1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IEBC kumtangaza mshindi Kenya, Jumatatu

30 Oktoba 2017

Tume ya Kusimamia Uchaguzi nchini Kenya imekamilisha matayarisho ya kumtangaza mshindi wa uchaguzi mpya wa urais uliofanyika tarehe 26 mwezi huu.

https://p.dw.com/p/2mjVv
Kenia Wahl Annullierung Uhuru Kenyatta
Picha: Reuters/T. Mukoya

Rais Uhuru Kenyatta wa chama Jubilee anatarajiwa kutangazwa mshindi kwa asilimia 98 kwenye uchaguzi ambao hakuwa na ushindani mkubwa baada ya kiongozi wa upinzani Raila Odinga kujiondoa. Aidha kiongozi wa upinzani Raila Odinga anatarajiwa kutoa tamko lake kwa wafuasi wake Jumatatu pia.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi nchini Kenya Wafula Chebukati anatarajiwa kumtangaza Uhuru Kenyatta mshindi wa marudio ya urais uliosusiwa na upande wa upinzani licha ya kuwa majimbo manne ya eneo la Nyanza hayakupiga kura.

Wapinzani sita wa Kenyatta hawajafikisha asilimia mbili ya kura zilizopigwa. Katiba inaeleza kuwa majimbo yote ya taifa yanastahili kushirikishwa kwenye upigaji wa kura. Tangazo la Chebukati Jumatatu huenda likaibua hali ya taharuki zaidi hususan kwenye maeneo ya upinzani ambayo yameshuhudia makabiliano na maafisa wa polisi.

Ruto aishutumu upinzani kwa IEBC kushindwa kufanya kazi yake

Chebukati ameonekana kuchanganyikiwa kila mara anapohutubia waandishi habari kuhusu idadi ya wale waliojitokeza kupiga kura  Alhamisi juma lililopita. Kwenye ukurasa wa mtandao wake wa kijamii wa Twitter alisema kuwa asilimia 48 ya Wakenya walijitokeza kupiga kura hiyo ikiwakilisha Wakenya milioni 6.5 Hata hivyo alibadilisha tamko lake baada ya rais Uhuru Kenyatta kufikisha kura milioni 7.4.

Kenia Präsident William Ruto
Naibu rais wa Kenya William RutoPicha: Reuters/T. Mukoya

Akihojiwa na vituo vya kimataifa naibu wa rais William Ruto ameulaumu upinzani kwa Tume hiyo kushindwa kuendesha uchaguzi katika maeneo yao.

"Katika uchaguzi huu Wakenya milioni 6.7 walipiga kura, wale ambao hawakupiga kura waliamrishwa na upinzani. Kile tunachopinga ni Odinga kutumia makundi haramu kuzusha ghasia. Yeye alifaulu kushawishi asilimia 9 tu ya watu kutopitga kura," alisema Ruto.

Upande wa upinzani umeitisha kumtangaza Raila Odinga mshindi iwapo Chebukati atamtangaza Kenyatta mshindi, kwa kutumia matokeo ya mitambo ya uchaguzi wa tarehe nane mwezi wa nane.

Hatua hiyo huenda ikasababisha umwagikaji wa damu katika taifa ambalo lilishuhudia machafuko katika uchaguzi uliofanyika mwaka 2007 na kusababisha zaidi ya watu elfu moja kupoteza maisha yao.

NASA itamtangaza Odinga mshindi iwapo Kenyatta atapewa ushindi na IEBC

Kiongozi wa upinzani anatarajiwa kuhutubia wafuasi wake kuhusu kile wanachopaswa kufanya. Awali Odinga alinukuliwa akiwataka wafuasi wake wasusie baadhi ya bidhaa zinahusishwa na chama cha jubilee ili kuihujumu serikali kiuchumi. Kwa upande mwengine Wakili wa Muungano wa NASA, James Orengo ameishambulia serikali ya Jubilee.

Kenia Wahlwiederholung Raila Odinga
Kiongozi wa Upinzani NASA Raila OdingaPicha: picture-alliance/dpa/D. Bandic

"Akitumia uchaguzi huu wa tarehe 26 kujigamba kuwa yeye ni rais, sisi kama watu wa NASA tutatumia yale matokeo ya tarehe nane kwasababu wakifungua ile mitambo ya kutuma matokeo ni Raila ndiye aliyeshinda," alisema Orengo.

Wakati huo huo, ripoti ya shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International imethibitisha kuwa watu watatu waliuawa katika eneo pana la Nyanza wakati wa uchaguzi. Ripoti hiyo inasema kuwa jeshi la polisi lilitumia bunduki kuadhibu wakazi waliosusia uchaguzi wa urais.

Shirika hilo sasa linataka mamlaka ya huru ya kuchunguza utendaji kazi wa polisi inasstahili kuchunguza mauaji hayo na wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria. Shughuli zinaendelea katika jiji kuu la Nairobi ila watu wanawasiwasi kuhusu athari za tangazo la Chebukati.

Shisia Wasilwa, DW, Nairobi

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman