1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

India yavunja rekodi

Mohammed Khelef
15 Februari 2017

Watu nusu milioni nchini India wameweka rikodi mpya ya dunia kwa kuimba wimbo wa taifa hilo katika wakati ambapo hisia kali za kizalendo zikizidi kujaa juu chini ya serikali inayofuata siasa kali za utaifa.

https://p.dw.com/p/2Xa6D
Indische Städte - Chennai
Picha: picture-alliance/U.S. Meschede

Kwa mujibu wa kitabu cha kumbukumbu cha Guiness, wimbo huo uitwao "Jana Gana Mana" uliimbwa na watu 509,261 mjini Gujarat, ambako ndiko anakotokea Waziri Mkuu Narendra Modi, wakati wa uzinduzi wa hekalu moja la Kihindu.

Wafuatiliaji mambo wanasema tukio hilo liliwavutia watu wapatao milioni moja, lakini ni nusu yao tu walioweza kuingia kwenye eneo hilo. Ingawa sherehe hiyo ilifanyika mwezi Januari, imeweza kuingizwa rasmi kwenye kitabu hicho cha kumbukumbu leo.

Mkusanyiko huu unavunja rikodi iliyowekwa na Bangladesh mwaka 2014, ambapo watu 254,000 walikutana kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Dhaka.

"Tunaona fahari kubwa kuweza kuweka rikodi hii, ambayo ni zaidi ya mara mbili ya rikodi ya mwisho," alisema Paresh Gajera, mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya sherehe hiyo.

Juhudi hizi za kujenga moyo wa utaifa zinakuja huku kukiwa na mjadala mkali juu ya namna wimbo huo wa taifa unavyotumiwa na serikali ya Modi kujenga taswira ya ukandamizaji dhidi ya wengine.

Mnamo mwezi Novemba, Mahakama ya Juu iliamua kwamba majengo yote ya sinema yanapaswa kuonesha wimbo wa taifa kabla ya filamu kuanza na watazamaji wanapaswa kusimama kwa heshima ya wimbo huo, uamuzi ambao ulizua hasira kubwa kutoka kwa watetezi wa haki za kiraia.

Kumekuwa na taarifa za watazamaji sinema kushambuliwa kwa kukataa kusimama, huku wengine wakikamatwa kwa kutoheshimu uamuzi huo wa mahakama.

Wakosoaji wanasema uhuru wa kujieleza unakandamizwa na chama cha Bharatiya Janata cha Modi kilichoingia madarakani mwaka 2014.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman