1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

"Hofu haiwezi kutatua matatizo ya dunia hii

Ripoti ya mwaka ya shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu, Amnesty International, inaonya kuwa vita dhidi ya ugaidi vinaigawa dunia. Matokeo ya uchunguzi wa wanaharakati hao wa haki za binadamu pia ni mwito mkali unaowalenga viongozi wa nchi za kiviwanda za G8 watakaokutana wiki mbili zijazo hapa nchini Ujerumani. Haya anayasema Ulrike Mast-Kirschning katika uchambuzi wake.

default

Yule aliyeamini kuwa kumalizika kwa mvutano kati ya nchi za Mashariki na za Magharibi katika vita baridi kutaleta amani na uhuru duniani, basi lazima atambue kuwa matumaini haya hayatekelezi. Katika miaka 15 iliyopita kumetokea mambo mengi katika dunia hii, ambayo yameathiri amani na uhuru. Hasa itikadi za kiliberali ambazo zinasema fedha na mamlaka ya soko zitaleta maendeleo, zilivunja mioyo ya watu wengi maskini.

Ulimwenguni kuna mgawanyiko kati ya wachache walio matajiri na maskini wengi. Wakijaribu kuimarisha mamlaka yao, makundi ya kiuchumi yanayozidi kupata nguvu na serikali ambazo mamlaka yake yanapungua, zinatumia hofu kama mkakati wa mamlaka. Zinachochea hofu dhidi ya uhamiaji na wageni, dhidi ya ugaidi, maoni tofauti, watu wenye dini tofauti au hofu ya kutenganishwa kutoka kwenye jumuiya ya kimataifa.

Ripoti ya shirika la Amnesty International haijawahi kudokeza wazi kama ilivyofanya safari hii, jinsi ukiukaji wa haki za binadamu, pia haki za kiuchumi na za kijamii, unavyozidisha mizozo na vita, vile vile jinsi hofu inavyochochewa na wanasiasa, inavyoleta na ushawishi mkubwa katika jamii zetu.

Hofu inasababisha hisia za wasiwasi, na pia inasababisha ubaguzi dhidi ya makabila ya walio wachache. Katika ripoti yake, Amnesty International inatoa mifano mingi kutoka mabara yote. Hofu dhidi ya kutoa maoni huru ilisababisha maandamano na ghasia juu ya kartooni iliyomthihaki mtume Mohammed. Nchini Marekani, ripoti kuhusu jela ya Guatanamo ambazo hazikutakiwa na serikali zilipigwa marufuku kuchapishwa kwa muda mrefu.

Katika nchi kadhaa za Afrika Kaskazini na Mashariki ya Kati kunatumika taratibu za zamani za kukandamiza maoni ya watu na haki za kuandamana. Nchini Urusi, waandishi wa habari na watetezi wa haki za binadamu wanahofia maisha yao.

Pia kuna hofu dhidi ya uhuru wa wanawake ambayo haichochewi nchini Iran tu, bali pia katika nchi kama vile Afghanistan, Pakistan au Sudan, wanaharakati wanaopiga vita ubaguzi dhidi ya wanawake wanapata shida. Hali hii ya kuzidisha hofu kati ya raia wa kawaida inakuwa mbaya zaidi kutokana na hatua kali za kuhakikisha usalama kwenye mikutano ya kilele ya serikali kama zilivyochukuliwa hivi majuzi hapa nchini Ujerumani, hata ikiwa wasiwasi juu ya kufanyika mashambulio ni wa halali.

Lakini hofu haitaweza kutatua matatizo magumu ya enzi hii ya utandawazi. Badala yake, shirika la Amnesty International linadai kuwepo kwa mkakati endelevu, mbinu ya kuleta matumaini ambayo yataweza kuimarisha demokrasia na kuhakikisha haki za binadamu zinatekelezwa.

Hivi karibuni kutakuwa na fursa nzuri ya kuujibu mwito wa shirika hilo la kutetea haki za binadamu na kutimiza madai yake, yaani pale viongozi wa nchi muhimu za G8 watakapokutana mjini Heiligendamm, Ujerumani. Inawabidi wabadilishe mwenendo wa kisiasa kuelekea njia mwafaka. Wao ndio wana mamlaka ya kuupa kipaumbele uhuru, ikiwa ni uhuru wa kusema au wa kuamini.

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com