1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HONIARA: Watu takriban 15 wauwawa kwenye tsunami

2 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CCD2

Watu takriban 15 wameuwawa kufuatia tsunami katika visiwa vya Solomon iliyosababishwa na tetemeko kubwa la ardhi lililotokea katika eneo la kusini mwa bahari ya Pacific.

Visiwa vya Gizo, Lefung na Taro vimeathiriwa zaidi na mawimbi hayo ya tsunami. Waziri mkuu wa kisiwa cha Gizo, Alex Lokopio, amesema nyumba zote katika mwambao wa kisiwa hicho zimeharibiwa.

´Mtetemeko mkubwa wa ardhi umetokea katika kisiwa cha Gizo na kusababisha mawimbi makubwa ya tsunami. Maji yakaja juu na kuharibu nyumba zote katika eneo la mwambao la Gizo. Nadhani mawimbi yalikuwa na urefu zaidi ya mita tano na maji yaliposambaa, watu watatu wakapatikana wamekufa katika maeneo tofauti.´

Afisa mmoja katika visiwa vya Solomon amesema vijiji viwili vimefunikwa kabisa na maji.

´Vijiji viwili vimeripotiwa kuharibiwa kabisa. Pia katika kisiwa kilicho karibu kiitwacho Mono, tumepata taarifa zinazosema watu wanne hawajulikani waliko kufuatia tsunami. Vilevile tumepata ripoti ambazo hazijathibitishwa kwamba tsunami imepiga mjini humo lakini hakuna taarifa za walioathirika kwa wakati huu.´

Tatizo la mawasiliano katika visiwa vya Solomon linaifanya kazi ya kutathmini uharibifu uliosababishwa na tsunami hiyo kuwa ngumu.