1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hollande ashinda duru ya kwanza ya uchaguzi Ufaransa

23 Aprili 2012

Francois Hollande kutoka chama cha Kisoshalisti nchini Ufaransa ambaye anataka kuwahudumia vizuri zaidi watu masikini na wale wasiokuwa na ajira anaiingia duru ya pili ya uchaguzi wa rais dhidi ya Rais Nicolas Sarkozy.

https://p.dw.com/p/14jVC
Francois Hollande, Socialist Party candidate for the 2012 French presidential election, waves to supporters in Tulle before his speech, after early results in the first round vote of the 2012 French presidential election // Eingestellt von wa
Frankreich / Präsidentenwahl / HollandePicha: Reuters

Uchaguzi huu unaweza kubadili ramani ya kisiasa na kiuchumi barani Ulaya.Katika uchaguzi huo uliofanyika Jumapili (22.04.2012) nchini Ufaransa hakuweza kupatikana mshindi wa moja kwa moja na hiyo kulazimika kufanyika kwa duru ya pili ya uchaguzi hapo tarehe 6 Mei.

Huyo ni Francois Hollande ambaye anaingia duru ya pili ya uchaguzi wa rais wa Ufaransa akiwa anaongoza katika kura kwa kumpita chupuchupu mhafidhina Sarkozy alienadi kampeni yake kwa kutumia ilani ya kudhibiti uhamiaji katika dura ya kwanza ya uchaguzi huo.

Mshangao mkubwa kabisa wa uchaguzi huo ni kwamba katika kila wapiga kura watano mmoja amemchaguwa mgombea wa sera kali za mrengo wa kulia Marine Le Pen na kumfanya ashike nafasi ya tatu na pia nafasi ya kuwa na usemi katika siasa za Ufaransa kwa kutumia ilani ya kupinga uhamiaji ambayo inawalenga mamilioni ya Waislamu wa Ufaransa.

Rais anayetetea wadhifa wake Nicolas Sarkozy
Rais anayetetea wadhifa wake Nicolas SarkozyPicha: Reuters

Ikiwa asilimia 93 ya kura zikiwa tayari zimekwishahesabiwa Hollande amejipatia asilimia 28.4 ya kura,Sarkozy amejipatia asilimia 27 na Le Pen ambaye ameshika nafasi ya tatu amejipatia asilimia 18.3 ya kura ,ambayo ni matokeo mazuri kabisa kuwahi kushuhudiwa  na chama cha National Front kilichoasisiwa na baba yake Jean- Marie Le Pen. Idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura ni kubwa ambapo imepindukia asilimia 80 katika uchaguzi huo wa urais uliokuwa na wagombea 10.

Hollande mwenye umri wa miaka 57 ambaye aliyatia  wasi wasi masoko ya fedha kutokana na ahadi zake za kuongeza matumizi ya serikali aliapa kupunguza deni kubwa la Ufaransa,kukuuza uchumi wa nchi hiyo  na kuwaunganisha Wafaransa kufuatia kipindi kigumu chini ya muhula wa kwanza wa Sarkozy.

Sarkozy mwenyewe akizungunmza katika makao makuu ya kampeni yake ya Left Bank mjini Paris amesema anatambuwa wasi wasi wa wapiga kura kuhusu ajira na uhamiaji na wasi wasi wa wazalendo wa nchi hiyo kutaka kutunza utamaduni wao.

Kampeni kwa ajili ya duru ya pili ya uchaguzi huo tayari zimeanza leo ambazo sasa zitalenga katika kuziyumbisha kura za Le Pen ambapo yeye mwenyewe tayari amesema kwamba hawatowapa maelekezo wafuasi wake. Sarkozy alikwapua baadhi ya mada za kampeni dhidi ya uhamiaji na utambulisho wa kitaifa zilizokuwa zikipigiwa debe na mama huyo ambaye mara kwa mara alikuwa akimshutumu Sarkozy na kusema kwamba alikuwa hana fursa ya kushinda katika uchaguzi huo.

Mgombea wa urais wa sera kali za mrengo wa kulia Le Pen
Mgombea wa urais wa sera kali za mrengo wa kulia Le PenPicha: dapd

Chochote kile kitakachotokea katika uongozi wa Ufransa kitaathiri Umoja wote wa Ulaya wenye nchi wanachama 27. Ufaransa ni mojawapo ya mataifa sita ambapo katika miaka ya 1950 yaliasisi chombo kilichoutangulia umoja huo na ni mojawapo ya nchi zenye nguvu kubwa za kiuchumi katika kanda inayotumia sarafu ya euro barani Ulaya ikitanguliwa na Ujerumani.

Suala la sera za kigeni takriban halikutimiza dhima yoyote ile katika kampeni hii lakini litakuwa na dhima kubwa katika kazi ya rais mpya. Wagombea wa misimamo mbali mbali wanataka kurudishwa nyumbani kwa wanajeshi 3,600 wa Ufaransa walioko kwenye kikosi cha kimataifa kinachoongozwa na Jumuiya ya Kujihami ya NATO nchini Afghanistan na Hollande aliahidi kuondowa wanajeshi hao haraka ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Sarkozy amesema anataka kuwepo kwa midahalo mitatu kabla ya duru ya pili ya uchaguzi hapo tarehe 6 mwezi wa Mei juu ya masuala ya uchumi,jamii na uhusiano wa kimataifa.Lakini Hollande ametupilia mbali takwa hilo kwa kusema kwamba mdahalo mmoja uliopangwa hapo awali unatosha. 

Mwandishi:Mohamed Dahman/AP

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman