1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW yaishtumu serikali ya Uganda kwa ukandamizaji

Admin.WagnerD2 Machi 2016

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch-HRW limesema serikali ya Uganda inatoa vitisho dhidi ya vyombo vya habari na wanaharakati, katika juhudi za kuwanyamazisha kabla ya uchaguzi mkuu.

https://p.dw.com/p/1HbDW
Rais Yoweri Museveni
Rais Yoweri MuseveniPicha: Getty Images/AFP/D. Hayduk

Katika ripoti yake iliyotolewa leo na iliyopewa kichwa cha habari: ''Kutotoa Taarifa kwa Wananchi'', shirika la Human Rights Watch limesema waandishi wa habari wamesimamishwa kazi kutokana na shinikizo la serikali na vituo vya redio vimekuwa vikitishiwa kutofanya vipindi na wanachama wa upinzani kama wageni au kama wachambuzi wanaoelezea maoni yao katika kukikosoa chama tawala. Hali hiyo imeathiri vibaya uhuru wa kujieleza.

Ripoti hiyo yenye kurasa 48 imesema wakati waandishi wa habari wa magazeti wanaofanya kazi kwa lugha ya Kiingereza wakiwa wana uhuru kidogo, waandishi wa habari wa redio hasa wanaotumia lugha za makabila, ambao wasikilizaji wake wengi wako katika maeneo ya vijijini, wamekuwa wakinyanyaswa na kupewa vitisho kutoka kwa serikali au maafisa wa chama tawala.

Wagombea saba watashindana na Rais Yoweri Museveni ambaye ameitawala Uganda kwa miaka 30 katika uchaguzi wa Februari 18, na kuna hofu kwamba ghasia zinaweza kutawala katika kampeni. Washindani wakuu wa Museveni ni Waziri Mkuu wa zamani, Amama Mbabazi na afisa wa zamani wa jeshi, Kizza Besigye.

Amama Mbabazi
Amama MbabaziPicha: picture-alliance/AP Photo/A. Zemlianichenko

Mtafiti Mwandamizi kuhusu masuala ya Afrika wa shirika hilo lenye makao yake nchini Marekani, Maria Burnett amesema uchaguzi wa haki unahitaji uwanja sawa ambapo wagombea wote wanaweza kufanya kampeni zao kwa uhuru na wapiga kura wanaweza kufanya maamuzi sahihi.

Burnett anauliza ni vipi Uganda inaweza kufanya uchaguzi wa haki kama vyombo vya habari na mashirika binafsi hayawezi kukikosoa chama tawala au viongozi wa serikali bila ya woga wowote?

Mwandishi wa habari azungumza

Akizungumza na DW, Sadabu Kaaya, mwandishi wa habari wa gazeti la 'The Observer' nchini Uganda ambaye amewahi kupokea vitisho anasema waandishi wa habari wanaoripoti taarifa za wapinzani wamekuwa wakibugudhiwa na kunyanyaswa.

''Visa hivyo ni vya kweli. Kwa mfano mimi nimepoteza vifaa vyangu vya kazi. Baadhi ya waandishi tunaotumia mitandao ya kijamii tumekuwa tukivamiwa hasa wale tunaoripoti kuhusu mikutano ya wapinzani,'' alisema Kaaya.

Mwandishi huyo aliendelea kufafanua kwamba, ''Jana tu waandishi wa habari waliokuwa wanaripoti mkutano wa Dr. Kizza Besigye, walivamiwa na polisi wa Moroto na kunyang'anywa kamera zao na kisha kuvunjwa. Vitendo hivi vipo.''

Kizza Besigye
Kizza BesigyePicha: AP

HRW imesema serikali ya Uganda na maafisa wa chama tawala pia wamekuwa wakiyabinya mashirika ya haki za binaadamu likiwemo shirika la kutoa elimu kwa wapiga kura, ambalo limetembelewa mara kadhaa na polisi na kuzuiwa kufanya mikutano yake.

Msemaji wa serikali, Shaban Bantariza amekanusha tuhuma hizo akisema wamekuwa wakifanya chaguzi huru na za haki kwa miaka yote na wataendelea kufanya hivyo. Anasema kama watu hawakupata taarifa sahihi, mawaziri wengi na wabunge wasingepoteza viti vyao katika uchaguzi wa awali wa hivi karibuni katika chama tawala.

Shirika hilo limesema ripoti hiyo imezingatia mahojiano yaliyofanywa kwa zaidi ya waandishi wa habari 170, wanaharakati, wanachama wa vyama vya siasa pamoja na mashuhuda.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/HRW,DPA,AFPE
Mhariri: Mohammed Khelef