1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yaitisha mkutano na Iran na Syria

1 Machi 2007

Irak imetoa mualiko kwa mikutano 2 ikizishirikisha Iran na Syria na Marekani kuzungumzia hali tete ya Irak.Iwapo katika vikao hiovyo,Marekani itazungumza moja kwa moja na mahasimu wake -Iran na Syria,haijulikani kwa sasa.

https://p.dw.com/p/CHJC

Marekani itajumuika pamoja na Syria na Iran mwezi huu wa Machi na ujao kuhudhuria mikutano 2 ya kimataifa kuzungumzia hali nchini Irak.

Waziri wa nje wa Marekani Dr.Condoleeza Rice amearifu kwamba mualiko unatoka serikali ya Irak.Dr.Rice amekaribisha pendekezo hilo na kuelezea matumaini kwamba uhusiano baina ya nchi za eneo hilo utatengenea kupitia mazungumzo hayo.

Usalama,ushirikiano na suluhu-mada hizi si za kawaida unapoizungumza Irak.Mshauri wa waziri mkuu wa Irak Al Maliki, alizitaja mada hizo alipotangaza mkutano huo ambao serikali ya Irak inatazamia utabadili sura ya mambo.

Mchango wa walioalikwa mkutanoni kutatua matatizo yanayo onekana hayatatuliki unatarajiwa.Mbali na Marekani, zimealikwa pia nchi mbili hasimu wa marekani-Iran na Syria.Serikali mjini Baghdad imethibitisha mualiko huo lakini bila shaka kwanza ilishauriana na Marekani.

Mjumbe wa Iran Ali Larijani hakukawia kuitikia mualiko huo kuhudhuria Iran .Larijani amesema ikiwa mkutano huo ni kwa masilahi ya Irak,Iran itashiriki.

Bado lakini hakuna maelezo ya mipango ya kikao hiki lakini thamyani yake kwa sasa ni zaidi kuitishwa kwake kuliko matokeo yake.Ni hayo tu yanayofahamika kwa sasa.Mkutano wa kwanza mwezi huu wa machi haujawekewa bado tarehe.Inafahamika tu kwamba umeitishwa na Irak.Mbali na nchi zilizotajwa,majirani wengine wa Irak wamealikwa:Saudi Arabia,Jordan na Uturuki.Halkadhalika, Misri na Jumuiya ya nchi za kiarabu-Arab League imepewa mualiko.

Wataakilishwa pia wajumbe wa wanachama wa kudumu wa Baraza la usalama la UM –yaani mbali na Marekani, Russia,China,Uingereza na Ufaransa na hata pia Umoja wa Ulaya.

Duru hizo 2 zitafanyika kwa wajumbe wasio wa hadhi ya juu alao katika kikao cha kwanza.Mwezi ujao ndipo mabalozi watakaposhiriki na kuyaendeleza mazungumzo.Kile hasa kitakachojadiliwa, kwa sasa hakifahamiki.Wazi ni matarajio ya mchango wa kila nchi inayoshiriki kuchangia kuleta utulivu nchini Irak.

Iran itatarajiwa kutumia ushawishi wake kwa waumini wa madhehebu ya kishia nchini Irak kuacha mapambano yao na wale wa madhehebu ya Sunni .Syria itatarajiwa kuulinda barabara mpaka wake mrefu na Irak na kuzuwia wapiganaji kuvuka mpaka kuingia Irak.Na Marekani ianzishe mazungumzo yatakayoiwezesha baadae kungatuka na vikosi vyake nchini Irak.

Iwapo katika mikutano yote 2 kutafanyika mazungumzo baina ya Marekani na Syria au Marekani na Iran ni jambo la kuvumisha kwa sasa,kwani hakuna nguzo ya kuegemea .Pia ni vigumu kwa sasa kusema Marekani inabadili sera zake kuelekea Iran.Kwani miezi 2 nyuma tu, rais Bush aliyapa mgongo mashauri yaliotolewa na Tume ya “Baker na Hamilton” yalioitisha mawasiliano ya moja kwa moja na Syria na Iran.