Iran yaipongeza Uingereza kwa kubadili msimamo | Matukio ya Kisiasa | DW | 04.04.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Iran yaipongeza Uingereza kwa kubadili msimamo

Iran imeikaribisha hatua ya Uingereza kuanza kutumia njia za kidiplomasia kuutanzua mzozo wa mabaharia wake 15 wanaozuiliwa mjini Tehran.

Waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair

Waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair

Spika wa bunge la Iran leo ameipongeza hatua ya Uingereza kuregeza msimamo wake kuhusiana na mabaharia 15 waliokamatwa wakati walipoingia himaya ya Iran katika ghuba la Uajemi. Gholam Ali Hadad Adel amesema hatua ya Uingereza kuanza kutumia diplomasia kuutanzua mgogoro huo inafaa.

Aidha spika huyo amesema hatua zilizochukuliwa na Uingereza katika siku chache zilizopita zinabadili maneno makali ambayo yamekuwa yakitolewa na Uingereza na badala yake inataka kuwa na mazungumzo ya kuumaliza mzozo huo kwa njia ya kidiplomasia. Hata hivyo Gholam Ali amesisitiza kwamba Uingereza inatakiwa ikubali makosa yake na ibadili tabia.

Sambamba na taarifa hiyo, Syria inazipatanisha Uingereza na Iran kuhusu mzozo unaoendelea. Waziri wa mashauri ya kigeni wa Iran, Walid Muallem, ameliambia gazeti la Al Anbaa hii leo mjini Damascus kamba ana matumaini suluhisho litapatikana kwa njia ya kidplomasia na Syria inafanya juhudi kuhakikisha mzozo huo unamalizika.

Maafisa wa Uingereza wamesema David Treisman, afisa wa wizara ya mashauri ya kigeni, alifanya mazungumzo jana jioni na balozi wa Iran mjini London. Mkutano huo ulikuwa wa nane tangu kukamatwa kwa mabaharia 15 wa Uingereza.

Uingereza inasubiri majibu rasmi kutoka kwa serikali ya Tehran kuhusiana na pendekezo ililoliwasilisha ikitaka mazungumzo ya ana kwa ana kuumaliza mgogoro ambao umekuwa ukiendelea kwa siku 13. Maofisa wa serikali ya Uingereza mjini London wameeleza shauku yao wakitaka swala hilo litatuliwe haraka iwezekanavyo.

Taarifa iliyotolewa jana na waziri mkuu wa Uingereza Tony Blar ilisema kiongozi huyo atawajibika kuumaliza mzozo baina ya Uingereza na Iran kwa njia ya kidiplomasia. Blair anaamini nchi zote mbili zinataka kuumaliza mzozo huo haraka iwezekanavyo kupitia mazungumzo ya ana kwa ana.

Rais wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad, anatarajiwa hii leo kufanya mkutano na waandishi wa habari ambapo atazungumzia kuhusu mabaharia wanaume 14 na mwanamke mmoja wa Uingereza waliokamatwa mnamo tarehe 23 mwezi uliopita. Televisheni ya Iran imetangaza kwamba rais huyo atafanunua wazi msimamo wa Iran kuhusu mzozo huo.

Kwa mujibu wa utawala wa sharia nchini Iran, sera ya kigeni huamuliwa na kiongozi mkuu wa kidini nchini humo, Ali Khamenei. Lakini wachambuzi wanasema kiongozi huyo husikiliza maoni yanayotolewa kwa hiyo pande zinazozana zina nafasi ya kuchangia uamuzi wa kisera atakaopitisha.

Wairan wenye msimamo mkali kama walinzi wa mapinduzi wa Iran wameelezea azma yao kutaka kuonyesha uwezo wao kwa mataifa ya magharibi hususan wakati huu ambapo Wairan watano wanaendelea kuzuiliwa na Marekani nchini Irak. Marekani inasema Wairan hao wana uhusiano na jeshi la mapinduzi la Iran, lakini Iran inasema ni wanadiplomasia.

 • Tarehe 04.04.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHGw
 • Tarehe 04.04.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHGw

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com