-alliance/dpa

Sisi ameuambia mkutano wa waandishi wa habari uliohudhuriwa na Waziri Mkuu wa Italia Matteo Renzi kwamba "Pendekezo la Misri ni fursa ya dhati ya kutafuta ufumbuzi kwa mzozo wa Gaza na kukomesha umwagaji damu".

Amesema wakati ni muhimu na kutaka fursa hiyo itumiwe haraka kuzima moto unaowaka katika Ukanda wa Gaza na kukomesha umwagaji damu wa Wapalestina.

Sisi amesisitiza kwamba pendekezo hilo la Misri unaweza kuwa msingi wa kuanzisha mazungumzo kati ya Israel na Hamas.

Ujumbe wa pamoja wa Wapalestina wakiwemo wawakilishi wa Hamas na Jihad unatazamiwa kuwasili Cairo leo kwa ajili ya mazungumzo ya kuwa na makubaliano ya usitishaji wa mapigano wa muda mrefu hata hivyo Israel imesema haitahudhuria mazungumzo hayo kwa kuwa Hamas haitaki mapatano na badala yake inawapotosha wasuluhishi wa kimataifa..

Mwandishi: Mohamed Dahman/AP/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef