1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran kurutubisha madini kwa asilimia 20.

Halima Nyanza8 Februari 2010

Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Iran ameonya kuwa nchi yake karibuni itaanza yenyewe kurutubisha madini ya uranium kwa kiwango cha asilimia 20, iwapo mataifa yenye nguvu yataendelea kuichezea nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/LvQT
Rais wa Iran Mahmoud Ahmadinejad.Picha: AP

Rais wa Iran ametoa kauli hiyo wakati wanachama watano wa kudumu katika baraza la Usalama la Umoja wa Matafa pamoja na Ujerumani wakiwa wamekutana kwa siku tatu kuanzia Ijumaa, wiki iliyopita, mjini Munich Ujerumani kuizungumzia nchi hiyo na mradi wake wa nyuklia.

Akizungumza mjini Tehran Rais Mahmoud Ahmadinejad, hata hivyo amesema bado wana nia ya kushirikiana na nchi za magharibi, ili kufikia makubaliano, lakini ikiwa bado nchi za maharibi zinataka kuendelea kulichezea taifa hilo, watajiandaa wenyewe kurutubusha madini hayo, na kwamba Shirika la Nguvu za Atomiki la nchi hiyo -IAO- liko tayari kuanza kurutubisha madini hayo na hatimaye watafanya hivyo.

Rais wa Iran amesema aliyapa mataifa hayo yenye nguvu muda kukubali makubaliano hayon kwamba sasa atamuagiza mkuu wa Shirika la Nguvu za Atomiki la hapa nchini Dakta Ali Akbar Salehi kuanza kazi ya kuzalisha mafuta kwa kiwango cha asilimia 20 kwa kutumia mashine.

Amesisitiza kuwa milango kwa ajili ya majadiliano iko wazi.

Wiki iliyopita Rais Ahmadinejad alisema nchi yake iko tayari kuruhusu madini yake ya Uranium kwenda kurutubishwa nje ya nchi hiyo.

Amesema Iran kamwe haijazuia makubaliano hayo, lakini hawataweza kupoteza muda wao kwa kufanya majadiliano yasiyopaswa, hivyo wataanza wao wenyewe kurutubisha kwa kiwango cha asilimia 20.

Nalo Shirika la Habari la Iran -IRNA- limearifu kwamba Mkuu wa Shirika la Nguvu za Atomiki nchini humo Dokta Ali Akbar Salehi leo atalifahamisha Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki kuhusu uamuzi wa Iran wa kuanza urutubishaji huo kwa kiwango cha asilimia 20 na kwamba nchi hiyo itaanza yenyewe mpango wake huo siku ya Jumanne katika mtambo wa Natanz ulioko katikati ya nchi hiyo.

Wakati huo huo, Waziri wa Ulinzi wa Marekani Robert Gates amesema iwapo Jumuiya ya Kimataifa itakuwa na msimamo wa pamoja na kutoa shinikizo kwa serikali ya Iran, anaamini kuwa muda bado upo wa kuiwekea vikwazo nchi hiyo.

Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Karl-Theodor zu Guttenberg, amesema jumuiya ya kimataifa inapaswa kuieleza Iran waziwazi kuwa subira yake imefikia mwisho.

Wakati uwezekano wa Iran kuwekewa vikwazo ukiongezeka, China, nchi ambayo ina kura ya turufu katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa imeweka wazi kwamba inayataka mataifa makubwa kuendeleza mazungumzo na Iran kuliko kuiwekea vikwazo vipya nchi hiyo.

Katika hatua nyingine Mkuu wa Shirika la Nyuklia la Iran amefahamisha kuwa nchi yake itajenga mitambo mipya kumi ya kurutubishia nyuklia katika kipindi cha mwaka mmoja.

Mwezi Novemba mwaka jana Iran ilitangaza mpango wake huo wa kujenga vinu vipya, lakini haikutangaza muda gani.

Nchi za magharibi zimekuwa zikihofia kuwa Iran inatengeneza nyuklia hiyo kwa ajili ya kutengenezea silaha, jambo ambalo limekanushwa na Iran yenyewe na kusema kuwa ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya raia.

Mwandhishi: Halima Nyanza (dpa, Reuters)

Mhariri: Josephat Charo