1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hugo Chavez ataka mhula wa rais usiwekewe kikomo

Oummilkheir16 Agosti 2007

Rais wa Venezuela amepania kutia njiani ndoto ya kubuni " ujamaa wa mafuta"na kukomesha mitindo ya zamani ya kuchimba na kusafirisha mafuta

https://p.dw.com/p/CH9T
Rais Hugo Chavez akihutubia bungeni
Rais Hugo Chavez akihutubia bungeniPicha: AP

Rais Hugo Chavez wa Venezuela amependekeza katiba ifanyiwe marekebisho na kufutiliwa mbali kifungu cha sheria kinachopiga marufuku mhula wa rais kupindukia mara mbili.

Na mhula wenyewe pia wa miaka sita anataka urefushwe kwa mwaka mmoja.Kwa upande mwengine rais huyo wa Venezuela ametangaza mpango wa mageuzi unaowekea kikomo uhuru wa benki kuu katika kujipitishia maamuzi na kumfungulia njia kiongozi wa taifa ya kukagua akiba ya sarafu za kigeni.

Akihutubia bunge linalodhibitiwa kikamilifu na wafuasi wa chama chake,rais Hugo Chavez amesema “hamshangazi yeyote” kwa kutaka kubadilisha kifungu nambari 230 cha katiba kinachomtaka rais asisalie madarakani kwa zaidi ya mihula miwili.

Azma ya Chavez ya kufutilia mbali muda wa mihula - kuweza kusalia madarakani - kuendeleza “siasa yake ya mapinduzi angalao hadi mwaka 2021 na kujenga “ujamaa wa karne ya 21”-ilikua ikijulikana,lakini jana usiku ameipamba kwa kushauri mhula huo urefushwe kwa mwaka mmoja na kua miaka sabaa.

Kwa kuchaguliwa upya mwezi December uliopita,kwa mhula wa pili wa miaka sita,Hugo Chavez alikua ang’atuke madarakani mwaka 2013.

Upande wa upinzani uliosusia uchaguzi wa bunge mwaka 2005,umekosoa kile walichokiita “miradi ya kifashisti” yenye lengo kwa maoni yao ya kuleta aina ya utawala unaolingana na ule wa Cuba nchini Venezuela.Rais Hugo Chavez alipinga pendekezo la upande wa upinzani la kuundwa kamisheni maalum kujadili masuala yanayohusiana na mageuzi ya katiba.

Katika hotuba yake jana usiku bungeni,rais Chavez amezisuta kwa mara nyengine tena lawama za upande wa upinzani akisema tunanukuu:”wananituhumu kuandaa njama ya kutaka kusalia milele madarakani,au kutaka kudhibiti madaraka,sote tunajua huo ni uwongo mtupu”.Mwisho wa kumnukuu rais huyo wa Venezuela.

Mapendekezo yake ya mageuzi yanavihusu vifungu 33 kati ya 350 vya katiba-kwa maneno mengine,asili mia kumi ya katiba ambayo ameshaifanyia marekebisho katika mwaka 1999.Yana nafasi nzuri ya kuidhinishwa bila ya shida bungeni kwasababu viti vyote 167 vinakaliwa na wabunge watiifu kwa rais.Lakini baadae mapendekezo hayo yatabidi yaidhinishwe kwa kura ya maoni ya wananchi.

Rais Hugo Chavez amewaambia wabunge “mageuzi hayo ya katiba yatakomesha mamlaka ya dola moja kudhibiti mafuta na kuhitimisha mfumo wa zamani wa kibepari katika biashara ya mafuta na kuchipuka hatimae dola mpya.”

Akiongoza nchi ya tano miongoni mwa nchi zinazosafirisha mafuta kwa wingi ulimwenguni,Hugo Chavez amedhamiria kubuni utaratibu mpya wa kiuchumi na kijamii ambao mwenyewe anauita “Ujamaa wa mafuta”.

Hugo Chavez ni mkosoaji mkubwa wa siasa za Marekani,na viongozi wa mjini Washington kwa upande wao wanamuangalia kama chanzo cha machafuko katika eneo la Latin America,seuze tena Hugo Chavez hafichi usuhuba wake na Cuba na Iran.