1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW yatahadharisha Kenya

8 Februari 2013

Ripoti ya Human Rights Watch imesema serikali ya Kenya haikufanya vya kutosha katika ahadi yake ya kufanya mabadiliko na kushindwa kukabiliana na vitendo vinavyoendea vya ukiukwaji wa haki za binaadamu

https://p.dw.com/p/17ahk
Human Rights Watch Logo
Nembo ya Human Rights Watch

Hali hiyo inaelezwa kusababisha wasiwasi mkubwa kwa raia wa taifa hilo kuelekea uchaguzi mkuu wa Machi 4. Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa leo, Human Rights Watch imeitaka serikali ya Kenya kuchukua hatua za haraka, zikiwemo kuwakamata, kuwafikisha katika mikono ya sheria wale wote waliohusika moja kwa moja au kupanga vurugu, kusaidia kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uhuru, amani na haki.

Ripoti hii yenye kurasa 58 iliyopewa jina la "Vurugu za Kisiasa na Uchaguzi wa 2013 wa Kenya" imeonesha ishara ya kutokea vurugu pale ambapo serikali ya taifa hilo itashindwa kufanya mabadiliko kadhaa yanayohitajika kwa wakati huu.

Tayari mpaka sasa kwa mwaka 2012 na mwanzoni mwa mwaka 2012 vurugu katika jamiii miongoni mwa wakenya zinadaiwa kugharimu maisha ya watu zaidi ya 477 na wengine 118,000 kuachwa bila ya makazi. Matukio mengi yaliyosababisha vifo hivyo yanatajwa kusababishwa na mbinu chafu za wanasiasa katika maeneo husika kwa lengo la kujipatia uungwaji mkono wa kisiasa.

In this photo taken Thursday, Sept. 13, 2012 and made available Friday, Sept. 14, 2012, a man picks up belongings from the smoldering remains of a house in the village of Shirikisho, after it was attacked in the Tana River delta of southeastern Kenya. Kenyan authorities should expand investigations into the alleged roles of four politicians in clashes in the country's southeast which killed 110 people in three weeks, an international human rights group said Thursday. (Foto:AP/dapd)
Matokeo ya vurugu katika neo la Tana River, KenyaPicha: dapd

Daniel Bekele ambaye ni Mkurugenzi wa Human Rights Watch katika kanda ya Afrika amesema serikali imeshindwa kukabiliana na kiini cha vurugu hizo ambazo vuguvugu lake lilianza tangu uchaguzi wa vyama vingi wa 1992. Na hasa kuzingatia vitendo vya kinyama vya baada ya uchaguzi wa 2007-2008 kwa hivyo hatua za dharura zinahitajika kuwalinda raia wa Kenya.

Baada ya uchaguzi huo vurugu za kikabila zilizojumuisha pia jeshi la polisi zilizuka na kusababisha watu 1,300 kuuwawa na wengine 650,000 kuachwa bila ya makazi. Mapema 2012 mwendesha mashitaka wa serikali alifungua kiasi cha majarada 5,000 lakini mpaka sasa watu 14 ndio waliokutwa na hatia za vurugu za uchaguzi ule ambao ulifanyika miaka mitano iliyopita.

Uchaguzi wa Machi, utakuwa uchaguzi wa kwanza unaofanyika chini ya katiba mpya ya Kenya ambayo ilipitishwa 2010. Shabaha ikiwa ni kuwaleta pamoja raia wa taifa hilo. Wapiga kura watachagua rais wa taifa hilo pamoja na nafasi nyingine katika majimbo mapya 47 ya uchaguzi yaliyoundwa.

Ripoti hii ya Human Rights Watch imetayarishwa kwa kuwahoji watu 225 katika maeneo ya Kati nchini Kenya, Pwani, Mashariki, Kaskazini Mashariki, Nyanza na Bonde la Ufa. Lakini viashiria vya viwango vya hatari katika maeno yote hayo vinatofautiani.

Mwandishi: Sudi Mnette HRW
Mhariri: Josephat Charo