1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran inaweza kulipiza kisasi ikishambuliwa?

24 Novemba 2009

Wanajeshi wa Iran wameanzisha mazoezi ya kijeshi ya angani yaliyo na azma ya kuuonyesha uwezo wake katika mapambano endapo viwanda vyake vya nuklia vitashambuliwa.

https://p.dw.com/p/KdIc
Rais wa Iran Mahmoud AhmedinejadPicha: AP

Wakati huohuo Marekani imeitolea wito Iran kuyakubali mapendekezo ya kuusitisha mpango wake wa nuklia katika kikao cha usalama kinachoendelea Halifax,Canada.Kwa upande mwengine Rais was Iran Mahmoud Ahmedinejad  yuko katika ziara ya siku tano huko Amerika kusini iliyo na azma ya kutafuta kuungwa mkono katika mpango wake wa nuklia.Maandamano ya kuipinga ziara hiyo tayari yamefanyika Brasil mjini Rio de Janeiro.

Iran will nach Fristablauf Uran-Anreicherung wieder aufnehmen Iran Atomkraftwerk im Süden des Landes undatiertes Foto Uran Atomstreit
Kiwanda cha nuklia cha BushehrPicha: dpa

Wanajeshi wa kikosi cha anga wameanza mazoezi ya kijeshi yakiwemo yale ya mapambano endapo viwanda vyake vya nuklia vitashambuliwa.Kulingana na kituo cha televisheni cha taifa pamoja kile cha Al-Alam mazoezi hayo yatadumu kwa kipindi cha siku tano zijazo.Mkuu wa kikosi cha jeshi cha angani Brigadia Jenerali Ahmad Mighani alisema kuwa lengo hasa ni kuyazuia mashambulio dhidi ya viwanda vya Iran vya nuklia vilevile kuuimarisha utendaji wa vitengo mbalimbali vya kijeshi.Vitengo hivyo vinakijumuisha kikosi cha Revolutionary Guards pamoja na wapiganaji wa Basj.Viwanda ambavyo vinayarutubisha madini ya uranium viko katika eneo la Isfahan na karibu na Teheran ila kile ambacho hakijaanza operesheni hiyo kiko katika jimbo la Bushehr.Mataifa ya magharibi yanaamini kuwa shughuli ya kuyarutubisha madini ya uranium huko Iran ina azma ya kutengeza silaha za nuklia madai inayoyakanusha.Wakati huohuo katika kikao cha usalam akinachofanyika Halifax,Canada- Marekani imeitolea wito Iran kushirikiana na mataifa ya magharibi katika suala hilo la nuklia.

Kwa mujibu wa Robert Wood naibu msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani wawakilishi  wa mataifa makubwa yanayohusika katika majadiliano hayo--Urusi,China,Uingereza,Ufaransa na Ujerumani-- bado wana imani kuwa mazungumzo yanaweza kuwa suluhu.Kiongozi anayeondoka wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na uangalizi wa masuala ya nuklia IAEA Mohamed El Baradei alililisitiza''Naona kwamba tuko katika wakati muhimu.Naona kwamba tumebadili misimamo badala ya kushambuliana kuna uwazi zaidi na ushirikiano''.

El Baradei spricht mit Ahmadinedschad über Atomstreit IAEA Iran
Kiongozi wa IAEA Mohamed ElBaradei na Rais Mahmoud Ahmadinejad wa IranPicha: picture-alliance/dpa

Viongozi hao hata hivyo wamesema kuwa wamevunjwa moyo na Iran ambayo iliyakataa Ijumaa iliyopita mapendekezo yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa ya kupokea msaada wa mafuta ya nuklia au kuridhia kushiriki katika mazungumzo mapya.Hata hivyo suala la kuichukulia Iran hatua za kijeshi huenda lisifanyike kwa sasa ila kuna uwezekano wa kuiongezea vikwazo.Mwezi wa Septemba mwaka huu Iran ilitangaza kuwa inajenga kiwanda cha pili cha kurutubisha madini ya uranium kwenye eneo lililo karibu na mji mtukufu wa Qom jambo lililoyaghadhabisha mataifa ya magharibi.Kufuatia tangazo hilo mataifa hayo yalitisha kuwa huenda yakaiwekea vikwazo vipya endapo Iran haitouelezea bayana mpango wake wa nuklia.Rais Barack Obama wa Marekani alisema kuwa Iran haina budi ila kutoa ushirikiano''Iran lazima iyafuate maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na ihakikishe kuwa inawajibika kama mwanachama wa jumuiya ya kimataifa.Tumeinyoshea Iran mkono ili iweze kuwa sehemu ya jamii ya kimataifa ikiwa itatimiza wajibu wake na hilo bado halijabadilika''alisisitiza. 

Yote hayo yakiendelea Rais wa Iran Mahmoud Ahmedinejad anaelekea kwenye mataifa ya Amerika ya Kusini ili kupata kuungwa mkono katika suala hilo la nuklia linalozua utata.Rais Ahmedinejad alianzia ziara hiyo Gambia alikokutana na Rais Yaya Jammeh walikojadili masuala ya biashara na usalama.Katika eneo la Latin Amerika kituo chake cha kwanza kitakuwa Brasil na anatarajiwa kufanya mikutano ya faragha na Rais Lula da Silva aliyesema kuwa amepata heshima kubwa kwasababu ya ziara hiyo na anaiunga mkono Iran katika mpango wake wa nuklia.Ifahamike kuwa Brasil ina uhusiano mzuri na Marekani,Israel na mataifa mengine ambayo yanaiunga mkono hatua ya kuusitisha mpango wa nuklia wa Iran.Viongozi hao huenda wakalijadili suala la ushirikiano katika sekta ya nuklia.

Kabla ya kuwasili Rio de Janeiro mamia ya watu walikusanyika mjini humo kuipinga ziara ya Rais Mahmoud Ahmedinejad.Hii leo maandamano mengine ya wayahudi yanatarajiwa kufanyika katika mji mkuu wa Brasilia.Hii ni kwasababu kiongozi huyo alitoa wito wa Israel kufutwa katika ramani ya dunia.Rais Ahmedinejad anapanga kuzizuru pia Bolivia na Venezuela.

Mwandishi:Thelma Mwadzaya/ DPAE-AFPE

Mhariri:Abdul-Rahman