1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ISLAMABAD : Makomandoo 15 wauwawa katika mripuko

14 Septemba 2007
https://p.dw.com/p/CBPu

Taarifa kutoka Pakistan zinasema kwamba mtuhumiwa mshambuliaji wa kujitolea muhanga amejiripuwa na kuuwa makomando 15 wa Pakistan kwenye bwalo la kula katika kambi ya kijeshi hapo jana.

Duru zinasema wanajeshi wengine 11 wamejeruhiwa sita kati ya hao wakiwa mahtuti katika mripuko huo uliotokea huko Tarbela Ghazi katika jimbo la Mpaka wa kaskazini magharibi. Hata hivyo jeshi limesema bado linaendelea kuchuguza kile kilichosababisha mripuko huo.

Shambulio hilo linakwenda sambamba na mapigano makali ya siku mbili ambapo jeshi linadai kuwa limewauwa wanamgambo 50 wa kikabila na ziara ya naibu waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Negraponte nchini humo.

Wanamgambo wamekuwa wakililenga jeshi la Marekani katika mashambulizi yao tokea mwezi wa Julai wakati lilipouvamia Msikiti Mwekundu kuwatokomeza Waislamu wa itikadi kali waliokuwa wamejikomelea ndani.

Zaidi ya watu 250 waliuwawa katika uvamizi huo wa jeshi.