1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IEBC yashinda kesi nyingine dhidi yake

John Juma
24 Julai 2017

Mahakama kuu mjini Kisumu nchini Kenya imetupilia mbali kesi ya kuitaka tume huru ya mipaka na uchaguzi kushinikizwa kutangaza matokeo ya uchaguzi wa urais chini ya masaa saba

https://p.dw.com/p/2h4SK
Kenia Wahlen
Picha: Reuters/M. Eshiwani

Mahakama kuu mjini Kisumu nchini Kenya imetupilia mbali kesi ya kuitaka tume huru ya mipaka na uchaguzi nchini humo - IEBC kushinikizwa kutangaza matokeo ya uchaguzi wa uraisi chini ya masaa saba baada ya zoezi la kupiga kura kukamilika, kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Kesi hiyo ni mojawapo ya nyingine nyingi ambazo zimewasilishwa mahakamani na wanasiasa pamoja na wanaharakati, kuhusu mambo yanayotakiwa kufanyika kabla ya uchaguzi mkuu nchini humo wa tarehe nane mwezi Agosti  mwaka huu kufanyika.

Waliowasilisha kesi hiyo ambao ni kundi la vijana wa kujitegemea la Sumawa, kwa kunukuu ripoti ya tume ya Krieglar iliyochunguza fujo zilizozuka baada ya uchaguzi wa mwaka wa 2007, walikuwa wameelezea hofu yao kuwa kucheleweshwa kwa kuhesabiwa kwa kura, kunakiliwa na kutangazwa kwa matokeo huenda kukatoa mwanya wa udanganyifu wa kutumbukizwa karatasi za kura za ziada katika masanduku, hali inayoweza kuleta hofu na hata kuzua vurugu.

Kadhalika walisema kuwa kutokana na tume ya uchaguzi kujipatia vifaa vya kielektroniki vya kuhesabu kura, hakuna sababu yoyote ya kutoweza kuwasilisha matokeo hayo ya urais na hata mengine, saa chache baada ya kufungwa kwa vituo vya kupigia kura.

Jamaa akipiga kura wakati chama cha Jubilee kilipowateua wawaniaji wake mnamo mwezi Aprili 2017
Jamaa akipiga kura wakati chama cha Jubilee kilipowateua wawaniaji wake mnamo mwezi Aprili 2017Picha: Reuters/M. Eshiwani

Kulingana na taratibu mpya kila mtambo huo wa kielektroniki unaweza kutambua wapigaji kura wasiozidi 700 katika kila kituo.

Hata hivyo akitoa uamuzi wake jaji wa mahakama hiyo David Majanja, alisema kuwa katiba pamoja na sheria za uchaguzi haziitaki tume ya uchaguzi kutangaza matokeo ya kura ya uraisi kama wanavyotaka walalamishi. "Sioni uhusuiano uliopo kati ya malalamiko ya walalamishi na majukumu ya tume hii ya kuandaa uchaguzi."

Ni lazima ikumbukwe kuwa chini ya kipengele cha 249 cha katiba, tume ya uchaguzi ni tume huru ambayo haitakiwi kufuata uongozi au ushauri wa mamlaka yoyote isipokuwa katiba na sheria.

Kadhalika walalamishi wameshindwa kudhihirisha kuwa tume hii kulingana na katiba au sheria inatakiwa kutangaza matokeo ya awali katika kipindi cha masaa saba baada ya zoezi la kura kukamilika.

Mwanasheria wa wawasilishaji wa kesi hii Amondi alisema kuwa hatakata rufaa. "Kilio cha wapiga kura kimesikika na tume ya uchaguzi imeachiwa jukumu la kuhakikisha kuwa matokeo hayacheleweshwi."

Kesi hii ni kati ya nyingine nyingi zilizowasilishwa mahakamani kwa nia ya kuhakikisha kuwa uchaguzi unakuwa huru na wa haki.

Mwandishi: John Marwa

Mhariri: Yusuf Saumu