1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yajaribu kombora la masafa marefu

28 Septemba 2009

Katikati ya mgogoro mpya uliozuka kuhusu mradi wa nyuklia wa Iran, nchi hiyo kama ilivyoarifu hii leo imejaribu kombora la masafa marefu Shahab-3.

https://p.dw.com/p/Jsan
Iranian President Mahmoud Ahmadinejad listens during a press conference in New York, Friday Sept. 25, 2009. (AP Photo/Bebeto Matthews)
Rais wa Iran,Mahmoud Ahmadinejad.Picha: AP

Hilo ni kombora lenye uwezo wa kwenda umbali wa kilomita 2,000 na hivyo linaweza kufika hadi Israel na hata vituo vya kijeshi vya Marekani katika nchi za Ghuba. Licha ya vitendo vya uchokozi vya mara kwa mara, serikali ya Marekani inasema mgogoro wa nyuklia wa Iran unapaswa kusuluhishwa kwa njia ya kidiplomasia.

Vyombo vya habari vya Iran vimearifu kuwa leo, nchi hiyo imefanikiwa kufanya jaribio la kombora la masafa marefu Shahab-3 linaloweza kwenda umbali wa kilomita 2,000. Mwisho wa juma lililopita, Iran ilikwishajaribu makombora ya masafa mafupi na ya wastani. Hii leo msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran Hassan Ghashghavi alieleza kuwa majaribio yaliyofanywa hayahusiki na mtambo wa pili unaojengwa kurutubusha madini ya uranium. Hayo ni majaribio ya kawaida yanayofanywa kila mwaka kuchunguza uwezo wake wa kujihami. Ni kawaida kwa kila nchi kujaribu uwezo wake wa kijeshi.

Majaribio hayo ya makombora yamefanywa baada ya juma lililopita kujilikana kuwa Iran inajenga mtambo wa pili wa kurutubisha uranium. Habari hiyo imesababisha wasiwasi katika jumuiya ya kimataifa na Iran imekosolewa vikali. Rais wa Marekani Barack Obama alieleza hivi:

"Kuwepo kwa mtambo huo kunadhihirisha kuwa Iran inakataa kuitikia mito ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na masharti ya Shirika la kimataifa la nishati ya nyuklia IAEA."

Hata hivyo Waziri wa Ulinzi wa Marekani Robert Gates anaamini kuwa bado upo uwezekano wa kusuluhisha mgogoro huo wa nyuklia wa Iran kwa njia ya kidplomasia. Siku ya Alkhamisi wajumbe wa nchi tano wanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama yaani Marekani, Ufaransa,Urusi,Uingereza,China pamoja na Ujerumani watakutana na Iran mjini Geneva Uswissi. Lakini Iran imesema inataka kuzungumzia masuala ya kimataifa na sio mradi wake wa nyuklia. Inasema,mtambo wake mpya haukiuki sheria ya kimataifa na hofu za nchi za magharibi hazina msingi.

Marekani na washirika wake wa magharibi wana hofu kuwa Iran inautumia mradi wake wa nyuklia kujipatia kwa siri bomu la atomiki. Iran lakini inakanusha tuhuma hizo na mara kwa mara imesisitiza kuwa lengo la mradi huo wa nyuklia ni kuzalisha nishati kwa matumizi ya amani.

Mwandishi: K.PfefferZPR - (P.Martin/RTRE/AFPE)

Mhariri: Othman, Miraji