Iran, EU kutafuta msimamo wa pamoja makubaliano ya nyuklia
11 Januari 2018Umoja wa Ulaya, pamoja na mawaziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza, Ujerumani na Ufaransa watajiunga pamoja kutetea makubaliano hayo ya kinyuklia pamoja na Iran, ambayo yanadhibiti azma ya Iran kujipatia silaha za kinyuklia ili kuweza nchi hiyo kupunguziwa vikwazo vikali lakini ambavyo Rais Donald Trump wa Marekani amevikosoa mara kwa mara na kutishia kujitoa kutoka katika makubaliano hayo.
Wakati mkuu wa sera za mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini anataka kuliweka suala la kinyuklia tofauti na masuala mengine yenye utata na Iran, waziri wa mambo ya kigeni wa Iran, Mohammad Javad Zarif pia atakabiliana na maswali mazito juu ya maandamano ya hivi karibuni ya kuipinga serikali ambayo yamesababisha watu 21 kuuwawa. Zarif alisema kwamba nchi yake inatekeleza sehemu yake ya makubaliano hayo.
"Kwa bahati mbaya mjumbe mwingine wa kamati ya kuchukua hatua si tu hajatimiza majukumu yake lakini pia anatekeleza sera za uharibifu."
Makubaliano ya kinyuklia na Iran yamejumuisha mzozo mkubwa katika Mashariki ya Kati na ni moja kati ya mzizi wa masuala ambayo dunia haingependa kuyaacha yaongezeke. Amesema waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani sigmar Gabriel. Ameongeza kwamba kwa mataifa ya Ulaya kama majirani wa eneo la mashariki ya kati hilo ni sehemu kubwa ya usalama wa mataifa hayo.
Marekani yatafakari
Rais Donald Trump wa Marekani, ambaye mwezi Oktoba alikataa kuthibitisha kwamba Iran inatekeleza makubaliano yaliyofikiwa, lakini pia hakufikia kujitoa kutoka makubaliano hayo, anatarajiwa kuamua kesho Ijumaa iwapo atarefusha hatua ya kuiondolea Iran vikwazo vinavyohusiana na suala hilo la kinyuklia.
Umoja wa Ulaya na mataifa mengine yenye nguvu duniani umeonya mara kadhaa kuwa itakuwa ni makosa kujiondoa kutoka katika makubaliano hayo, yaliyofikiwa pamoja na Iran kwa muda wa miaka 2 kati ya Marekani, Uingereza, Ufaransa, China, Ujerumani na Urusi.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza Boris Johnson ameyaita makubaliano hayo, muhimu ambayo yanauweka ulimwengu katika hali ya usalama".
"Ni muhimu kwamba tunaendelea kufanya kazi pamoja na washirika wetu wa mataifa ya Ulaya kuendeleza makubaliano hayo na Iran, na usalama na ustawi unaotokana na makubaliano hayo unawafikia watu wa Iran na dunia kwa jumla.
Kwa mujibu wa vyanzo nchini Marekani, Trump hajafanya maamuzi hadi ilipofika jana Jumatano, wakati Johnson aliliambia bunge la Uingereza siku ya Jumanne kwamba, Uingereza inawataka "marafiki zao katika Ikulu ya Marekani ya White House kutoyatupa makubaliano hayo".
Mwandishi: Sekione Kitojo /afpe
Mhariri: Grace Patricia Kabogo