ICTR yamhukumu Nizeyimana kifungo cha maisha | Matukio ya Afrika | DW | 19.06.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

ICTR yamhukumu Nizeyimana kifungo cha maisha

Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) imemhukumu kifungo cha maisha jela afisa wa mwisho wa jeshi la Rwanda kuwahi kushitakiwa na mahakama hiyo, Kapteni Idelphonse Nizeyimana kwa maujai ya Rwanda.

Kapteni Idelphonse Nizeyimana.

Kapteni Idelphonse Nizeyimana.

Kapteni Nizeyimana ni afisa wa 15 na mwisho kuwahi kushitakiwa na kuhukumiwa na mahakama hii tangu kuanzishwa kwake miaka zaidi ya 17 iliyopita kwa ajili ya kushughulikia kesi za vigogo na wenye madaraka makubwa mwaka 1994 nchini Rwanda na ambao walishiriki kwenye mauaji ya kimbari.

Kati ya maafisa hao 15 wa jeshi, 14 walitiwa hatiani ambapo afisa mmoja pekee, Bragadia Jenerali Gratien Kabiligi aliyekuwa Mkuu wa Operesheni za Kijeshi nchi humo aliachiwa huru.

Katika hukumu ya jana Jaji Lee Muthoga aliyekuwa anaongoza jopo la majaji watatu, alitamka adhabu hiyo baada ya kumtia hatiani Kapteni Nizeyimana kwa kuamuru mauaji ya kimbari, kuteketeza kizazi na mauaji kama ukatili dhidi ya binadamu katika maeneo mbalimbali mkoani Butare, Kusini mwa Rwanda mwezi Aprili, 1994.

Lakini kufuatia hukumu hiyo, John Philpot, Wakili Kiongozi wa Kapteni Nizeyimana aliiambia DW muda mfupi baada ya kutolewa kwake kuwa watakata rufaa "kwani ushahidi uliotolewa kwa kiasi kikubwa ulikuwa umepangwa kutoka nchini Rwanda.''

Maafisa kadhaa wa jeshi la Rwanda watiwa hatiani

Jopo la majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kwa Rwanda (ICTR).

Jopo la majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kwa Rwanda (ICTR).

Ukimtoa Kapteni Nizeyimana, maafisa wengine wa jeshi waliotiwa hatiani ni pamoja na Mnadhimu Mkuu wa zamani wa Jeshi, Jenerali Augustin Bizimungu na aliyekuwa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Polisi, Jenerali, Augustin Ndindiliyimana.

Wengine katika orodha hiyo ni maluteni Kanali Tharcise Muvunyi na Anatole Nsengiyumva pamoja na Meja Francois-Xavier Nzuwonemeye na Kapteni Innocent Sagahutu.

Makamanda wengine wawili wa Jeshi la Rwanda ambao bado wanasakwa vikali na Mahakama hiii ni pamoja na Meja Protais Mpiranya, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Walinzi wa Rais na Luteni Kanali Pheneas Munyarugarama aliyekuwa kamanda wa kambi ya jeshi ya Gako katika mkoa wa Kigali Vijijini.

Hata hivyo maafisa hao pindi wakitiwa mbaroni, kesi zao hazitasikilizwa tena na Mahakama hii ya Umoja wa Mataifa bali nchini Rwanda ambako watuhumiwa wa mahakama hiyo ambao hajawakamatwa watakuwa wanapelekwa au nchi nyingine watakakoyopangiwa kusikilizwa kwa kesi zao.

Kuanzia Julai Mosi, mwaka huu, Chombo Maalum kilichoundwa na Umoja wa Mataifa kurithi kazi za ICTR, kijulikanacho kama Residual Mechanism (IRM) kitaanza kazi rasmi na miongoni mwa majukumu yake ni pamoja na kufuatilia washitakiwa tisa ambao hajawajitiwa mbaroni wakiwemo maafisa hao wawili wa jeshi.

Hivi sasa mahakama hii ya Umoja wa Mataifa imebakiwa na kesi moja tu ambayo ipo katika hatua za mwisho kabla ya kupangiwa tarehe ya hukumu inayomhusu aliyekuwa Waziri wa Mipango wa Rwanda, Augustin Ngirabatware.

Mwandishi: Nicodemus Inkonko/DW Arusha
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman