1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ILO: Wanawake bado wataabika kupata ajira

Daniel Gakuba
8 Machi 2018

Wakati Siku ya Wanawake Duniani ikiadhimishwa leo tarehe 08 Machi, Shirika la Kazi la Umoja wa Mataifa, ILO limeonya kuwa hatua katika kutoa fursa sawa za ajira kwa watu wa jinsia zote imekwama, na pengine inarudi nyuma.

https://p.dw.com/p/2tv80
USA Weinkellerei im Pahrump Valley produziert ersten Rotwein Nevadas
Picha: picture-alliance/dpa/B. Sweet

ILO imesema katika ripoti yake kwamba kwa wakati huu ni asilimia 48.5 ya wanawake wenye umri wa zaidi ya miaka 15 walio na ajira, na hiyo ni pungufu ya asilimia 26.5 ya wanaume walio katika umri huo, wanaoshiriki katika soko la kazi duniani. Kwa kila wanaume kumi walio na ajira, kuna wanawake sita tu, kulingana na ripoti hiyo.

Na pale wanawake wanapokuwa na kazi, kuna uwezekano mkubwa wa kuajiriwa katika sekta iso rasmi, ambayo ina malipo duni na usalama mdogo. ''Katika sehemu nyingi za dunia, wanawake ndio wanaokabiliwa na tatizo kubwa la kukosa kazi'', imesema ILO katika ripoti yake.

Mabadiliko yahitajika, tena haraka

Shauna Olney, mkuu wa kitengo cha usawa wa jinsia katika shirika la ILO, amesema hakuna maendeleo katika juhudi za kufikia usawa wa ajira.  ''Hali ni ya mkwamo, na hakuna dalili za mustakabali mwema'', amesema Olney na kutoa rai ya kuwepo mabadiliko makubwa, tena ya haraka kuhusu hali hiyo.

Burundi Landwirtschaft
Wanawake wengi hufanya kazi zisizo na malipo mazuriPicha: picture-alliance/Ton Koene

Afisa huyo aliyezungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, amesema kuwa miongoni mwa changamoto ambazo zimeendelea kuwakuma wanawake katika sekta ya ajira, ni kulipwa mishahara na ujira mdogo, ikilinganishwa na wenzao wanaume. Kulingana na shirika la kazi ulimwenguni, bado wanaume wanalipwa asilimia 20 zaidi ikilinganishwa na wanawake.

Changamoto nyingine ni kupandishwa vyeo na kuteuliwa katika nyadhifa za kuchukua maamuzi, licha ya hatua kubwa waliyopiga wanawake katika kupata elimu. Ikija katika suala la kutoa ajira, wanaume wenye uwezo wa kuwaajiri watu wengine, ni mara nne zaidi ya wanawake wenye uwezo kama huo.

Kiwingu mnamo siku za usoni

ILO imesema tangu mwaka 1990, pengo la ajira kati ya wanaume na wanawake limepungua kwa asilimia 2 tu, na maendeleo hayo yalifikiwa hadi mwaka 2009, na baada ya hapo hali ilianza kudorora, huku ikitarajiwa kuwa mbaya zaidi kati ya mwaka 2018 na 2021.

Afghanistan - Herat - Afghanische Frauen programmierten Computerspiel gegen Drogenkonsum
Maendeleo kielimu bado hayajasaidia kupunguza pengo la kijinsia katika nafasi za kaziPicha: DW/S. Tanha

Maeneo ambayo yanaongoza kwa tofauti kubwa kati ya wanawake na wanaume walioajiriwa ni nchi za Kiarabu Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika, na Ukanda wa Asia Kusini.

ILO inasema kwa hali isiotarajiwa, pengo la kijinsia katika nafasi za kazi ni dogo katika mataifa yanayoendelea. Katika nchi za Ulaya ''Mashariki na Amerika Kaskazini, idadi ya wanawake wasio na ajira ni ndogo hata kuliko ya wanaume'', limesema shirika hilo katika ripoti yake.

Ripoti hii imetolewa sambamba na maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, mnamo wakati vuguvugu la #MeToo, yaani, MimiPia, likipigia debe mjadala juu ya haki za wanawake, na kupinga unyanyasaji wa kijinsia.

Shauna Olney amesema mwezi Juni mwaka huu, ILO itapendekezwa kuwekwa kwa mkataba wa kimataifa dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia sehemu za kazi, ambao anasema unawakwaza wanawake wengi kupata ajira.

''Ikiwa mkataba huo utatiwa saini, utakuwa chachu muhimu ya maendeleo'', amesema afisa huyo wa ILO.

 

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe, rtre

Mhariri: Caro Robi