1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran kuwekewa vikwazo ?

23 Februari 2007

Iran haikuitikia azimio la UM kusimamisha mradi wake wa kinuklia na jumatatu ijayo itaamuliwa ni hatua gani kuichukulia.

https://p.dw.com/p/CHJM

Iran imekataa kusimamisha mradi wake wa kinuklia.Shirika la nguvu za Atomiki Ulimwenguni (IAEA) lilitoa jana ripoti yake mjini Vienna,Austria kuhusu mradi wa Iran.

Ripoti hiyo ilisema kwamba, Iran inaendelea na mradi wake na hivyo inakiuka azimio nambari 1737 la UM ambalo liliitaka Iran isimamishe kabisa kurutubisha madini ya uranium katika vinu vyake vya kinuklia.Jumatatu ijayo kwahivyo, Baraza la Usalama la UM na Ujerumani litakutana kuamua hatua gani ya kuichukulia Iran:

Yule anaesoma mambo makuu yaliomo katika ripotio hiyo juu ya Iran iliochapishwa mjini Vienna, hagundui lolote lile ambalo hapo kabla halikujulikana:

Jamhuri ya kiislamu ya Iran imepuuza kabisa amri iliomo katika azimio la UM nambari 1737 kusimamisha mradi wake wa kinuklia.Isitoshe, imeanzisha kazi hukjo Natanz ya kurutubisha madini ya uranium.Halkadhalika, Iran inapanga kuongeza kipimo cha urutubishaji wa madini hiyo kufikia 3.000 hadi mwezi Mei.

Kinachotia wasi wasi sio hasa taarifa hizo ambazo rais Ahmadinejad tayari alikwisha zinadi hadharani, bali ni taarifa za Shirika la Nguvu za Atomiki Ulimwenguni kuwa halina uwezo tangu wa kujua iwapo kuna harakati zaidi za kinuklia zinazoendelea nchini Iran na hata kutoa taarifa madhubuti iwapo mradi wa Iran wa kinuklia kweli kama inavyodai serikali ya Iran ni wa nishati tu.

Imeonekana tena na tena Iran ikifungua kwa taabu sana milango yake ya vinu vyake vya kinuklia kwa wakaguzi kutoka Vienna au wakati mwengine wakikomea kabisa milango pasmoja na kutowaruhusu kabisa baadhi ya watumishi wa shirika hilo kukanyaga ardhi ya Iran.

Tabia hii sio tu yazusha shaka-shaka ,bali pia inapingana na hoja za wanasiasa wenye siasa kali wa Iran wanaodai nchi yao –Iran, ni mhanga wa siasa za kambi ya magharibi za kumiliki nchi nyengine.

Wakati umewadia kwa Teheran kutambua kwamba inazidi kujitenga binafsi na ulimwengu kisiasa kama ilivyodhihirika katika kupitishwa kwa azimio nambari 1737 la UM.

Limebkia swali la kutatanisha:Kifanywe nini sasa ? Vikwazo vikali zaidi vinaweza tu kuonesha mafanikio ikiwa vitazidisha kudhofisha uchumi wa Iran na hivyo kuchochea kutoridhika na uongozi wa rais Mahmoud Ahmadinejad.

Hatahivyo, hatua hii inaleta hatari 2:Kwanza ,Urusi na China zaweza kujitenga na kuiwekea Iran vikwazo na pili, kunaweza kukashadidia ile dhana kuwa Iran ni mateka na hivyo ikapata wafuasi wengi zaidi wa kuihurumia na kukakuza mpambano .

Matumaini yapo katika kuendelea na mazungumzo ya moja kwa moja na Teheran,lakini bila ya masharti.

Njia hii itaitoa kambi ya magharibi mhanga mkubwa,kwani itakuwa na maana azimio la kwanza nambari 1696 la majira ya kiangazi mwaka jana na la pili 1737 la Desemba mwaka uliopita hayakufua dafu.Lakini kuna njia nyengine ya kufuata ?

Ama Iran itajitoa kutoka mkataba wa kutoeneza silaha za kinuklia au itashambuliwa kijeshi-jambo ambalo matokeo yake mtu hahitaji mpiga ramli kuagua –kwani si Iran tu itakayoumia .