1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Huenda tarehe ya mkutano wa amani Syria ikasogezwa nyuma

21 Januari 2016

Mazungumzo ya amani baina ya serikali ya Syria na makundi ya upinzani yaliyotarajiwa kufanyika tarehe 25 Januari yanaweza kusogezwa nyuma, amesema mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria Staffan de Mistura.

https://p.dw.com/p/1HhXM
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria, Staffan de Mistura
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria, Staffan de MisturaPicha: picture-alliance/AA

Hayo Staffan de Mistura ameyasema mjini Davos, katika mahojiano na kituo cha televisheni cha kimarekani CNN, saa chache baada ya mkutano kati ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov mjini Zurich, ambao haukuonyesha dalili ya kuafikiana juu ya orodha ya makundi ya waasi yatakayoshiriki kwenye mazungumzo hayo yanayoandaliwa na jumuiya ya kimataifa.

Kabla ya hapo baraza la upinzani linaloungwa mkono na Saudi Arabia, lilikuwa limesema bayana kwamba halitashiriki katika mazungumzo na serikali ya Syria, ikiwa kutakuwa na upande mwingine utakaoletwa katika mazungumzo hayo. Kwa kauli hiyo baraza hilo lilimaanisha makundi mengine ya waasi ambayo Urusi inataka yashirikishwe.

Hata hivyo, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi, amesisitiza kuwa hakuna mpango wa kuyasogeza mazungumzo hayo hadi mwezi ujao.

''Hakuna wazo la aina yoyote la kubadilisha kuanza kwa mazungumzo hayo kutoka Januari kwenda Februari. Huo ndio msimamo wa Urusi kama ulivyo wa Marekani. Tunatumai kwamba mazungumzo hayo ya amani yataanza baadaye mwezi huu'. Amesema Lavrov.

Waziri wa Mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov, na mwenzake wa Marekani John Kerry
Waziri wa Mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov, na mwenzake wa Marekani John KerryPicha: Getty Images/AFP/J. Martin

Tarehe nyingine haijaamuliwa

Tarehe kadhaa za kuanzisha mazungumzo hayo zimefikiriwa, lakini kwa mujibu wa mjumbe wa Umoja wa Mataifa, Staffan de Mistura, jukumu la kuamuwa ni la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani John Kirby amezungumzia umuhimu wa kuendeleza mchakato kuelekea suluhisho la kisiasa kwa mzozo wa Syria, akisema kwa upande wao bado wangependa mazungumzo hayo yaanze tarehe 25. Hata hivyo amesema ikiwa yatacheleweshwa kwa siku mbili au tatu, hali hiyo haitaashiria ''mwisho wa dunia''.

Hapo jana Umoja wa Mataifa ulisema hauwezi kutuma barua za mwaliko kwa makundi yanayotarajiwa kushiriki, kwa sababa wadau wawili muhimu, Urusi na Marekani, bado hawajakubaliana kuhusu makundi ya upinzani yatakayoalikwa.

Umma wa dunia waombwa kuweka shinikizo

Huku hayo yakijiri, mashirika yapatayo 100 yanayojumuisha yale ya Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya msaada, yametoa wito kwa umma wa dunia nzima kuweka shinikizo ili mzozo wa Syria unaokaribia kuingia mwaka wa sita sasa, ukomeshwe. Mashirika hayo yamesema yanatoa wito huo kwa ajili ya mamilioni ya wasyria wasio na hatia wanaoendelea kuteseka, na mamilioni wengine ambao wataanza kuteseka ikiwa suluhisho halitapatikana sasa.

Vita vya miaka zaidi ya minne vimeuwa watu wengi nchini Syria na kuharibu miundombinu
Vita vya miaka zaidi ya minne vimeuwa watu wengi nchini Syria na kuharibu miundombinuPicha: Getty Images/AFP/Y. Karwashan

Tangu kuanza kwa mzozo huo mwezi Machi mwaka 2011, watu zaidi ya 260,000 wamekwishapoteza maisha, na wengine milioni 13.5 wamekuwa wakimbizi ndani na nje ya Syria. Hizo sio takwimu rahisi ''amelalamika Mkuu mpya wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia Wakimbizi, UNHCR Filippo Grandi, mmoja wa waandalizi wa wito huo.

Ama kuhusu hali ya vita nchini Syria, mkutano wa nchi za Magharibi zinazochangia katika operesheni inayoongozwa na Marekani dhidi ya Kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS, umefikia azimio la kuzidisha shinikizo dhidi ya kundi hilo, hususan kwa kuzivunja ngome zake muhimu katika miji ya Mosul nchini Iraq, na Raqqa nchini Syria.

Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre/afpe

Mhariri:Iddi Ssessanga