1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ibada ya Hajj yaanza.

25 Novemba 2009

Ibada ya kila mwaka ya Hajj, imeanza rasmi leo mjini Mecca. Kiasi cha milioni mbili na laki tano ya Waislamu, wamekusanyika mjini Mecca, kutekeleza ibada hiyo.

https://p.dw.com/p/KfNq
Milioni mbili ya Waslamu wako Mecca kwa ibada ya Hajj.Picha: AP

Hajj ya mwaka huu pia inafanyika wakati kuna wasiwasi wa kusambaa kwa homa ya nguruwe, ambayo tayari imewaua mahujaji wanne.

Jana ndio ilikuwa siku ya mwisho ya mahujaji kuwasili katika mji wa Mecca, tayari kwa kuanza rasmi kwa ibada ya hajj leo hii. Waislamu kutoka kila pembe ya dunia, wa tabaka mbali mbali, wakubwa kwa wadogo, wanawake kwa wanaume wamemiminika mjini Mecca, kutekeleza ibada hii ya Hajj ambayo ni nguzo moja kati ya nguzo tano za dini ya kiislamu. Na kila muislamu mwenye uwezo na afya njema anawajibika kufika kutekeleza ibada ya Hajj angalau mara moja maishani.

BdT Hajj Mina
Bonde la Jamarat, huko Mina, Mahujaji wanaporusha vijiwe kumpiga shetani.Picha: AP

Ibada ya mwaka huu hata hivyo, imezongwa na wasiwasi wa maambukizi ya homa ya nguruwe. Tayari mahujaji wanne wamefariki kutokana na kuambukizwa virusi vya homa hiyo ya nguruwe. Serikali ya Saudia Arabia hata hivyo imesema imechukua tahadhari zote na hakuna hofu ya kusambaa kwa virusi vya homa hiyo.

Hajj inaanza rasmi leo, kwa ile ibada ya tawaf, ambayo ukipenda ni zoezi la kuzunguka Kaaba mara saba- Kaaba ni jengo la mraba lililokati kati mwa msikiti mkuu mjini Mecca, na ni eneo ambalo waislamu kote duniani huelekeza wanapotekeleza ibada zao tano za sala kila siku.

Mahujaji baadaye wataelekea huko Mina, watakakokaa usiku kabla ya kuamkia kupanda mlima Arafa, hapo kesho. Arafa ndio eneo mtume Muhammad alipotoa risala zake za mwisho. Amina Abdalla anatoka nchini Kenya, amefika Hajj mwaka huu, anasema,

'' Najisikia nimepata bahati kubwa kwamba mimi ni mmoja kati ya milioni mbili ya Waislamu waliofika Mecca mwaka huu kutekeleza Ibada ya Hajj. Nimetoka nchini Kenya, na kiasi cha wakenya 2000 wako hapa Mecca kwa Ibada hii ya Hajj. Najisikia kwamba huu sio ufanisi wangu bali Mwenyezi Mungu ndio ameniwezesha.''

Saudi Arabien Hajj Soldaten Flash-Galerie
Maafisa wa Usalama Saudia Arabia, wanaimarisha usalama wakati wa Hajj.Picha: AP

Huku ibada ya Hajj ikiendelea, mafundi walikuwa bado wanaendeleza ukarabati wa kupanua sehemu za msikiti mkuu kutoa nafasi zaidi kwa mahujaji. Msikiti huo mkuu wa sasa una uwezo wa kuingia watu milioni moja.

Sehemu zingine ambazo zimepanuliwa ni ile njia inayoelekea katika milima ya Safa na Marwa. Ni wakati wa kupanda safa na Marwa ndio mara kwa mara imegeuka kuwa eneo la mkasa, mahujaji wanapokanyagana, wanapokuwa wanapanda na kushuka milima hiyo miwili.Mwaka wa 2006, mahujaji 364 walikufa kwa kukanyagwa katika bonde la Jamarat huko Minna, katika siku ya mwisho ya kutekeleza ile ibada ya kurusha vijiwe, mithili ya kumpiga shetani. Kuzuia visa hivi, serikali ya Saudia imejenga daraja la ngazi tano, kutoa nafasi ya watu kufanya safwa na Marwa bila ya msongamano mkubwa.

Usalama pia umeimarishwa vilivyo, zaidi ya laki moja ya maafisa wa usalama wamesambazwa kote katika maeneo Hajj inafanyika.

Mwandishi: Munira Muhammad/ AFPE

Mhariri: Abdul-Rahman.