Israel itajenga makaazi mapya Jerusalem ya Mashariki
9 Novemba 2010Wizara ya mambo ya ndani imetangaza mradi wa kujenga nyumba 1.300. Tangazo hilo limetolewa wakati usio mzuri kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu. Hivi sasa yupo Marekani kwa majadiliano ya kutafuta njia ya kufufua majadiliano ya amani pamoja na Wapalestina yaliyokwama.
Msemaji wa serikali ya Marekani, amesema kuwa Washington imesikitishwa sana na tangazo hilo. Nae mpatanishi mkuu wa Wapalestina, Saeb Erekat amesema, mradi wa kuendelea na ujenzi wa makaazi ya Wayahudi katika ardhi ya Waarabu, unalenga kuvuruga mchakato wa amani.
Wakati huo huo,Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ujerumani Guido Westerwelle ametoa mwito kwa Israel kuondosha vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Ukanda wa Gaza tangu miaka minne iliyopita. Amesema, kuwazingira kiasi ya watu milioni 1.5 ni hali isiyokubalika. Vile vile hiyo inaimarisha itikadi kali na ni kizuizi kwa majadiliano ya amani yanayotafuta ufumbuzi wa mataifa mawili.
Wakati wa ziara yake hiyo fupi katika Ukanda wa Gaza, waziri Westerwelle alikataa kukutana na maafisa wa Hamas wanaodhibiti eneo hilo.Waziri huyo akatoa mwito kwa Wapalestina kumuachilia huru mwanajeshi wa Kiisraeli Gilad Shalit alietekwa nyara miaka minne iliyopita. Mwanasiasa huyo wa chama cha kiliberali cha FDP, ni waziri wa kwanza wa Ujerumani kutembelea Ukanda wa Gaza tangu mwaka 2006.