1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Human Rights Watch yailaumu serikali ya Zimbabwe kwa kuwaandama wapinzani

Othman, Miraji17 Juni 2008

Shirika la Human Rights Watch linalalamika namna upinzani unavyokandamizwa na serekali huko Zimbabwe.

https://p.dw.com/p/ELki
Morgan Tsvangirai, kiongozi wa Chama cha upinzani cha MDC cha Zimbabwe ( kushoto) na Rais Robert Mugabe wa nchi hiyo.Picha: AP

Hali inayozidi ya kuwakandamiza viongozi wa upinzani na jumuiya zisizokuwa za kiserekali katika Zimbabwe ni ushahidi zaidi kwamba uchaguzi wa marudio wa urais hapo Juni 27 hautokuwa huru na wa haki. Hayo yamesemwa na Shirika la kupigania haki za binadamu duniani, Human Rights Watch.

Wakaguzi wa uchaguzi kutoka Jumuiya ya Maendeleo ya Kiuchumi ya Kusini mwa Afrika, SADC na wale wa Umoja wa Afrika, AU itawabidi wachunguze na kutoa taarifa hadharani juu ya vitendo vinavokwenda kinyume na uutu ambavyo vinaendeshwa na chama tawala cha ZANU-PF cha Rais Robert Mugabe. Georgette Gagnon mkurugenzi wa Afrika wa Shirika la Human Rights Watch, amesema serikali ya nchi hiyo mwanzoni iliwaandama wanachama wa vyama vya upinzani na sasa inawakamata viongozi wa vyama hivyo. Hilo ni jaribio jingine wazi la Rais Mugabe kuuteka nyara uchaguzi huo. Aliuliza wapi hali ya kuenea vitendo hivyo visivokuwa vya kisheria itaishia?

Kukamatwa mara tatu

Juni 12, polisi wa Zimbabwe walimkamata kiongozi wa Chama cha MDC, Morgan Tsvangirai kwa mara ya tatu mnamo siku nane ikiwa ni jaribio lililo wazi la kuchafua kampeni yake kabla ya uchaguzi. Polisi walimzuwia katika kizuizi cha njiani huko Kwekwe na kumweka ndani kwa zaidi ya saa mbili. Baada ya kuachwa huru Tsvangirai alielekea Gweru ambako huko alikamatwa na kuwekwa ndani pamoja na wasaidizi wake kwa saa mbili kabla ya kuachwa huru bila ya kushtakiwa.

Pia Juni 12, polisi walimkamata katibu mkuu wa MDC, Tendai Biti katika kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Harare alipowasili kutokea Afrika Kusini. Polisi walisema wanataka kumshtaki Bwana Biti kwa tuhuma za uhaini, kwa vile alimtangaza Morgan Tsvangirai kuwa mshindi wa chaguzi za Machi 29 kabla ya matokeo kutolewa rasmi. Ameshikiliwa katika mahala pasipotajwa na hajaruhusiwa kuonana na wakili.

Bi Gagnon alisema tuhuma za uhaini dhidi ya Tendai Biti ni jaribio jingine lililo na mizengwe kutoka upande wa serekali ili kuwazuwia viongozi wa MDC wasiweze kufanya kampeni. Pia kushindwa kusema wapi anakoshikiliwa mpinzani huyo ni jambo linalotia wasiwasi na kwamba inabidi aachiliwe huru mara moja.

Mnamo siku chache zilizopita polisi kinyume na sheria imewakamata wanaharakati kadhaa wa jumuiya za kiraia na kuzilazimsha jumuiya kadhaa zisizokuwa za kiserekali kusitisha shughuli zao.

Juni 11 polisi waliziamuru jumuiya kadhaa zisizokuwa za kiserikali kufungwa kutokana na barua ya waziri wa utumishi wa serekali, kazi na ustawi wa jamii, Nicholas Goche akipiga marufuku kusambazwa misaada ya vyakula kutoka jumuiya hizo.

Bi Gagnon wa Human Rights Watch amesema usumbufu unaofanywa na serikali, vitisho na kuwakamata maafisa wa jumuia za kiraia havidhuru tu makundi hayo, lakini watu wote wanaotegemea makundi hayo kwa vyakula na misaada mingine. Hali hii ya ukandamizaji na hofu inayoenzwa ni maafa kwa Wa-Zimbabwe wote.

Mateso yakome

Mashambulio dhidi ya jumuiya za kiraia na upinzani ni hali ya karibuni iliojitokeza katika kampeni inayoendelea ya serikali ya ZANU-PF kueneza hofu miongoni mwa watu waliokipigia kura chama cha upinzani cha MDC katika uchaguzi wa Machi 29. Shirika la Human Rights Watch katika taarifa yake limesajili vitendo vya mateso na vifo vya zaidi ya watu 36 katika ghasia zilizosababishwa na siasa.

Shirika hilo limeihimiza Jumuiya ya Maendeleo ya Kiuchumi Kusini mwa Afrika, SADC na wakaguzi wa AU watoe taarifa kila wakati na hadharani kuhusu uhalifu wote unaosababishwa na siasa pamoja na vitendo vinavokwenda kinyume na haki za binadamu wakati wa kampeni za uchaguzi ili kuhakikisha kwamba walio na dhamana ya vitendo hiyvo wanawajibika. Pia Jumuiya ya SADC na wakaguzi wengine lazima wachunguze kama uchaguzi huo wa marudio unaambatana na vipimo na muongozo wa SADC juu ya kuendeshwa chaguzi pamoja na vipimo vingine vya kimataifa kuhusu chaguzi.