1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hollande aapishwa rais mpya wa Ufaransa

15 Mei 2012

Msoshialisti Francois Hollande ameapishwa rasmi kama rais wa saba wa Jamhuri ya Tano ya Ufaransa baada ya sherehe za kukabidhiwa hatamu za uongozi na mtangulizi wake, Nicolas Sarkozy.

https://p.dw.com/p/14vig
Nicolas Sarkozy (kushoto) na rais mpya Francois HollandePicha: Reuters

Kama ilivyo desturi za kukabidhiana madaraka nchini Ufaransa, rais anayemaliza wadhifa wake amempokea rais mpya alipoingia katika kasri la Elysée. Baada ya kupeana mikono, wakakutana kwa mazungumzo ya siri ya dakika 30 ili kumwezesha rais wa zamani kumuarifu rais mpya kuhusu mada muhimu ambazo hazistahiki kujulikana hadharani, pamoja na kumpatia nambari za siri za mradi wa kinyuklia wa Ufaransa.  Baada ya sherehe hizo kumalizika, rais wa zamani huenda zake. Na hivyo hivyo ndivyo ilivyokuwa kati ya Nicolas Sarkozy na Francois Hollande.

Kipya safari hii Hollande aliyeapa kuwa "rais wa kawaida" hakufuatana na watoto wake katika sherehe za kuapishwa huko Elysée, kinyume na vile alivyofanya mtangulizi wake miaka mitano iliyopita.

Akihutubia katika kasri la Elysée, Hollande amesisitiza azma yake ya kuiongoza Ufaransa katika njia ya haki na kuifungulia Ulaya njia mpya.

Francois Hollande Frankreich Paris
Francois Hollande apeana mikono na wakuu wa chama cha kisoshialistiPicha: AP

Francois Hollande ametoa mwito wa kuwa na umoja na kusema Wafaransa wanabidi wajiamini. "Ufaransa ni dola kuu ambayo daima imekuwa ikifanikiwa katika majukumu yake." Ameahidi kuhakikisha maisha ya usawa kwa Wafaransa wote kwa kuzingatia maadili, hadhi na muruwa wa Jamhuri ya Ufaransa.

Leo mchana rais huyo mpya wa Ufaransa anatazamiwa kufichua jina la waziri wake mkuu kabla ya kuondoka jioni hii kuelekea Berlin kwa ajili ya mazungumzo yake ya kwanza pamoja na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel.

Kombibild Francois Hollande Angela Merkel
Francois Hollande na kansela Angela MerkelPicha: picture-alliance/dpa

Hata kabla ya Hollande kuwasili Berlin, Kansela Merkel alisema atampokea kwa mikono mikunjufu. "Tutashirikiana na baadaye tutaona. Kusaka msimamo wa aina moja barani Ulaya haijawahi kuwa kazi rahisi, lakini daima tumekuwa tukifanikiwa."

Mazungumzo kati ya Kansela Merkel na mgeni wake wa kutoka Paris yanagubikwa na mgogoro wa Ugiriki na msimamo tofauti kuhusu mkataba wa Ulaya wa kuleta utulivu wa bajeti ambao Hollande anataka kwa kila hali ufanyiwe marekebisho na kuingizwa kifungu kinachohusu mikakati ya kuinua uchumi..

Kwa mujibu wa viongozi wa serikali mjini Berlin, mazungumzo ya leo kati ya Angela Merkel na Francois Hollande hayajalengwa kupitisha maamuzi, bali kujuana.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AFP
Mhariri: MIraji Othman