1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ibada kuwakumbuka wahanga wa Germanwings

17 Aprili 2015

Watu wapatao 1,500, wakiwemo 500 kutoka familia za wahanga wa ajali ya ndege ya Germanwings, wameshiriki katika ibada mjini Cologne kuwakumbuka wahanga hao. Pia bendera zilipepea nusu mlingoti kote Ujerumani.

https://p.dw.com/p/1F9s4
Madhabahu ya kanisa la jimbo kuu la Cologne ilikofanyika ibada hiyo
Madhabahu ya kanisa la jimbo kuu la Cologne ilikofanyika ibada hiyoPicha: AFP/Getty Images/O. Berg

Kengele zililia kote mjini Cologne mchana wa leo (Ijumaa) kuashiria kumbukumbu ya wahanga hao 150 waliopoteza maisha katika ajali ya ndege ya shirika la Germanwings namba 4U9525.

Viongozi mbali mbali wameshiriki katika ibada hiyo, wakiwemo Kansela wa Ujerumani Nagela Merkel, Rais wa Ujerumani Joachim Gauck, na Waziri Mkuu wa Jimbo la North Rhine Westphalia Hannelore Kraft.

Kansela Angela Merkel na rais Joachim Gauck ni miongoni mwa viongozi walioshiriki katika ibada hiyo
Kansela Angela Merkel na rais Joachim Gauck ni miongoni mwa viongozi walioshiriki katika ibada hiyoPicha: Getty Images/S. Schuermann

Waziri wa usafirishaji wa Ufaransa, Alain Vidalies na waziri wa mambo ya ndani wa Uhispania Jorge Fernandez Diaz pia wamehudhuria ibada hiyo. Ndege iliyopata ajali ilikuwa ikisafiri kutoka mjini Barcelona nchini Uhispania, na ilipata ajali kusini mwa Ufaransa. wajerumani 72 na wahispania 50 ni miongoni wa waliouawa katika ajali hiyo iliyotokea tarehe 24 Machi.

Nguvu za upendo

Ibada hiyo iliongozwa na mkuu wa jimbo kuu katolika la Cologne Kadinali Rainer Maria Woelki, na mwenyekiti wa kanisa la kiprotestanti katika eneo la Westphalia, Annette Kurschus.

Katika ujumbe wake Kadinali Woelki amesema ''Upendo una nguvu kuliko kifo'', naye rais wa Ujerumani Gauck akasema taifa la Ujerumani bado linaghubikwa na ajali hiyo ya mwezi uliopita. Muziki wa huzuni uliambatana na ibada hiyo kuzifariji familia zilizopoteza wapendwa wao.

Kote nchini Ujerumani, bendera zimepeperushwa nusu mlingoti kuomboleza vifo vya watu hao wanaokumbukwa leo.

Maua na mishumaa kuwakumbuka waathiriwa

Waombolezaji wameruhusiwa kuacha maua na mishumaa katika ngazi za kanisa hilo la Cologne na nje ya kituo kikuu cha reli cha mji huo kilicho karibu na kanisa hilo. Mishumaa 150 iliyowashwa mbele ya madhabahu iliwakilisha watu wote waliokuwa katika ndege hiyo aina ya Airbus chapa A-320.

Watu wengine walifuata ibada wakiwa katika uwanja wa kanisa la Cologne
Watu wengine walifuata ibada wakiwa katika uwanja wa kanisa la ColognePicha: Reuters/S. Schuermann

Ndege hiyo ya shirika la Germanwings ambalo ni shirika tanzu la Shirika la ndege la Ujerumani, Lufthansa ilikuwa inatoka Barcelona kuelekea Duesseldorf mnamo tarehe 24 mwezi Machi wakati, kulingana na maoni ya wachunguzi, ilipoangushwa kwa makusudi na msaidizi wa rubani Andreas Lubitz aliyekuwa na maradhi ya msongo wa mawazo baada ya kumfungia nje ya chumba cha rubani rubani mkuu.

Ibada ya kuashiria umoja wa kitaifa

Jamaa za waathiriwa awali walikuwa wamefanya misa nyingine ya makumbusho karibu na eneo la mkasa katika kijiji cha Le Vernet nchini Ufaransa.Mnamo tarehe 13 mwezi huu mawaziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Uhispania na Ufaransa walitoa rambi rambi zao katika uwanja wa ndege wa Barcelona.

Wachunguzi katika milima ya Ufaransa wakitafuta mabaki ya ndege ya Germanwings
Wachunguzi katika milima ya Ufaransa wakitafuta mabaki ya ndege ya GermanwingsPicha: picture-alliance/dpa

Wanasaikolojia wanasema kuja pamoja kwa jamii ya wajerumani kuomboleza na kuwakumbuka waliofariki katika ajali hiyo ni ishara ya umoja wa kitaifa na italeta faraja.

Profesa wa masuala ya saikolojia katika chuo kikuu cha Leipzig Immo Fritsche amesema wajerumani wameungana tangu kufichuliwa kuwa ajali hiyo ilisababishwa na masidizi wa rubani na kisa hicho kinahitaji watu kuwa na hakikisho kuwa kuna haja ya kujizuia kufanya vitendo vitakavyowadhuru wengine na hasa jamii inataka kuwa na hali ya kuamini tena kuwa walio na udhibiti wa vyombo kama ndege wanaweza kutegemewa na wanajali usalama wao.

Mwandishi:Caro Robi/afp/dpa

Mhariri: Gakuba Daniel