1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya watoto wanaokufa kwa ukimwi yaongezeka

29 Novemba 2013

Idadi ya watoto walio na umri kati ya miaka 10 na 19 wanaokufa kutokana na ukimwi duniani imeongezeka kufikia asilimia 50 kati ya mwaka 2005 na 2012.

https://p.dw.com/p/1AQe2
Nyongeza ya ufadhili yahitajika kusaidia tatizo hilo-UNICEF.
Nyongeza ya ufadhili yahitajika kusaidia tatizo hilo-UNICEF.Picha: picture-alliance/dpa

Ripoti iliyotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia watoto-UNICEF imesema hali hiyo sasa ni ya kutisha na mpango wa haraka unahitajika kukabiliana na hilo, sambamba na kuongeza misaada kutatua tatizo hilo.

Ripoti hiyo imesema kuwa idadi ya watoto 71,000 walio na umri kati ya miaka 10 na 19 walifariki kutokana na ukimwi mwaka 2005, ambapo idadi hiyo ya vifo imeongezeka kufikia watoto 110,000 mwaka 2012, hali iliyoelezwa kuwa ni kutokana na kukosekana kwa vifaa vya upimaji na ushauri nasaha miongoni mwa vijana.

Kati ya vijana hao, ripoti hiyo imesema kuwa karibu asilimia 90 wanatoka katika nchi 22 duniani kote, lakini wengi kutoka katika Jangwa la Sahara.

Dola bilioni 5.5 zahitajika

Kutokana na matokeo ya utafiti huo, shirika hilo la UNICEF limesema kunahitajika nyongeza ya ufadhili wa dola bilioni 5.5 za Marekani ifikapao mwaka 2014, kwa ajili ya kusaidia kuwakinga watoto milioni 2 wasiambukizwe virusi vya Ukimwi katika miaka ijayo.

Wastani wa watoto milioni 2.1 walikadiriwa kuwa wanaishi na virusi vya Ukimwi duniani kote mwaka 2012.

Mkurugenzi wa shirika hilo, Anthony Lake anasema kwa sasa kunahitajika mpango wa haraka kuwafikia watoto ambao wapo hatarini zaidi kuambukizwa na kuwa mpango thabiti utakaoingilia kati hali hiyo utasiaidia katika kuleta matokeo mapya na kuibua maambukizi mapya ifikapo mwaka 2020.

Maambukizi toka kwa mama kwenda mtoto yapungua

Kwa upande wa watoto wachanga, ripoti hiyo imeleta matokeo chanya, ambapo idadi ya vifo vya watoto wachanga wanaofariki kutokana na kuambukizwa virusi vya HIV kutoka kwa mama zao, imepungua kutoka vifo 540,000 mwaka 2005, kufikia vifo 260,000 mwaka 2012, kutokana na mpango wa kinga kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wa kuwakinga watoto wasiambukizwe virusi wanapozaliwa na wanawake wanaoishi na virusi vya ukimwi, na ule wa kuwazuia kunyonya.

Mpango wa kuzuia kunyonyesha umesaidia kupunguza maambukizi.
Mpango wa kuzuia kunyonyesha umesaidia kupunguza maambukizi.Picha: imago/blickwinkel

Kwa hatua hiyo, mkurugenzi huyo wa UNICEF amepongeza juhudi zinazofanywa kuwaokoa watoto wanaozaliwa na kusema kuwa dunia sasa inashuhudia mafanikio ya kufikia taifa litakalokuwa huru dhidi ya maradhi ya ukimwi na watoto wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kunufaika na mafanikio hayo, na kuwa wa mwisho kunapotokea mapungufu.

Katika hatua nyingine, shirika la Afya duniani-WHO-limesema kuongezeka kwa idadi ya vijana wanaofariki kwa ukimwi ni kwa sababu ya kukosekana kwa huduma bora za afya miongoni mwa vijana, hasa kwa sababu hakuna huduma zinazowalenga vijana moja kwa moja.

Vijana wanahitaji kufuatiliwa kwa karibu

Mkurugenzi wa kitengo cha afya kinachoshughulikia maradhi hayo katika shirika hilo, Gottfried Hirnschall, amesema vijana wanahitaji huduma maalum za afya na ufuatiliaji wa karibu wa mahitaji yao kiafya.

Watoto kati ya miaka 10 na 19 wapo hatarini zaidi kuambukizwa.
Watoto kati ya miaka 10 na 19 wapo hatarini zaidi kuambukizwa.Picha: UNICEF

Anasema nchi zilizopo katika ukanda wa Jangwa la Sahara zinaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya maambukizi, lakini ni asilimia 10 tu ya vijana wa kiume na asilimia 15 ya wasichana wanaofahamu juu ya hali zao kiafya ikiwa wameambukizwa virusi vya HIV au hawajaambukizwa, na kutoa ushauri mbali mbali, ikiwemo vijana hao kupimwa bila idhini ya wazazi wao, matumizi ya kondom na dawa za kuongeza muda wa kuishi.

Mwandishi: Flora Nzema/DPAE

Mhariri: Saumu Yusuph Mwasimba