1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya watu kufikia bilioni 8.5 mwaka 2030

30 Julai 2015

Idadi ya watu duniani inatarajiwa kufika watu bilioni 8.5 ifikapo mwaka 2030 na idadi hiyo kuongezeka hadi watu bilioni 9.7 ifikapo 2050 kutokana na kukua kwa idadi ya watu duniani hasa katika nchi za Afrika.

https://p.dw.com/p/1G7Ed
Picha: Getty Images

Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa hapo jana inakadiria kuwa idadi ya hivi sasa ya watu duniani ya bilioni 7.3 itaongezeka hadi watu bilioni 11.2 ifikapo mwaka 2100 yaani mwisho wa karne hii.

Nusu ya idadi ya watu duniani itapatikana kwa nchi tisa nazo ni India, Nigeria, Pakistan, Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, Ethiopia, Tanzania, Marekani, Indonesia na Uganda.

India itaipiku China kwa kuwa na watu wengi zaidi

Ifikapo mwaka 2022, idadi ya watu nchini India itaipiku ile ya China ambayo hivi sasa ndiyo iliyo na watu wengi zaidi duniani. India na China zina takriban watu bilioni moja kila mmoja hivi sasa nayo Nigeria itaipiku Marekani na kuwa nchi ya tatu duniani yenye watu wengi zaidi.

Watoto wachanga waliozaliwa mjini Leipzig
Watoto wachanga waliozaliwa mjini LeipzigPicha: picture-alliance/dpa

Nchi za Afrika zinatarajiwa kuwa na nusu ya idadi jumla ya watu duniani ifikapo mwaka 2050 kwani idadi ya watu katika nchi 28 barani humo inatarajiwa kukua mara mbili ya ilivyo hivi sasa katika kipindi cha miaka 35 ijayo.

Nchi kumi za Afrika Angola, Malawi, Mali, Niger, Somalia, Tanzania, Uganda, Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, Zambia na Burundi zinatarajiwa idadi ya raia wake itaongezeka mara tano ya ilivyo hivi sasa ifakapo mwaka 2100.

Mkuu wa kitengo cha kuhesabu idadi ya watu katika idara ya umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya kiuchumi na kijamii John Wilmoth amesema tangu mwaka 2003 kuna ongezeko la takriban watu bilioni moja duniani

Makadirio ya idadi yatasaidia katika mipango

Makadirio hayo ya idadi ya watu yanachangia pakubwa katika kuisaidia jumuiya ya kimataifa kutafuta njia za kupunguza kitisho cha kuongezeka kwa joto duniani na kutimiza malengo ya maendeleo kama kupambana dhidi ya umaskini na njaa.

Wanawake wakiwa wamepanga foleni India
Wanawake wakiwa wamepanga foleni IndiaPicha: Reuters

Wilmoth amesema licha ya kuwa makadirio hayo hayapaswi kuzua wasiwasi, ni muhimu kutambua kuwa kuendelea kuongezeka kwa watu, hasa katika nchi maskini kunafanya juhudi za kukomesha umaskini, njaa, ujinga, kutolewa huduma bora za afya na kufikia usawa kuwa mambo magumu kuyafikia wakati ambapo mikakati inawekwa kuanza kutekelezwa kwa malengo ya maendeleo endelevu ifikapo mwezi Septemba mwaka huu.

Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa pia inagusia idadi ya watu wazee duniani. Ifikapo mwaka 2050 idadi ya watu walio zaidi ya umri wa miaka sitini inatarajiwa kuwa mara mbili ya hivi sasa huku bara Ulaya likitarajiwa kuongoza kwa asilimia 34. Mara ya mwisho Umoja wa Mataifa ulitoa data hizo za kuonyesha idadi ya watu na makadirio ya idadi hiyo katika siku za usoni ilikuwa mwaka 2010.

Mwandishi: Caro Robi/dpa/ap/Reuters

Mhariri: Elizabeth Shoo