1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel na Hamas huko Gaza

22 Mei 2007

Israel inajiandaa kuimarisha mashambulio yake dhidiya viongozi wa kipalestina na hata waziri mkuu Haniyeah yumo hatarini.

https://p.dw.com/p/CHDx

Machafuko yanazidi kupambamoto tena katika mwambao wa Gaza:Baada ya wapalestina wenye siasa kali kuendelea kuuhujumu mji mdogo wa Israel- Sderot kwa makombora hadi 100,kikosi cha wanahewa cha Israel, kinauhujumu mwambao wa Gaza usiku na mchana na hadi sasa wapalestina 36 wameuwawa.

Isitoshe,Israel imeanza upya siasa yake ya kuwalenga kuwaua viongozi wa kipalestina na imetishia hata kumua waziri-mkuu Ismail Haniyeh wa chama cha Hamas.

Israel imeahidi leo jibu kali kwa mashambulio ya makombora ya wapalestina ambayo yamemua mwanamke mmoja wa kiisrael.Hatahivyo, waziri mkuu Ehud Olmert ameungama hana suluhisho la haraka la hujuma za mfululizo za makombora yanayovurumishwa kutoka Gaza.

Vitisho hivi vya Israel vinafuatia siku ya mapigano makali ambamo wafuasi 5 wenye siasa kali

Wa kipalestina wameuliwa kwa mashambulio ya anga ya waisraeli.Hali hii yabainisha hakutasimamishwa mapigano kati ya pande hizo mbili yalioanza wiki sasa.

Wakuu wa ulinzi wa Israel wamearifu kuwa jeshi la Israel litaimarisha mashambulio dhidi ya wafuasi wenye siasa kali wa kipalestina na kuonya kuwa viongozi wa usoni kabisa wa chama cha HAMAS pamoja nao waziri-mkuu Ismail Haniyeh,waweza kuwa hatarini.

Viongozi wa Hamas kwahivyo, wameanza kuchukua hadhari pamoja na vikundi vyengine vya wapalestina vyenye siasa kali.

Baada ya shuari ya miezi 6 ,Israel imeanzisha upya hujuma zake za anga dhidi ya wakereketwa wa kipalestina huko Gaza.

Tawi la kijeshi la chama cha HAMAS limesema limefyatua makombora 2 katika mji huo mdogo wa Sderot mapema asubuhi ya leo.Sami Abu zuhri,mjumbe wa chama cha Hamas amesema Israel inapaswa kwanza kusimamisha hujuma zake kwa wapalestina kabla wao kuitikia .

Mkaazi mmoja wa mji wa Israel wa Sderot amenukuliwa kusema:

“Ninaomba laiti mmoja kati ya watoto wao anauwawa namna hii.Tumegeuzwa hapa Sderot “mabomu ya watu walio hayai”.Mnapaswa kwahivyo,kusaka jibu kuwanusuru watoto wa mji wa Sderot.”

Chama cha HAMAS,Islamic Jihad na kamati ya upinzani katika Gaza vimejitwika jukumu la hujuma hizo za makombora dhidi ya mji wa Sderot.

Ripota mmoja anasimulia :

“Mji wa Sderot umehujumiwa tena jana usiku kwa mlolongo wa makombora.Dakika moja iliopita tumesikia vishindo vya miripuko.Lilikua kombora lililoanguka si mbali na hapa tulipo.Magari ya kupakia majeruhi yamewasili hivi punde.Yadhihirika, kuna majeruhi.Usiku huu haukuanza vyema.”

Waziri wa ulinzi wa Israel,Amir Peretz akikutana jana na msemaji wa siasa za nje na maswali ya ulinzi wa Umoja wa Ulaya Bw.Javier Solana,aliitisha haraka mazungumzo ya kkidiplomasia ya kimataifa kuepusha kuibuka “ kwa ukosefu wa sheria na fujo utawala wa wapalestina ukiporomoka chini.”

Peretz akaongeza,

“Huu ni mtihani kwa diplomasia ya UU na ni mtihani kwa diplomasia ya ulimwngu huru.”