1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IS watekeleza mauaji kadhaa Iraq

Mjahida6 Januari 2015

Kundi linalojiita Dola la Kiislamu limewauwa wanaume wanane katika mkoa wa Salahuddin, kaskazini mwa Iraq, kwa kwa madai ya kushirikiana na serikali katika kulidhibiti kundi hilo.

https://p.dw.com/p/1EFiz
Wanamgambo wa IS
Wanamgambo wa ISPicha: Reuters

Baadhi ya picha zilizotumwa jana jioni (05.01.2015) katika mtandao wa kijamii wa Twitter unaotumiwa mara kwa mara na wanamgambo hao, zilionesha wanaume hao waliovalia nguo za rangi ya machungwa wakiwa wameuwawa huku mikono yao ikiwa ikifungwa nyuma ya migongo yao.

Watano kati yao walitambuliwa kama maafisa wa polisi huku wawili wakitambulika kama wapasha habari lakini hakuna maelezo yoyote yaliotolewa kwa muathiriwa wa nane.

Picha hizo zilionesha wanaume hao wakipelekwa karibu na kingo za mto na watu waliofunika nyuso zao, kisha wakapiga magoti wakiwa katika msitari mmoja na kupigwa risasi vichwani. Hata hivyo kundi hilo halikusema vifo hivyo vilitekelezwa wakati gani.

Huku hayo yakiarifiwa Shirika la uangalizi wa haki za binaadamu nchini Syria limesema mmoja wa maafisa wakuu katika kikosi cha polisi cha wanamgambo wa IS ambacho kimekuwa kikitekelezwa mauaji, alipatikana akiwa ameuwawa kwa kukatwa kichwa Mashariki mwa mkoa wa Deir al-Zor.

Moshi ukionekana baada ya mapigano Kati ya IS na wanajeshi wa Peshmerga
Moshi ukionekana baada ya mapigano Kati ya IS na wanajeshi wa PeshmergaPicha: picture-alliance/E. Yorulmaz /Anadolu Agency

Shirika hilo lililo na makao yake nchini Uingereza limesema, Afisa huyo anasemekana kuwa raia wa Misri aliyejulikana kama naibu kiongozi wa kundi la ulinzi la al Hesbah katika mkoa huo. Mwili wake ulioonesha dalili za mateso ulipatikana karibu na mtambo mmoja wa umeme katika mji wa al-Mayadeen.

Kundi la wanamgambo wa dola la Kiislamu waliotokea kutoka kundi la kigaidi la Al Qaeda wanaendelea kudhibiti baadhi ya miji nchini Syria na katika nchi jirani ya Iraq wamekuwa wakilengwa katika mataifa yote mawili kwa mashambulizi ya angani na muungano unaoongozwa na Marekani tangu mwezi Septemba mwaka uliopita. Mpaka sasa haijawa wazi ni nani aliyetekeleza mauaji hayo.

IS watoa amri ya kusitisha elimu katika maeneo wanayoyadhibiti

Watu hao ambao bado hawajajulikana pia walijaribu kuwauwa wanamgambo wengine wawili mjini humo lilisema shirika hilo la kueteta haki za binaadamu. Jaribio la kwanza ni pale gari moja lilipojaribu kumgonga mwanamgambo mmoja karibu na mzunguko wa magari. Na mwengine alipigwa na mshambuliaji aliyekuwa na silaha ya chuma akiwa katika pikipiki. mwanamgambo huyo anasemekana kujeruhiwa vibaya.

Wakati huo huo shirika la kuwashughulikia watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF limesema takriban watoto 670,000 nchini Syria wananyimwa haki ya elimu, kufuatia wanamgambo wa dola la kiislamu kutoa amri ya kufungwa kwa shule nchini humo na kubadilisha mtaala wa elimu.

Ndege zinazofanya mashambulizi dhidi ya IS
Ndege zinazofanya mashambulizi dhidi ya ISPicha: picture-alliance/dpa/S. Nickel

Mwezi Novemba mwaka jana kundi hilo lilifunga shule katika maeneo inayoyadhibiti Mashariki mwa Syria kwa kukosekana masomo ya kidini katika mtaala wa elimu. Kundi hilo linadaiwa kuhusika katika visa vya ubakaji mauaji ya halaiki kuwatumia wanawake na watoto kama watumwa na kuwasajili watoto kama wapiganaji.

Kwa upande wake msemaji wa shirika la UNICEF Christophe Boulierac aliuambia mkutano wa waandishi habari kwamba mwezi Desemba shirika hilo lilitoa amri ya kusitisha elimu katika maeneo inayoyashikilia au kuyadhibiti.

Mwandishi: Amina Abubakar/AP/Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef