1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Infantino: FIFA sio polisi ya dunia

Bruce Amani
20 Desemba 2016

Rais wa FIFA Gianni Infantino amefuta uwezekano wa kuipokonya Urusi kibali cha kuandaa Dimba la Kombe la Dunia 2018 kufuatia matokeo ya karibuni ya ripoti ya McLaren kuhusu dawa zilizopigwa marufuku michezoni

https://p.dw.com/p/2UY07
Schweiz Zürich - Fifa Präsident Gianni Infantino während "World Summit on Ethics and Leadership in Sports"
Picha: picture-alliance/dpa/W. Bieri

Infantino ameliambia gazeti la Ujerumani Der Spiegel kuwa FIFA sio polisi ya ulimwengu na sio polisi ya kupambana na matumizi ya dawa za kuongeza misuli nguvu duniani. Amesema mashirika ya kinidhamu yatashughulikia kitakachoibuka katika ripoti ya McLaren ambacho kitahusu kandanda. Rippto ya McLaren, ambayo sehemu ya pili ilitangazwa siku kumi zilizopita, ilifichua matumizi ya dawa za kuongeza misuli nguvu nchini Urusi kati ya 2011 na 2015 ambayo yaliwahusisha zaidi ya wanamichezo 1,000 katika michezo mbalimbali ikiwemo kandanda.

Chama cha Kandanda Nigeria kufanyiwa uchunguzi

Waziri wa michezo wa Nigeria Solomon Dalung ameamuru kuanzishwa uchunguzi kuhusu matumizi ya fedha za Shirikisho la Kandanda la nchi hiyo – NFF baada ya FIFA kusitisha ufadhili wake chama hicho. Dalung amesema inatia wasiwasi kuwa FIFA imesitisha ufadhili wa maendeleo kwa Nigeria kukisubiriwa uchunguzi wa namna msaada wa awali wa dola milioni 1.1 zilivyotumika. Waziri huyo ameitaka NFF kuiteua kampuni inayoheshimiwa kufanya ukaguzi wa mahesabu yao. Hata hivyo NFF imesisitiza kuwa rekodi zake za kifedha ziko sawa

Mwandishi: Bruce Amani/AP/Reuters/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga