1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya watoto wanaozaliwa nchini Ujerumani yaongezeka

Sekione Kitojo30 Desemba 2010

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanazungumzia zaidi kuhusu ongezeko la watoto nchini Ujerumani, shambulio la kigaidi huko Denmark na nafasi ya Palestina kujitangazia taifa lao huru.

https://p.dw.com/p/zrTM

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo wamezungumzia zaidi kuhusu ripoti inayoeleza kuwa watoto sasa wanaongezeka, pia kuna suala la shambulio la kigaidi, pamoja na nafasi ya Palestina kujitangazia taifa lao mwezi ujao.

Tukianza na gazeti la Westdeutsche Zeitung la mjini Düsseldorf, kuhusiana na mada ya ongezeko la idadi ya watoto nchini Ujerumani , gazeti linaandika.

Ujerumani inahitaji watoto, ambao hapo baadaye watafanyakazi katika nchi hii na kuweza kutumia uwezo wao maalum katika masuala ya sayansi, biashara na kazi za mikono. Ni muhimu kwa hiyo kuzuwia hali iliyopo sasa ya kuporomoka kwa hali ya maisha na kuwaingiza watu katika mtindo wa kupokea mafao tu ya kijamii, na hii itakuwa ni mageuzi muhimu katika mwaka 2011.

Nalo gazeti la Berliner Morgenpost likizungumzia mada hiyo linaandika:

Fedha zinazotolewa kwa ajili ya watoto na serikali ni kichocheo kikubwa cha ongezeko la idadi ya watoto waliozaliwa nchini Ujerumani mwaka huu. Hii ni changamoto kubwa kwa wazazi, ambayo hakuna mwanasiasa, mkuu ama daktari anaweza kuibeba. Ni muda mrefu umechukua hadi pale wanawake sasa nchini Ujerumani wanajiamini, kwamba wanawajibu wa kujenga msingi wa familia. Kwa kuwa hapo kabla walifikiri kuwa wanapaswa kufikia umri wa miaka 40 ndipo wapate mtoto wao wa kwanza. Na hata wanaume wanapata hamu ya kuwa na familia katika umri mkubwa, na mara nyingi hamu hiyo haipo kabisa. Ikitokea kwamba baba anapata mtoto katika umri mkubwa, inamuwia vigumu kufahamu jukumu lake kama baba wa kisasa, ama hafahamu kabisa. Iwapo kutakuwa na mjadala zaidi , itakuwa rahisi kupata suluhisho la jukumu hilo na la haraka. Na idadi ya watoto itaongezeka na itakuwa ni kawaida.

Gazeti la Badische Neueste Nachrichten la mjini Karlsruhe linaandika kwamba Ujerumani inawajibika kuwatunza watoto wengi zaidi hivi sasa wakati huu wa matatizo ya kiuchumi na kifedha duniani. Mhariri anaendelea:

Huenda pengine ni ishara, kwamba familia hizi zenye watoto wadogo, zitaendelea kupambana na matatizo ya haya na kuyashinda.

Likitubadilishia mada gazeti la Neue Presse la mjini Hannover linazungumzia shambulio la kigaidi huko nchini Denmark. Gazeti linaadika.

Bara la Ulaya linamulikwa zaidi na Waislamu wenye imani kali. Kwa muda mrefu wanaishi katika bara hili watu wenye mtazamo wa kijihad miongoni mwetu. Watu hawa wamezaliwa hapa, wamekwenda shule katika bara hili na hadi vyuo vikuu, wanaufahamu mfumo wa kijamii wa Ulaya, bila ya wao kupata ishara za maadili ya kuvumiliana pamoja na uhuru wa vyombo vya habari. Kinyume chake wamejiingiza katika hali ya hatari baina ya kujihisi dhalili na imani kali ya kidini.

Nalo gazeti la Frankfurter Rundschau, linazungumzia kuhusu nafasi ya Palestina kujitangazia taifa lao. Gazeti linaandika.

Mwishoni mwa Januari, Wapalestina watawasilisha azimio katika umoja wa mataifa kutaka kutambuliwa rasmi taifa lao, na kusitisha ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi yao. Marekani italazimishwa kukubali. Iwapo itapinga itajiweka katika hali mbaya. Kujitangazia uhuru hata hivyo hakutatua mzozo huo na kutaongeza tu hatari mpya ya kiusalama. Kutofanya hivyo pia kutaleta hatari zaidi.

Hayo ni maoni ya wahariri wa magazeti ya hapa Ujerumani kama mlivyokusanyiwa na Sekione Kitojo.

Mwandishi : Sekione Kitojo / Inlandspresse

Mhariri: Josephat Charo.