1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Taarifa ya Habari za Ulimwengu kutoka Idhaa ya Kiswahili ya DW

Habari | 31.05.2016 | 06:42

Majeshi ya Iraqi yaanza kuuvamia mji wa Fallujah forces begin storming IS-held city of Fallujah

Vikosi  maalum vya  jeshi  la  Iraq  maalum  kwa kupambana  dhidi  ya  ugaidi  vimeanza  kuingia  katika ngome  ya  kundi  la  Dola  la  Kiislamu  ya Fallujah jana.

Operesheni  hiyo  ya  kuwaondoa  wapiganaji  hao  katika mji  huo  , ulioko  kilometa  50 kutoka  mji  mkuu  wa  iraq Baghdad, inatarajiwa  kuwa  na  mapambano makali.

Kiasi  ya  wapiganaji  wa  jihadi 500 hadi  700 wamo  katika mji  huo, ambako  wanaaminika  kujenga  njia  za  chini  ya ardhi  na  kuficha  mabomu.

Mamia  kwa  maelfu  ya  raia  bado  wamekwama  katika mji  huo.

Jaribio la kurusha kombora lashindwa Korea kaskazini

Korea kaskazini imejaribu  kufyatua  kombora kutoka  pwani ya  mashariki mapema  leo  Jumanne asubuhi lakini jaribio hilo  linaonekana  kushindwa.

Maafisa  wa  kijeshi  wa  Korea kusini wameliambia  shirika la  habari  la  Reuters  kwamba  jaribio  hilo lilifanyika mapema  alfajiri  ya  leo.

Japan iliweka  jeshi  lake  katika  hali  ya  tahadhari  jana Jumatatu  kwa  ajili  ya  uwezekano  wa  Korea  kaskazini kurusha  kombora  hilo.

Hali  ya  wasi  wasi  katika  eneo  la  kaskazini  mashariki mwa  Asia  imekuwa  ya  juu  tangu  Korea  kaskazini kurusha  jaribio  lake  la  nne  la silaha  za  nyuklia  mwezi Januari  na  kufuatiwa  na  kurushwa  kwa  satalaiti  na majaribio ya  makombora  kadhaa.

Shirika  la  habari  la  Korea  kusini Yonhap  lilisema  kuwa Korea  kaskazini  inaonekana ilijaribu  kurusha  kombora  la Musudan la  masafa  ya  kati.

Dikteta wa zamani wa Chad Habre ahukumiwa kifungo cha maisha

Mahakama  nchini Senegal  jana  ilimhukumu  dikteta  wa zamani  wa  Chad Hissene Habre, kifungo  cha  maisha.

Dikteta huyo  wa  zamani  mwenye  umri  wa  miaka  73 alikuwa  akikabiliwa  na  madai  ya  uhalifu wa  kivita  na uhalifu dhidi  ya  ubinadamu wakati  wa  utawala  wake kuanzia  mwaka  1982  hadi 1980. makundi  ya  haki  za binadamu  yamemshutumu  Habre kwa  kuhusika  na  vifo vya  zaidi  ya  watu 40,000.

Habre  alikimbia  Chad  mwaka  1990 na  amekuwa  akiishi katika  mji  mkuu  wa Senegal , Dakar , tangu wakati  huo. Alikamatwa  mjini  Dakar  Julai  mwaka 2013.

NATO yawataka wanachama wake kuipinga Urusi

Katibu  mkuu  wa  NATO Jens Stoltenberg  amezitaka  nchi wanachama  kusimama kidete kwa  kile  alichoeleza  kuwa  ni hatua  ya  Urusi kuonesha  mabavu kijeshi .

Stoltenberg  alikuwa  akizungumza  jana  mjini  Warsaw , ambako alikuwa  akiweka msingi  wa  mkutano  wa  NATO  mwezi  Julai.

Amesema  jumuiya  hiyo  itajibu  shambulio  lolote dhidi  ya  nchi mwanachama .

NATO  ilivunja  mahusiano  na  Urusi  baada  ya  Urusi  kuikamata Crimea  mwaka  2014.

Kesi mjini Paris dhidi ya kundi la mtandao wa Jihadi

Watu  saba  wanaohusishwa  na  madai  ya  kuwa  katika mtandao  wa  kundi  la  Jihadi  wamefikishwa  mahakamani  mjini Paris.

Miongoni  mwao  ni Karim Mohammed -Aggad , kaka yake Foued Mohammed - Aggad , mmoja  kati  ya  washamabuliaji  wa kujitoa  muhanga  ambao  walishambulia ukumbi  wa  maonesho wa  Bataclan mjini  Paris  Novemba  13 mwaka  jana.

Washitakiwa  wanadai  walikwenda  Syria  kufanya  kazi  za kujitolea  mwaka  2013  na  walishawishiwa  kujiunga  na wanamgambo  wa  kundi  la  Dola  la  Kiislamu.

Walioishambulia ndege ya Somalia kwa mabomu wafungwa maisha

Mahakama  ya  kijeshi  nchini Somalia  jana  iliwahukumu kifungo cha maisha  watu  wawili  waliopatikana  na  hatia ya  kupanga  shambulio  la  bomu  dhidi  ya  shirika  la ndege la  nchi  hiyo  mwezi  Februari.

Kundi la itikadi  kali  la  al-Shabaab  lilidai  kuhusika  na shambulio  hilo dhidi  ya  ndege  ya  shirika  la  ndege  la Daallo, muda  mfupi baada  ya  kuruka  kutoka mji  mkuu Mogadishu. Mripuko  huo ulitoboa  tundu  katika  sehemu ya  ubavu  wa  ndege  hiyo na  mtu  mmoja  alifariki, ambaye  ni mshambuliaji wa  kujitoa  muhanga.

Ndege  hiyo  iliweza  hata  hivyo kutua  kwa  dharura.

Afisa  wa  zamani  wa  usalama  katika  uwanja  wa  ndege wa  Mogadishu alihukumiwa  pamoja  na  mtu  mwingine ambaye  alihukumiwa  akiwa  hayupo.

Mahakama  hiyo  pia  iliwahukumu   watu  wengine wanane kwa  kushiriki  katika  kupanga  shambulio  hilo.

Mashambulio dhidi ya majeshi ya Usalama Uturuki

Kiasi  watu wanne wameuwawa katika  shambulio  la bomu  lililofanywa  na  wapiganaji  wa  Kikurdi  kusini mashariki  mwa   Uturuki  jana. Hadi  watu  wengine  19 wamejeruhiwa.

Kundi  hilo  liliripua  bomu katika  mji unaoishi  Wakurdi wengi  wa  Silopi  wakati  gari  ya  polisi  ilipokuwa inapita. Katika shambulio jingine, mapema  jana  Jumatatu, polisi  wawili  waliuwawa  na  wa  tatu  alijeruhiwa   karibu na  mji  wa  mashariki  wa  Van.

Shambulio  hilo  limekuja  saa  chache  baada  ya  ndege za  kijeshi  za  Uturuki kushambulia  kambi inayomilikiwa na  kundi  la  wapiganaji  wa  chama  kilichopigwa marufuku  cha  PKK, kaskazini  mwa  Iraq.