1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran na Umoja wa Ulaya wapanga kuuendeleza mpango wa nyuklia

Yusra Buwayhid
15 Mei 2018

Waziri wa mambo ya nje wa Iran anatarajiwa Jumanne kukutana na wanadiplomasia wa mataifa ya Ulaya, mjini Brussels akitafuta uungwaji mkono wa kuyanusuru makubaliano ya nyuklia baada ya Marekani kujitoa hivi karibuni.

https://p.dw.com/p/2xjQs
Symbolbild Kündigung Atomabkommen mit Iran durch USA
Picha: Imago/Ralph Peters

Akitokea nchini Iran, waziri wa mambo ya nje wa Iran Mohammad Javad Zarif kwanza alitua mjini Beijing, China na baadae kuelekea Moscow, Urusi, kabla ya kufunga safari ya kwenda mjini Brussels ambapo atawasili Jumanne jioni na kukutana na wenzake kutoka Uingereza, Ufaransa na Ujerumani mataifa matatu ya barani Ulaya yaliyosaini makubaliano hayo na kukasirishwa na hatua ya Rais wa Marekani Donald Trump kujitoa katika makubaliano hayo ya nyuklia na Iran. Mawaziri hao watajadili juu ya namna ya kuyaendeleza makubaliano hayo yaliyoafikiwa mwaka 2015 ili kudhibiti programu ya silaha za nyuklia ya Iran.

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergey Lavrov pamoja na mawaziri wenzake wa Ufaransa, Ujerumani na Uingereza, tayari wameshaweka wazi kwamba wanataka kuyanusuru makubaliano hayo. Haya hapa ni miongoni mwa masuala muhimu ambayo yanatarajiwa kujadiliwa katika mazungumzo ya leo:

Iran inahitaji uhakikisho kutoka kwa nchi zilizosaini kwamba makubaliano hayo ya nyuklia bado yataendelea kuwepo, hata baada ya Marekani kujiondoa. Iran inataka kupewa jawabu baada ya siku 60 lakini Umoja wa Ulaya ambao ni miongoni mwa pande zilizosaini makubaliano hayo imeomba siku 90.

China Mohammed Dschawad Sarif, Außenminister Iran
Waziri wa mambo ya nje wa Iran Mohammad Javad zarifPicha: Reuters/T. Peter

Masharti ya Iran 

Iran pia inadai kupewa fidia ya fedha kutoka katika mataifa mengine yaliyosaini makubaliano hayo ya nyuklia, pindi Marekani itakapoiwekea vikwazo. Trump ameahidi kuiwekea Iran vikwazo vikali vya kibiashara. Bado haijulikani Iran itadai kiasi gani cha fedha.

Marekani pia inataka kuziadhibu kampuni za Ulaya pamoja na nchi ambazo zitafanya biashara na Iran. Waziri wa fedha wa Ufaransa Bruno Le maire amesema nchi yake itaunda mfumo wa kuzilinda kampuni za Kifaransa. Na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Luxemborg Jean Asselborn amependekeza kutolewa leseni mpya ya biashara kati ya nchi za Ulaya na Iran. Pia amesema lazima kuwepo na njia ya kuendeleza biashara ya mafuta ya Iran.

Umoja wa Ulaya - Marekani

Umoja wa Ulaya bado unataka kuishawishi Marekani kubaki katika makubaliano hayo. Ndiyo maana Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akapendekeza kuyapanua makubaliano yao ya awali na kujumuisha pia nguvu ya kijeshi ya Iran, ikiwamo kujihusisha kwake na vita vya Syria pamoja na programu yake ya makombora. Iran hata hivyo huenda isikubaliane na hilo.

Suala muhimu kuliko yote kuhusu makubaliano hayo ya nyuklia, hata hivyo, ni iwapo kama yataweza kuendelezwa bila ya msaada wa Marekani. Wanadiplomasia wa Marekani wamesema nchi yao itaendelea kusaidia suala la ukaguzi la shirika la kimataifa la kudhibiti nishati ya nyuklia - IAEA.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/dw/afp

y86world

Mhariri: Iddi Ssessanga