ISLAMABAD:Mazungumzo kati ya Rais Musharraf na Bi Bhutto huenda yakafanikiwa | Habari za Ulimwengu | DW | 04.10.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Habari za Ulimwengu

ISLAMABAD:Mazungumzo kati ya Rais Musharraf na Bi Bhutto huenda yakafanikiwa

Rais wa Pakistan Pervez Musharraf anasema kuwa ana imani kuwa mazungumzo kati yake na Bi Benazir Bhutto yatafua dafu hata baada ya kutisha kuwa wabunge wa chama chake watajiondoa bungeni.Chama cha Bi Bhutto cha Pakistan Peoples PPK kinakutana mjini London ili kufanikisha harakati za wabunge hao kujiuzulu ili kuathiri uchaguzi kwa kutoaminika.

Kulingana na Waziri mkuu huyo wa zamani mazungumzo ya kugawana madaraka yamekwama kabisa na kukanusha ripoti kuwa serikali huenda ikamfutia mashtaka ya rushwa yanayomkabili jambo lililomfanya kuenda uhamishoni.

Hata hivyo kwa mujibu wa maafisa wa serikali mjini Islamabad huenda Rais Musharraf hii leo akatangaza rasmi hatua hiyo ya kufutiwa mashataka ya rushwa ili aweze kushiriki katika uchaguzi.Hilo ni moja ya madai ya Bi Bhutto kabla kurejea nchini mwake tarehe 18 mwezi huu.Matokeo yanategemea mazungumzo ya dakika za mwisho nchini Pakistan na Uingereza yanayolenga kushawishi wandani wa kisiasa wa Rais Musharraf kumfutia mashtaka ya rushwa aidha kumvutia kushirikiana nao.

Chama cha PPK cha Bi Bhutto kinajiandaa kwa siku ya pili ya mazungumzo ya kuamua iwapo wabunge wao watajiuzulu.

Wakati huohuo mahakam kuu inaendelea kusikiliza maombi ya rufaa yaliyowasilishwa na wapinzani wa Rais Musharraf kupinga uteuzi wake tena siku ya jumamosi.Wanasiasa hao wanatoa wito wa uchaguzi huo kuahirishwa kwa madai kuwa Jenerali Musharraf hastahili kugombea wadhifa huo vilevile uchaguzi kufanywa na bunge jipya baada ya uchaguzi wa wabunge unapopangwa kufanyika mwanzoni mwa mwaka ujao.

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com