1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ishara za matumaini mema

Philipp, Peter (DW)3 Juni 2008

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier ziarani Mashariki ya kati

https://p.dw.com/p/EBqx
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Steinmeier anazungumza na kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina Mahmoud AbbasPicha: AP


Kwa miezi kadhaa siasa ya Ujerumani kuelekea Mashariki ya kati ilituwama katika maadhimisho ya miaka 60 tangu kuundwa dola la Israel.Masuala yanayozihusu nchi za kiarabu na Palastina yaliachwa kando kidogo.Ndio maana waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier ameingia njiani kwa muda wa siku nne mashariki ya kati,akizitembelea Libnan,Israel na ukingo wa magharibi wa mto Jordan.


Hali imerejea kua ya kawaida hivi sasa katika siasa ya Ujerumani kuelekea Mashariki ya kati.Angalao hiyo ndio sura inayotokana na ziara ya ghafla ya waziri wa mambo ya nchi za nje Frank-Walter Steinmeier katika eneo hilo.Katika miezi ya hivi karibuni,maadhimisho ya miaka 60 ya kuundwa dola la Israel ndio yaliyohodhi siasa ya nje.Binafsi kansela Angela Merkel alifika ziarani nchini humo.Taarifa zake za kushadidia urafiki na mafungamano pamoja na Israel ziliwafanya watu kujiuliza kama Ujerumani sasa inafuata nyayo za Marekani katika eneo hilo.


Hasha.Kwa kulitembelea eneo hilo hivi sasa,waziri wa mambo ya nchi za nje Frank-Walter Steinmeier ametaka kubainisha ukweli wa mambo,baada ya hotuba za sherehe za kuundwa dola la Israel.Mfano pale alipokosoa mipango ya Israel ya kujenga makaazi mepya ya wahamiaji wa kiyahudi katika ukingo wa magharibi akisema ni pingamizi kwa utaratibu kwa amani.La ziada hakuna aliyelitarajia kutoka kwa mwanasiasa wa Ujerumani,hasa tukizingatia ukweli kwamba mchango wa serikali kuu ya mjini Berlin katika eneo la mashariki ya kati,unasaidia  upande wa takwimu tuu licha ya dhamiri zote njema zilizoko.


Ni Takwimu za maana lakini. Frank Walter Steinmeier kwa hivyo anajaribu kuwapa moyo wapalastina waliopotelewa na matumaini kuelekea utaratibu wa amani,kwa kuwaahidi msaada wa Ujerumani katika kuimarisha miundo mbinu katika maeneo ya utawala wa ndani.


Hali ya kiuchumi na usalama ikiimarika,ndipo wananchi watakapoanza kuamini kwamba utaratibu wa amani ni bora zaidi kuliko msimamo shupavu wa wafuasi wa itikadi kali wa Hamas.


 Ujerumani inasalia na itaendelea kua mshirika muhimu na wa maana hasa katika kadhia  tete mfano makubaliano kati ya Israel na wafuasi wa Hisbollah nchini Libnan.Majadiliano yamekua yakiendelea tangu muda sasa kuhusu utaratibu wa kubadilishana wafungwa-na Berlin imechangia pakubwa katika majadiliano hayo.Mazungumzo hayo pamoja pia na muongozo mpya wa kisiasa uliofikiwa baada ya makubaliano ya Doha ndio chanzo cha ziara ya waziri wa mambo ya nchi za nje mjini Beirut.Bila ya shaka sio kwasababu ya kujihusisha moja kwa moja na maingiliano ya kichini chini,bali kwanza kutathmini serikali ya aina gani inaingia madarakani mjini humo.


Hadi wakati huu sertikali kuu ya Ujerumani ilikua ikimuunmga mkono waziri mkuu Fouad Siniora.Ikiwa hivi sasa analazimika kuwajumuisha Hisbollah katika serikali ya muungano, hawatampa kisogo,badala yake  siasa ya Ujerumani kuelekea Libnan itabidi idurusiwe.


Hali kama hiyo inaihusu pia Syria.Kinyume na kansela Merkel,waziri wa mambo ya nchi za nje Steinmeier anatetea umuhimu wa kujumuishwa Syria ,na hoja zake zinaonyesha kupata nguvu kutokana na mazungumzo ya siri kati ya Damascus na Jerusalem na utayarifu wa  Syria kuwaruhusu wataalam wa shirika la umoja wa mataifa la nguvu za atomiki waingie nchini humo.


Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani anatambua pia kwamba maendeleo na ufanisi pamoja na Syria na pia pamoja na Palastina utategemea matokeo ya mzozo wa kashfa inayomkaba waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert.Na katika kadhia hiyo Ujerumani haiwezi kushawishi chochote kile.